-NGORONGORO
MAMLAKA ya Hifadhi ya
Ngorongoro, imeadhimisha siku ya Utalii Duniani katika Makumbusho kubwa Afrika,
Olduvai Gorge, inayoelezea historia ya chimbuko la binadamu wa kale hadi sasa.
Mhifadhi kutoka
Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, Dk Agnes Gidna, alisema mabadiliko ya
binadamu bado yanaendelea na kwamba dalili zimeanza kuonekana.
“Tunaendelea kubadilika
lakini hatuwezi kuona kwa sasa…mazingira yetu yanasababisha kwa mfano kupungua
meno kutokana na chakula tunachotafuna tofauti ilivyokuwa kwa binadamu wa
kale,” alisema.
Katika maadhimisho hayo
yalifanyika Olduvai Gorge jana, yalikuwa na lengo la kuelimisha wananchi kuhusu
chimbuko la binadamu na maendeleo yake.
Alisema walipata nafasi
ya kuonyesha mabaki ya kale ya zamadamu yaliyopatikana eneo hilo zaidi ya miaka
milioni 3.7.
Alisema makumbusho hiyo
imejengwa n kupangiliwa katika hatua nne za uhifadhi wa masalia ya kale ambazo
ni sehemu inayohifadhi masalia yaliyopatikana bonde la Laetoli zaidi ya miaka
milioni 3.7.
Alisema waliwaonyesha
baadhi ya wananchi na watalii mabaki ya mifupa, mafuvu, zana za mawe na nyayo
za zamadamu na wanyama waliokuwa tangu wakati huo.
Aidha walionyesha nakala
za masalia ya zamadamu kutoka Ethiopia, Kenya na Afrika Kusini kwa lengo la
kuelezea jinsi walivyokwa wakifafana na wa hapa.
“Tulichukua nakala za
masalia hayo ili kukamilisha historia kamili ya maendeleo ya binadamu ili kutoa
elimu kwa wananchi,” alisema.
Katika sehemu ya pili,
alisema imehifadhi masalia yaliyopatikana katika bonde la Olduvai miaka zaidi
ya milioni 2 iliyopita kama vile mimea, wanyama na binadamu na jinsi
walivyokuwa wakiishi kwa pamoja na aina ya chakula walichokuwa wakila.
Alisema ipo pia sehemu
inayohifadhi zana za mawe walizokuwa wakitumia na aina ya chakula walichokuwa
wakila, zaidi ya miaka milioni moja iliyopita.
Sehemu ya mwisho ni ile
inayoonyesha masalia ya binadamu wa sasa zaidi ya miaka laki saba iliyopita.
Baadhi ya binadamu
waliokuwa wakiishi eneo hilo walitajwa kuwa ni jamii za Wadatoga, Wahadzabe
(hawa mpaka sasa wanaendelea kuokota matunda, kurina asali na kuwinda ili
kujipatia chakula) na Wamasai.
Alisema Wadatoga ndio
wanaoaminika awali kuishi katika bonde hilo wakifuatiwa na Wahadzabe na sasa
Wamasai.
Alisema sehemu hii ndiyo
inayoonyesha uhusiano wa karibu kati ya babu na binadamu wa sasa.
Alisema makumbusho hiyo
ni ya pekee kwa sababu kila mfupa (masalia) uliopo unaonyeshwa na picha ya huyo
binadamu au mnyama hivyo kuwa rahisi kumwelewesha mtu wa kawaida.
Alisema lengo pia ni
kuwekeza kwa wanafunzi ili walimu waweza kufika hapo na kujifunza maendeleo ya
binadamu ambayo bado yanaendelea.
Kwa upande wake, Kaimu
Meneja Uhusiano wa NCAA, Joyce Mgaya, alisema, jana ilikuwa Siku ya Utalii
Duniani, ambapo walitambulisha na kujulisha umma kuhusu makumbusho hiyo ya
kisasa kabisa Afrika.
“Makumbusho hii imeongeza
thamani ya utalii kutokana na masalia yanayoonyesha historia ya chimbuko na
maendeleo ya binadamu yanayopatikana eneo hili,” alisema.
Aliwataka wanafunzi,
watafiti na wananchi kwa ujumla kupenda kutembelea makumbusho hiyo na
kujifunza.
MWISHO
No comments:
Post a Comment