Monday, January 15, 2018

ASKOFU DK.STANLEY HOTAY: WAFUGAJI LITUNZENI BONDE LA NGORONGORO

ASKOFU wa Kanisa la Anglikani Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Dk. Stanley Hotay amewataka wafugaji wa kimaasai wilayani Ngorongoro kuhakikisha wanalitunza Bonde la Ngorongoro ili lizidi kuwaletea maendeleo wao na Watanzania.

Askofu Dk. Stanley Hotay 
Alitoa kauli hiyo juzi kijijini Kakesyo, Tarafa ya Ngorogoro wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Enyorata Ereko iliyojengwa na Mwinjilisti Jane Kim(Mama Maasai), raia wa Marekani mwenye asili ya Korea anayefanya kazi ya Ujilisti na kanisa hilo.


Mama Maasai alitembelea eneo hilo akiwa mtalii aliyekuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali ambapo kabla ya kurejea kwao aliahidi kurudi nchini kwa ajili ya kufanya kazi ya Mungu kwenye eneo hilo ikiwamo ujenzi wa makanisa na shule.

Askofu Dk. Hotay akijadiliana jambo na Muinjilist Jane Kim, katika yao ni Askofu Mstaafu Boniphace Kwangu

Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Jimbo hilo William Ole Nasha, Dk. Hotay alisema wafugaji wanapaswa kutambua kuwa wanaishi eneo nyeti linaloileta dunia, Tanzania.


Alisema kutokama na umuhimu wa Bonde la Ngorongoro, wafugaji wanaoendesha shughuli zao wanapaswa kulitunza bonde hilo kwa kupunguza mifugo yao na kuwekeza katika maeneo nje yatakayowawezesha kuendelea kujiingizia kipato zaidi.  

“Mmepewa eneo muhimu linaloileta dunia, Tanzania. Kama mngeamua kukata miti, kuharibu mazingira na kuua wanyamapori  basi haya mataifa tunayoyaona yakija kutembelea Bonde la Ngorongoro yasingeweza kuja,” alisema Dk. Hotay.

Moja ya Shule zilizojengwa kwa ufadhili wa Muinjilist Kim 

“Wafugaji mnaofuga ng’ombe wengi ni wasihi mkielimika basi tumieni ng’ombe hawa kwa faida. Kuliko wafe kwa hasara kwa kukosa malisho na kuwahudumia mkawauza kwa Sh 100,000 ni bora mkawabadilisha wakawa uchumi mwingine.

“Uzeni wakiwa katika soko la Sh Milioni 1 au zaidi,wekezeni kwingine huku mkiendelea kubakia na mifugo wachache mnaoweza kuwatunza. Niwasihi mliomo humu tusaidiane kulitunza Bonge la Ngorongoro,” alisema Askofu Dk. Hotay.

Kwa upande wake Naibu Mhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), Dk. Maurus Msuha akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, matokeo ya ujenzi wa majengo ya shule hiyo yametokana na rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo. 


“Ndugu zangu, kama tumemuelewa Baba Askofu Dk. Hotay amesema msikate tawi mlilokalia,” alisema Dk. Msuha.

Kuhusu kutumiwa majengo hayo aliwataka wazazi kuhakikisha wanapeleka watoto shule badala ya kuchuga mifugo na kujikuta madarasa yaliyojengwa kwa gharama yakikaa bila watoto.

Naye Naibu Waziri Nasha alimshukuru mfadhili huyo akisema, ilikuwa ndoto ya miaka mingi ya kuwa na shule kwenye eneo hilo kutokana na watoto wadogo kutembea umbali mrefu kwenda kusoma shule nyingine.

Naibu Waziri wa Elimu akizungumza

“Shule hii itasaidia kuokoa maisha ya watoto dhidi ya wanyama wakali, kukaa muda mwingine darasani tofauti na awali kutembea Kilomita 28 hivyo kujikuta wakiwahi kutoka dasarani ili kurudi nyumbani,” alisema Naibu Waziri Nasha.

Aidha mfadhili huyo alimshukuru Mungu kwa kupata fedha na kutimiza ahadi ya kujenga shule tatu zikiwamo Shule ya Msingi Loresho na Irkiporin zilizozinduliwa na Naibu Waziri Nasha na zote zimesajiliwa na kuanza kupokea wanafunzi.

Muinjilist Kim akiwahubiria wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro 


“Tumejenga majengo haya kwasababu Mungu anatupenda,sisi ni watoto wake namshukuru Mbunge Nasha na timu yake ikiwamo Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngrongoro kwa kutusaidia katika baadhi ya mambo,” alisema Kim.

No comments:

Post a Comment