WAZIRI wa Maliasili na Utalii Professa Jumanne Maghembe ameagiza mmiliki wa Kampuni ya Utalii inayodaiwa kutapeli watalii kutoka nchini Canada kiasi cha Dola za Marekani 12,000 sawa na Sh.Milioni 26,640,000 akamatwe mara moja.
Agizo la kukamatwa kwa mmiliki huyo ambaye hakuwa tayari kumtaja jina wala kampuni yake alilitoa jana mjini hapa wakati wa hafla ya utoaji vyeti na taarifa kwa huduma za malazi zilizokidhi viwango vya Nyota 1-5 kwa mujibu wa vigezo vya kupanga huduma za malazi vya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza na wamiliki wa mahoteli kutoka Mkowa wa Arusha na Manyara walioshiriki halfa hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Lake Nyassa uliopo Kituo cha Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Prof. Maghembe alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona sekta hiyo ikifa kwasababu za matapeli kujiingiza kwenye biashara hiyo.
“Kumeingia utapeli katika sekta ya utalii unakuta msafirishaji wa utalii amekubaliana na mtalii alipwe kwa siku Tano kwa ajili ya kumpeleka katika maeneo kadhaa.Lakini msafirishaji huyo anafanya utapeli kwa kumpeleka kila eneo alilotaka mgeni kwa siku tatu wakati mgeni amelipa kwa siku 5,” alisema Prof. Maghembe na kuongeza:
“Leo kuna familia ya Ki-canada imetoka kwao kuja nchini kutalii wamemlipa kampuni ya utalii moja hapa Arusha kiasi cha Dola 12,000, watalii hawa wamefikia Uwanja wa ndege wakijua watapokelewa na mwenyeji wao wanajikuta hakuna aliyekuja kuwapokea na wahusika hawapo.
“Naagiza mmiliki wa Kampuni hiyo atafutwe na akamatwe haraka kwa kuhujumu uchumi nanitaka kuona jambo hili mpaka mwisho.Serikali haiwezi kupoteza sekta ya utalii kwasababu ya matapeli. Tutahakikisha tunawasaka watu wa aina hii,” alisema bila kutaja jina la Kampuni wala mmiliki wake.
Prof. Maghembe alisema kwamba wafanyabiashara wote wanaofanya hujuma za aina hiyo tayari wamewekwa kwenye uangalizi mkali wa kuchunguzwa ambapo kama watarudia kufanya utapeli huo serikali itakuwa tayari kufuta leseni zao za biashara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi alilaani kitendo cha wasafirishaji watalii kwa kutokuwa waaminifu pindi wanapopokea fedha za wageni ikiwamo kutoa huduma zilizo chini ya viwango.
Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiharibu sifa na umaarufu wa nchi ya Tanzania zikiwamo Hifadhi wanazokuja kuzitembelea wageni ambapo aliowataka wafanyabiashara wote kuhakikisha wanazingatia maadili ya biashara hiyo pindi wanapopokea malipo kutoka kwa wageni.
“Ni vyema wafanyabiashara hawa wakapanga ratiba kulingana na malipo yalivyofanyika. Lakini pia wasiwe wadanganyifu kwa kuchukua fedha za wageni na kuzitumia kwenye matumizi mengine kabla wageni hawajafika. Kwani husababisha wageni usumbufu mkubwa wakiwa tayari wameshafika nchini,” alisema Kijazi na kuongeza:
“TANAPA tutajitahidi kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii na Chama cha Waendesha biashara ya Utalii nchini (TATO), kukaa pamoja na kufanya tathimini ya halii ili tuweze kutoa kauli ya pamoja itakayosaidia kujenga imani kwa wageni wa nje wanaopenda kutembelea Tanzania,”alisema Kijazi.
Aidha ripoti ya utoaji vyeti na taarifa kwa huduma za malazi zilizokidhi viwango vya Nyota 1-5 kwa mujibu wa vigezo vya kupanga huduma za malazi vya Afrika Mashariki EAC, imeuonyesha Mkoa wa Arusha kuwa una hoteli 8 za hadhi ya Nyota 5, Mkoa wa Manyara Hoteli 2 za hadhi ya Nyota Tano. Huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na Hoteli 4 za hadhi ya Nyota 5.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii Deograsias Mdamu alisema, utafiti huo unatarajiwa kufanyika nchi nzima ambao kwa sasa umekwisha fanyika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara na Arusha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment