SERIKALI imewataka wawekezaji wa viwanda vya mabomba ya
maji nchini, kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora wa kimataifa kwani
asilimia 75 ya Sh Trilioni 4.5 ya mradi wa maji unaotekelezwa nchi zima
inakwenda kwenye mabomba.
Agizo hilo kwa wenye viwanda nchini lilitolewa jana mjini hapa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Professa Kitila Mkumbo wakati
wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda cha Lodhia Plastic kilichopo mjini Arusha.
Mkurugenzi wa Lodhia Plastic Sailesh Pandit akielezea jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo.
Akizungumza baada ya kujionea uzalishaji wa mabomba ya
maji na Maabara ya kupima ubora na viwango vya mabomba kabla
hayajaingizwa sokoni Prof. Mkubo alisema, ameridhishwa na uwekezaji wa kiwanda
hicho.
Katika kutekeleza uchumi wa viwanda nchini, Prof. Mkumbo alisema
Wizara hiyo imejipanga kuhakikisha inachangia kwa kununua bidhaa hizo za
wawekezaji wa ndani hatua itakayoongeza mapato kwa serikali na kukuza ajira kwa
Watanzania.
“Tungependa kwa wakati huu tutumie viwanda vya ndani katika
kupata mabomba ya maji ili tuendeleze miradi ya maji.Lakini pia tuchangie uchumi
wa viwanda na kuongeza ajira Lodhia Plastic wameajiri watu 350,” alisema Prof.
Mkumbo na kuongeza:
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Mkumbo
“Kupitia kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
Arusha (AUWSA), natoa wito kadri iwezekanavyo tumieni mabomba yanayozalishwa na
viwanda vya ndani. Katika sekta ya maji tunaweza kusaidia agenda ya uchumi wa
viwanda kupitia miradi yetu.
“Kazi yetu kubwa sana kwenye miradi ya maji ni mabomba kwa sasa
tuna miradi ya maji nchi nzima inayofikia takribani Sh. Trilioni 4.5 na
asilimia 75 ya miradi hiyo ni mabomba,” alisema.
Aidha katika ziara hiyo Prof. Mkumbo alitoa tahadhari kwa wenye
viwanda hivyo kuhakikisha wanazalisha mabomba yenye viwango kwani katika suala
la ubora kutakuwa hakuna upendeleo.
“Lazima mjipange kushindana na lazima mtoe mabomba yenye viwango
vya kimataifa kwasababu miradi ya maji ni ghali sana,” alisema Katibu Mkuu
Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia Plastic Sailesh
Pandit alisema, kiwanda hicho kimefunga Maabara ya kisasa inayopima
mabomba kabla hayajaingizwa sokoni kwa wateja.
Kuhusu changamoto zinawazowakabili Pandit alisema, tatizo kubwa
walilonalo ni wakati wa kujaza Zabuni za kusambaza mabomba yao kwani moja ya
masharti wanayokumbana nayo ni kiwanda kuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 15 mpaka
20.
“Tatizo kubwa tulilonalo ukijaza Zabuni unatakiwa uwe na uzoezi
wa miaka 15 mpaka 20, hilo tumeshindwa kulielewa kwani sisi tumethibitishwa na
Shirika la Viwango (TBS) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).
“Lakini pia baadhi ya Wakandarasi waliopewa miradi ya maji
kuendelea kununua mabomba nje ya Arusha wakati hapa tuna viwanda vyenye ubora
unaotakiwa,” alisema Pandit.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akizungumza kwenye
ziara hiyo alisema, Serikali itaendelea kutumia viwanda vya ndani ili
waliojenga viwanda hivyo wawe na soko la uhakika.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo
“Kuna mradi wa maji wilayani Longido wa Sh Bilioni 16,
Mkandarasi alinunua mabomba kutoka Kenya, hii imewakatisha tamaa wenye viwanda
vya ndani, imepunguza mapato serikalini na ajira kwa Watanzania,” alisema
Gambo.
No comments:
Post a Comment