Baadhi ya wananchi wa Kata ya Ololosokwan wilayani Ngorongoro wakiwa na mizigo yao tayari kwa kuondoka maeneo ya ndani na mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hii ni kufuatia Oparesheni inayoendeshwa na Serikali ya kuwaondoa wananchi wote kwenye maeneo hayo.
Sehemu ya makazi ya Boma la mmoja wa wananchi wanaoishi katika Kata ya Ololosokwan wilayani Ngorongoro mkoani Arusha ikiwa imechomwa moto tayari.
Diwani wa Kata ya Ololosokwan wilayani Ngorongoro Yannick Ndoinyo akielezea namna nyumba hizo zilivyochomwa.
SERIKALI imeziondoa kwa nguvu zaidi ya kaya 25 za wafugaji
waliokuwa wakiishi ndani na wengine mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
na Pori Tengefu la Loliondo.
Kutekelezwa kwa Oparesheni hiyo iliyoanza Agosti 12, Mwaka
huu ikiwa tayari ilishatangazwa kumewaibua viongozi wa wananchi katika Tarafa
ya Loliondo, wilayani humo wakidai kutoridhishwa na zoezi hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana juu ya oparesheni
hiyo, Diwani wa Kata ya Ololosokwani Yannick Ndoinyo alidai kuwa katika Kata
yake oparesheni hiyo imechoma maboma ya kudumu matano yenye kaya 12.
Ndoinyo alidai kwamba tangu kuondolewa kwa kaya hizo
kumesababisha hasara kubwa kwani hawajui watu hao wameelekea wapi wakiwamo
watoto na mifugo yao.
“Ukichoma nyumba ya mtu pekee hiyo ni hasara, lakini pia
ukimsababishia hasara ya maisha yake nayo ni hasara, wale watu wana mifugo wana
watoto hatujui wapo wapi,” alidai Diwani Ndoinyo na kuongeza:
“Tukio kama hili ni la pili kufanyika mwaka 2009
lilifanyika kwa askari kuchoma maboma kama hivi lakini baadaye serikali ilikana
kuhusika kwa hiyo hata hili naamini si jambo la Serikali,” alidai.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Arashi Mathew Siloma alidai katika eneo lake
yamechomwa zaidi ya maboma 19 ya wananchi.
Filoma alidai kwamba oparesheni hiyo imefanyika katika
katika ardhi ya vijiji vilivyoko nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Tumepokea kwa mstuko mkubwa kuhusu oparehseni inayoendelea
kutokana na kuwapo kwa mgogoro mkubwa wa eneo la Kilometa 1,500, bado maamuzi
yake yalikuwa hajatoka kwa Waziri Mkuu.
“Juzi Agosti 12, Mwaka huu tumeona oparesheni ikichoma
maboma kimsingi hatupingi zoezi la kuondoa mifugo ndani ya hifadhi ya Serengeti.
Lakini kuchoma makazi ya wananchi kwenye ardhi ya kijiji hili
halikubaliki. Jambo hili linafanywa kwa usiri kubwa, tunafuatilia kujua kiini
cha oparesheni hii kama kweli ni zile Kilometa 1,500.
“Maeneo ya Ololosokwan, Arash wamechoma maboma yaliyoko nje
ya hifadhi zaidi ya Kilomita 3 kwingine mpaka 12 ni maeneo ya wananchi wameyatumia
kwa miaka mingi kwa malisho na kupata maji,” alidai Filoma.
Kwa mujibu wa barua ya Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Rashid
Taka ya Agosti 5, Mwaka huu kwenda kwa maofisa watendaji Kata na Vijiji, Kata
za Piyaya, Arash, Maalon, Oleipiri, Soitsambu, Lorien na Ololosokwan
kuwajulisha wananchi wao waliojitwalia maeneo ya kuishi ndani ya Hifadhi ya
Serengeti na mpakani mwa Pori Tengefu la Loliondo kuondoka kwenye maeneo hayo
na mifugo yao ifikapo Agosti 10, Mwaka huu.
Barua hiyo ilizitaja hatua kali zitakazochukuliwa baada ya
muda huo kumalizika kuwa ni pamoja na kuwaondoa kwa nguvu wale wote waliokaidi
ambapo Kamati ya ulinzi na usalama itakayofanya kazi na kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya ya Serengeti na kikosi maalumu kutoka SENEPA na NCA.
“Wale wote watakaokutwa wakiwa ndani ya hifadhi ya
Serengeti watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ikiwamo
kushitakiwa mahakamani.
“Wale watakaokutwa wakiwa bado wamejenga au kukaa mpakani
kabisa mwa hifadhi ya Serengeti kwenye (LGCA), wataondolewa kwa nguvu na
kurudishwa kwenye vijiji vyao yalikotengwa maeneo ya kuishi,” ilisema barua
hiyo iliyosainiwa na Dc Taka.
No comments:
Post a Comment