Ikulu,
Dar es Salaam.
Kampuni ya uchimbaji madini ya
Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana
kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.
Makubaliano hayo yametiwa
saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Mhe. Rais Dkt.
John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabuni na Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw.Faisal Juma.
Akizungumza mara baada ya
kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa
kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi
amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo
iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.
Amesema fidia hiyo inatakiwa
kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia
leo na haitahusisha Kodi. Pia Kampuni
hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali
na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.
Pia Serikali
imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya
sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio
wanaoruhusiwa kuchimba madini ya Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo
huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.
Aidha Prof. Kabudi amesema
kuhusu wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani utaratibu mpya unawekwa lengo kubwa ikiwa ni
kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inalenga madini ya vito kuwa
mikononi mwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuunda
kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo
wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na
malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.
Amesema Tanzanite One
itahakikisha inafuata taratibu zote za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo
la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu
wa sheria uliofanywa na kampuni hiyo hautajirudia tena.
"Sisi kama Tanzanite One
tunaihakikishia Serikali kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni
tutahakikisha tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana
na imani aliyotuonyesha Mhe. Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya
kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda"
amesema Faisal.
Faisal amesema Tanzanite One
itahakikisha haitafanya makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa
kampuni nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha
Watanzania.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi Mawasiliano
ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam
16 Mei, 2018
No comments:
Post a Comment