Monday, April 30, 2018

TANAPA YACHANGIA MILIONI 50 UJENZI SEKONDARI YA UFUNDI SIMIYU



Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi akimkabidhi mfano wa Hundi ya Sh milioni 50, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka, kushoto ni Meneja Uhusiano wa TANAPA Paschal Shelutete na kulia mwisho ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga. 

-ARUSHA 

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TÀNAPA), limekabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka hundi ya Sh milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Ufundi Simiyu.

Akikabidhi mchango huo jana mjini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Allan Kijazi alisema fedha hizo wamezitoa ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina yao na wananchi.

Kijazi alisema shughuli za uhifadhi na utalii zinazosimamiwa na Shirika hilo haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi wanaowazunguka.

"Tusimamia Hifadhi za Taifa kwenye mikoa tisa, pote huko tumepakana na wananchi, kwa Mkoa wa Simiyu ni wadau muhimu eneo la Hifadhi ya Serengeti,"

Wamekuwa wakisaidia katika kukabiliana na vitendo vya ujangiri ikiwamo kuendelea kuhifadhi maeneo yaliyopo mipakani mwao," alisema Kijazi.

Alisema kutokana na mkakati waliouanzisha  mkoa huo wa  ujenzi wa shule tatu za vipaji maalumu, TANAPA imeona jambo hilo ni umuhimu kwa ustawi wa taifa na kizazi kijacho. 

"Uongozi kupitia kwa Mkuu wa Mkoa, Mtaka wanatafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kukamilisha ndoto hizo, sisi TANAPA tumechangia Sh milioni 50 kwa kuanzia," alisema Kijazi. 

Kwa upande wake RC Mtaka akizungumza fedha hizo alisema, kwa kuanzia zitaanza na ujenzi wa madarasa yote ya Sekondari ya Ufundi Simiyu, na baada kulingana na upatikanaji wa fedha wataelekea majengo mengine. 

"Tunajenga shule tatu za vipaji maalumu tutaanza na Sekondari ya Ufundi, Sekondari ya Wasichana na kisha Wavulana mpaka tunakamilisha mradi huu wote tutakuwa tumetumia zaidi ya Sh bilioni 1.1," alisema Mtaka na kuongeza:
"Kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo mkoani kwake kutasaidia watoto wa Kitanzania kuwa na msingi mzuri wa kuingia kidato cha Tano, lakini pia kutoka nafasi kwa watoto wa Simiyu kuwa na maadili mazuri," alisema. 

Alisema shule hizo zote zitakuwa na majengo yote muhimu ikiwamo maktaba, jengo la chakula, nyumba za walimu, mabweni, majengo ya utawala. 

Alisema tayari wananchi mkoani wameanza kujitoa kwa shughuli za uchimbaji wa misingi kusomba mawe na shughuli nyingine ambapo wanatarajia ujenzi huo kufanywa na mafundi wa kawaida. 

"Tutatumia wataalamu wetu wa Halmashauri na Mkoa kuwaelekeza mafundi na vibarua, ili kuhakikisha tunakuwa na majengo imara na yenye viwango. 

"Fedha tulizopewa TANAPA zinatosha kabisa kuanza na ujenzi wa majengo ya shule ya Ufundi,  niwahakikishie tumejipanga kuhakikisha kila shilingi inatumika vyema, gharama yote ya Shule ya Ufundi mpaka kukamilika ni Sh milioni 350," alisema Mtaka. 

Katika makabidhiano ya hundi hiyo yaliyofanyika Makao Makuu ya TANAPA Arusha, Mtaka aliongozana pia na Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga. 

mwisho. 

No comments:

Post a Comment