Friday, August 18, 2017

RAIS WA GUINEA BISSAU: MASUALA YA HAKI ZA BINADAMU YANA UMUHIMU MKUBWA

RAIS wa Jamhuri ya Guinea Bissau Jose Mario Vaz amesema, masuala ya haki za binadamu yana umuhimu mkubwa katika kufikiwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi za Afrika ikiwamo kuwaondoa wananchi kwenye lindi la umaskini na ufukara.

Aidha Rais Vaz aliahidi kuwa, nchi yake itaridhia Itifaki iliyoanzisha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), mapema iwezekanavyo.


Akizungumza na ujumbe kutoka Mahakama ya Afrika uliotembelea ofisini kwake Ikulu nchini Guinea Bissau jana, Rais Vaz alisema, kuridhia hatua hiyo kunatokana na nchi yake kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo za Umoja wa Afrika kutia saini itifaki iliyoanzisha mahakama hiyo mwaka 1998.

“Masuala ya haki za binadamu yana umuhimu mkubwa katika kufikiwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi za Afrika na kuwaondoa wananchi wake katika lindi la umaskini na ufukara,” alisema Rais Vaz katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotumwa mjini hapa jana na kuongeza:

“Ahadi yangu ni kuhakikisha kuwepo kwa haki za binadamu katika nchi yangu,” alisisitiza mbele ya ujumbe huo ulioongozwa na Rais wa AfCHPR Jaji Sylvain Ore.

Taarifa kwa vyombo vya habari ilisema ujumbe huo ulikutana pia na Waziri Mkuu wa Guinea Bissau Umario Sissoco Embalo ambaye kwa upande wake alisema mamlaka husika za nchi yake zitaandaa nyaraka zinazohitajika ili kuzipeleka bunge la taifa kwa lengo la kuridhia itifaki iliyoanzisha AfCHPR.

“Mimi ni muumini mkubwa wa umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) na nitafanya kila linalowezekana kuimarisha Taasisi za Umoja wa Afrika,” alisisitiza Waziri Mkuu Embalo.

Naye Rais wa AfCHPR Jaji Ore alisema, ili kufanikisha malengo ya mahakama na pia kuimarisha mfumo wa haki za binadamu barani Afrika nchi nyingi za Umoja wa Afrika hazina budi kuridhia itifaki iliyounda AfCHPR kwa mujibu wa kifungu cha 34(6) na kutoa tamko rasmi la kutambua na kukubali mamlaka ya mahakama kuweza kupokea kesi za watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Jaji Ore aliyeongozana na Makamu wa rais Jaji Ben Kioko, Mheshimwa Jaji Angelo Matusse na baadhi ya maafisa wa ofisi ya msajili wa AfCHPR pia alikutana na  Jaji Mkuu, Waziri wa masuala ya jamii na pia Kamisheni ya haki za binadamu ya Guinea Bissau.

Hadi sasa ni Nchi 30 tu kati ya nchi 55 wanachama wa AU ndio zimeridhia itifaki husika.

AfCHPR yenye makao yake makuu jijini Arusha, ambapo ujumbe huo uko nchini Guinea Bissau kwa ziara ya kikazi ya siku 2 inayolenga kukutana na viongozi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuitangaza mahakama hiyo.

MWISHO

No comments:

Post a Comment