Friday, November 3, 2017

MRADI WA MAJI WENYE THAMANI YA SH BILIONI 476 WASAINIWA ARUSHA

   Utiaji saini mradi mkubwa wa maji Arusha 
   Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe

-ARUSHA

UTAFITI wa Kampuni ya Kifaransa ya Egis Eau umebainisha maeneo manne yanayotajwa kuwa vyanzo pekee vya maji katika Jiji la Arusha na maeneo jirani kwa ajili ya kuchimbaji visima virefu vya maji.

Aidha, wakati utafiti ukija na matokeo hayo, vyanzo vya maji vilivyopo Bonde la Mto Pangani vinakabiliwa na changamoto ya madini ya Fluoride yaliyozidi kiwango cha Milgramu 4 kwa Lita ambayo si rafiki kwa afya za binadamu.


Hayo yalisemwa mjini hapa jana wakati wa utiaji saini mradi wenye thamani ya Sh Bilioni 476 zitakazowezesha kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na maeneo jirani.

Akizungumza kwenye utiaji saini huo ulioshuhudiwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha, Mhandisi Ruth Koya alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2019.

Alisema mradi umelenga kutafutaji wa vyanzo vya maji, uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa matenki, ulazaji wa mtandao wa maji safi na maji taka, ujenzi wa mitambo ya kutibu maji, ujenzi wa mabwawa mapya ya kusafirishia majitaka.

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza Julai, mwaka 2016 kazi kubwa ikiwa ni utafiti wa vyanzo vya maji. Kupitia utafiti uliofanywa na kampuni ya Kifaransa ya Egis Eau tulibaini chanzo pekee cha maji kwa Arusha ni visima virefu,” alisema Mhandisi Koya na kuongeza:

“Utafiti huo umebainisha maeneo ya manne yanayofaa kuchimba visima virefu ambayo ni Magereza-Seed Farm, Tengeru- Makumira – Usa River, Valeska – Mbuguni na Maji Moto eneo lililopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro,” alisema. 

Mhandi Koya alitaja matokeo ya utafiti huo kuwa katika eneo la Magereza lililopo wilayani Arusha na Arumeru visima 11 vilipendekezwa kuchimbwa vinavyotarajiowa kutoa lita za maji 24,000,000 kwa siku.

Alisema eneo la Tengeru  kulipendekezwa visima 15 vinavyotarajiwa kutoa lita za maji 25,000,000, Valeska kulipendekezwa kuchimbwa visima 12 vinavyotarajiwa kuta lita 40,000,000 huku eneo la Maji Moto likipendekezwa kuchimbwa visima 18 vinavyotarajiwa kutoa lita 79,000,000.

Alisema kupitia mradi huo tayari mckato wa uchimbaji visima virefu 11 eneo la Magereza umekamilika na mkataba kati ya AUWSA na mzabuni aliyeshinda Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation na Mineral Company and Jiangxi Geo –engineering umeshasainiwa.

Mhandisi Koya alisema kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza kwa uzalishaji wa maji kutoka wastani wa Lita milioni 40 hadi kufikia Lita milioni 200 kwa siku, huku usambazaji huduma ya maji ukiongezeka kutoka asilimia 44 za sasa hadi asilimia 100.

Kwa upande wake Waziri Mhandisi Kamwelwe akizungumza kwenye utiaji saini huo alisema uhifadhi wa mazingira ni msingi endelevu wa upatikanaji wa maji, kwani uchafuzi wa vyanzo vya maji na uharibifu wa maizngira una ahatri ya kusababisha janga la ukame.

“Jambo hili hatimaye husababisha ukosefu wa maji kwa matumizi ya binadamu na shughuli za maendeleo zikiwamo kilimo, viwanda uvuvi na uhai wa viumbe vingine,” alisema Waziri Kamwelwe na kuongeza:

“Jamii yote nchini inapaswa kutunza vyanzo vya maji vyote vilivyopo chini ya ardhi na maeneo chepechepe, pamoja na vyanzo vya juu ya ardhi kama mito na chemchem ni lazima zitunzwe kama mboni ya jicho,” alisema.


Fedha za ujenzi wa mradi huo  zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo imetoa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani 210,962,581 huku Serikali ta Tanzania ikichangia Dola za Marekani 22,953,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. 

No comments:

Post a Comment