Akina mama kutoka jamii hiyo nao hawapo nyuma kwenye uvutaji wa bangi wanadai huwasaidia kusisimua mwili
KARATU
JAMII ya Wahadzabe wanaojishughulisha na uwindaji, kulina asali na kukusanya matunda porini wameomba kupelekewa msaada wa bangi angalau Tani 2 watakayoitumia kwa mwaka mmoja.
Wahadzabe wanaokadiriwa kufikia 500 ni jamii inayoishi porini maeneo ya Endamaghan, Qanden Tarafa ya Eyasi wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo bado wanakabiliwa na umasikini licha ya kuwa kivutio cha watalii katika Ziwa Eyasi.
Ombi hili walilitoa juzi kijijini Endamaghan wakati walipotembelewa na timu ya wataalamu kutoka serikalini iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya muundo wa kipindi cha pili cha mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF.
Akizungumza na MTANZANIA kwenye eneo la makazi yao yenye nyumba za asili za nyasi zilizoonekana kuwa wazi kutokana na kufunikiwa na nyasi kidogo, Mwenyekiti wa Jamii hiyo Julius Ndaya alizitaja sababu alizodai ni za msingi za kuomba wapelekewa bangi.
Alisema shughuli za kutembea kutafuta wanyama kwa ajili ya kitoweo huwalazimisha kutembea umbali mrefu kiasi cha Kilomita 50 kazi ambayo huwa ni sehemu ya majukumu ya mwanaume katika jamii hiyo.
“Kiasi hicho cha tani 1 kina weza kututosha watu kama 100 au 200 hivyo kwa miezi 6, sisi tunavuta bangi si kama ambavyo wengine au serikali wanafikiria kwamba tunaweza kusababisha kuanzisha vurugu, kuvunja nyuma za watu, kuiba wala kugombana na jamii nyingine, hapana.
“Mmea huu tumeukuta babu zetu wakiwa wanauvuta wameturidhisha na sisi tunaendelea kuvuta bila kuwa na madhara yeyote. Hii ni sehemu ya kiburudisho kwetu, huku porini hatunywi pombe hii ndio pombe yetu. Tunaiomba tupatiwe kipali cha kuitumia.
“Ikiwezekana turuhusiwe kulima angalau bustani za bangi lakini changamoto kubwa tunayokutana nayo ni pale Serikali inapopiga marufuku zao hili kwa madai kuwa ni sehemu ya dawa za kulevya,” alisema Ndaya.
Kiongozi wa jamii hiyo alikwenda mbali na kueleza pindi wanapovuta bangi huchangamsha akili na miili yao hivyo hujikuta wakipiga hadithi za matukio ya uwindaji porini au namna walivyokabiliana na au kukurupushana na wanyama wakati wa uwindaji.
Katika eneo la jamii hiyo lenye nyumba za asili za nyasi zikiwa zimezungukwa na mafuvu ya wanyama pori na miti mikubwa, lilikuwa na wanawake watu wazima walionekana wamekaa kwenye makundi pamoja na vijana wa kiume wakiendelea kuvuta bangi.
Akifafanuzi kuhusu maombi ya Wahadzabe kuomba tani 1 ya bangi, Mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahongo alisema, serikali haiwezi kukubaliana na maombi hayo.
“Hata sasa walikuwa wakiniomba, na hivi majuizi tuliteketeza kiasi kama cha hekari 5 za bangi maeneo ya milimani, kwa hiyo kwa sasa hawaipati inawaumiza zaidi.
“Kikubwa tunaendelea kuwapatia elimu kwamba bangi kwao si kitu kizuri hivyo tutatafuta mbadala na kwa vile wameniomba nikutane nao hilo nalo tutaliweka vizuri,” alisema Mahongo na kuongeza:
“Naamini vipo vitu mbadala wanavyoweza kutumia badala ya bangi, mnawaona wanalalamika kwasababu hawaipati. Tunajua ni wawindani wanakimbia na kupita maeneo magumu ndio maana wanaihitaji ili iwatoe nishai, ukweli ni kwamba jambo hilo hatuwezi kuliruhusu,” alisema.
Wakati watu hao takribani 200 kutoka jamii ya Kihadzabe wakiomba kupelekewa tani 2 ya bangi, katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge waliomba zao hilo liruhusiwe kuwa la kibiashara ili kuwaongezea kipato zaidi wakulima na wauzaji wa bangi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment