Msimamizi wa Kitengo cha Mita Mkoa wa Arusha, Charles John.
NA MWANDISHI WETU-ARUSHA
SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO), limewataka wananchi wa mikoa
ya Kaskazini kujiepusha na vitendo vya kuchakachua Mita za umeme kwani
atakayekutwa ametenda kosa hilo atafungwa jela miaka mitano.
Wizi huo wa umeme unayofanywa na baadhi ya wateja wasio
waaminifu umetajwa kuendelea kupoteza mapato yanayopaswa kukusanywa na shirika
hilo kutokana na kutumia umeme usiolipiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Nane
Nane ya Kilimo na Mifugo Kanda ya Kaskazini Njiro mjini hapa na Msimamizi wa
Kitengo cha Mita Mkoa wa Arusha, Charles John.
Alisema vitendo vya uchakachuaji wa Mita za umeme vinavyolenga
kupata huduma bure bila kulipia gharama yeyote ni uhujumu uchumi kwa taifa
havifai kufumbiwa macho.
“Niombe wananchi wawe wazalendo na nchi yao, wawafichue
wanaoharibu Mita za umeme. Lakini pia wakumbeke vitendo hivyo ni hatari kwa
usalama wa maisha yao pindi wanapofanya mchezo huo hatari,” alisema John na
kuongeza:
“Tupo hapa kwenye banda letu ndani ya viwanja vya maonyesho ya
Nane Nane Njiro tukishiriki kutoa elimu pana kwa wananchi juu ya matumizi
sahihi ya umeme ikiwamo kuacha vitendo vya wizi,” alisema.
Alisema mtu yeyote atakayekamatwa katika oparesheni zinaoendelea
kufanywa na maofisa wa Shirika hilo atafikiwa katika vyombo vya sheria na
kukabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini kubwa.
“Tunaendelea na oparesheni maeneo mbalimbali ili kuwakamata wale
wote wasiowaaminifu ambao kila wakati wamekuwa wakihujumu miundombinu ya
shirika na hivyo kulisababishia hasara,”
“Mbali na elimu hiyo tunawapatia pia elimu ya namna gani
wanaweza kutumia Mita zetu ambazo ni tofauti zinatumia Remote hivyo bila
kuwapatia elimu hii inaweza kuwa taabu kwao kuzitumia,” alisema John
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Said
Mremi awaliwahimiza wananchi kutembelea kwenye banda hilo ili waweze kupata
maelezo yote kuhusu namna bora ya kuunganishiwa umeme.
“Wananchi wakifike viwanja hivi waje hapa TANESCO kwani bado
elimu inahitajika kwao wajue hatua wanazotakiwa kufuata kabla ya kufungiwa
umeme, wenye umeme wakipita watapata elimu pia,” alisema Mremi.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kwapole wilayani Arumeru mkoani Arusha
Lazaro Mbisse alisema, amefanikiwa kupata maelezo ya kutosha kabla hajaingiza
umeme kwenye nyumba yake mpya.
“Huko mitaani wamejaa mafundi vishoka wanatapeli wananachi
wakiwaaminisha wao ndio wafanyakazi wa TANESCO kumbe si kweli, nimefika hapa
nimepewa maelezo kamili ya kufunga umeme ndani kwangu.
No comments:
Post a Comment