Tuesday, January 16, 2018

SHELUTETE: MAAFISA HABARI, MAWASILIANO, UHUSIANO, ITIFAKI 300 KUTOKA SERIKALINI KUKUTANA JIJINI ARUSHA


Mwenyekiti wa TAGCO Paschal Shelutete akizungumza na vyombo vya habari


CHAMA cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO), kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kimeandaa kikao kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki wa Wizara, Idara zinazojitegema, Taasisi, na Wakala wa Serikali (MDAs) kitakachofanyika mkoani Arusha kuanzia Machi 12 hadi 16 2018. Jumla ya maofisa 300 wanatarajiwa kushiriki katika kikao kazi hicho.


Taarifa kwa Vyombo vya habari iliyosainiwa na Mwenyekiti Shelutete ilisema, kikao kazi hicho kinachoandaliwa ni cha 13 katika mfululizo wa vikao vinavyofanyika kila mwaka kwa lengo la kuwajengea washiriki uwezo wa namna ya kutangaza shughuli za serikali na kuhakikisha Idara/vitengo vya mawasiliano na Uhusiano serikalini vinaimarishwa ili kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano. 

Mwenyekiti wa TAGCO Paschal Shelutete akizungumza na vyombo vya habari

Katika kikao kazi hicho, jumla ya mada 14 zitawasilishwa na ambazo zitajikita zaidi kwenye masuala mbalimbali yahusuyo habari, mawasiliano na itifaki. Mada hizo zitawasilishwa na watalaamu watakaoleta uzoefu mpana katika mawasiliano. Pia, kutakuwapo mijadala na fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya Maafisa Mawasiliano na wadau wengine wa habari.

Maafisa Habari, Mawasiliano na Itifaki wanahimizwa kuthibitisha ushiriki wao kabla ya  Machi 7, Mwaka huu.


TGCO ni Chama kilichoanzishwa rasmi mwaka 2012 na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Kila mtumishi wa umma anayeshughulika na masuala ya habari na mawasiliano anapaswa kuwa mwanachama wa TGCO. 

No comments:

Post a Comment