Saturday, October 14, 2017

TPW YAKABIDHI RUZUKU YA SH MILIONI 1 KWA WANAWAKE WAJASIRIAMALI WILAYANI SIMANJIRO

Wanawake wajasiriamali wilayani Simanjiro 

-SIMANJIRO

WAJASIRIAMALI wanawake 375 waliopo kwenye vikundi 15 vya mradi wa uhifadhi wa mazingira na ufugaji Nyuki kijijini Loiborsit-A, Kata ya Emborreti wilayani Simanjiro mkoani Manyara wamekabidhiwa ruzuku ya Sh Milioni 10.


Ruzuku hiyo ilitolewa juzi wilayani hapa na Asasi isiyo ya Serikali ya Tanzania People& Wildlife (TPW), inayoendesha Kambi ya Mazingira Naloholo kijijini Loiborseit na kukabidhiwa kwa wajasiriamali hao na Katibu Tawala wilaya ya Simanjiro Zuena Omar.

Akizungumza wakati wa kuwakabidhi ruzuku wajasiriamali waliopo kijijini Loiborsit-A, Omari aliwataka wajasiriamali hao kuhakikisha wanajipanga kuitumia ruzuku hiyo katika kushindana kujiletea maendeleo badala ya kuzielekeza kwenye anasa.

“Akina mama wajasiriamali ruzuku hii ni kubwa inayoweza kuwatoa eneo moja kwenda jingine katika miradi yenu ya vikundi mbali na ufugaji nyuki. Niwaombe mshindane katika maendeleo na si kukopa kwa ajili ya anasa,” alisema DAS Omar.

Kupitia fursa hiyo alizielekeza baadhi ya Asasi wilayani humo zimekuwa zikijinufaisha kupitia maisha ya wananchi wilayani humo kwa misaada kupokea misaada kutoka kwa wafadhili huku zikiwa hazijulikani zinafanya nini.

“Niwapongeze TPW, wanatusaidia Serikali kupambana na kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini. Lakini zipo baadhi ya asasi nyingine wahusika wake hawajulikani wanaishi wapi, sasa naagiza kupitia usajili huu mpya nazielekeza zihakikishe zinarudi Simanjiro kushirikiana na wananchi,” alisema Omar.

Kwa upande wake Mratibu wa Elimu ya Uhifadhi Mazingira kutoka Tanzania People&Wildlife Revocatus Magayane alisema ruzuku hiyo imetokana na mradi wa uhifadhi wa mazingira walioufanya kwa miaka miwili.

Magayane alisema mradi huo unatekelezwa katika vijiji vitatu vya Tarafa ya Emborreti, ambavyo ni Loiborsoit-A, Loiborsiret na Kijiji cha Narakao ambako zaidi ya mizinga 760 yenye thamani ya Sh Milioni 38 ilikwisha kugawiwa kwa wanawake wajariamali hao.

“Lakini pia wakati tumekuwa tukitoa ruzuku ya kujenga mradi ili kuwajengea uwezo wanawake hawa mpaka sasa zaidi ya Sh Milioni 36 zilishatolewa kwenye vikundi vya akina mama wapatao 1,100 wilayani Simanjiro,” alisema Magayane na kuomngeza:

“Mradi huu umeibuliwa na akina mama, kisha TPW tukatoa elimu ya ujasiriamali wa uhifadhi wa mazingira, kuwafundisha uhifadhi na utunzaji mazingira yao vyanzo vya maji kwa faida ya vizazi vijavyo,” alisema.

Alisema baada ya kutolewa kwa elimu hiyo akina mama hao waliona ni vyema waanzishe mradi utakaowawezesha wao kunufaika kupitia mazingira yanayowazunguka na ndipo wazo la kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki lilipoanza.

“Walipoelewa nini maana ya utunzaji mazingira na namna wanavyoweza kunufaika, TPW inayosimamia Kambi ya Mazingira ya Noloholo kijijini Loiboerseit iliwafadhili mizinga ya nyuki ili kuendelea utunzaji mazingira.

“Akina mama hawa wanaoka familia za kifugaji hawana njia ya kuwapatia fedha ili kuendesha familia na mambo mengine. Mradi huu umewezesha wao kuvuna Kilogram 900 za asali kwa mwaka huu huku soko la kuuza asali hiyo likiwa ni la uhakika kupitia TPW,” alisema Magayane.

Naye Mwenyekiti wa vikundi hivyo vilivyopokea kuanzia Sh 900,000 kwa kila kikundi kulingana na kilivyotekeleza masharti Naserian Kirya alisema, mradi umewezesha akina mama hao kuendesha familia zao bila kuwa wasiwasi kama ilivyokuwa awali.

“Akina mama wanasomesha watoto, bila kutegemea waume wala hela ya ng’ombe. Tumeweza kununua sare za watoto shuleni na mahitaji mengine ya chakula nyumba, baadhi wamejenga nyumba za kisasa kupitia mradi wa mazingirawa TPW,” alisema Kirya.


No comments:

Post a Comment