*Soko lahitajika tani milioni 4.5
FURSA mpya ya kilimo cha matunda aina ya Parachichi katika Mkoa wa Njombe, imetajwa kujificha kwenye mwinuko wa kati ya Mita 1,700 hadi 2,400 kutoka usawa wa bahari.
Mwinuko huo wa kipekee ndio unalifanya eneo la mkoa huo kuwa la
kipekee katika uzalishaji mkubwa wa Parachichi katika msimu ambao, maeneo mengi
duniani zikiwamo nchi za Peru na Mexico zinakuwa na kiwango kidogo cha
uzalishaji wa tunda hilo katika soko la dunia.
Hali hiyo ya hewa imewezesha utekelezaji mzuri na kutoka
mazingira rafiki ya ulimaji hasa kupungua kwa gharama za umwagiliaji kwani
ardhi yake hubakia nyevunyevu kwa muda wa kutosha kutokana na uwapo wa mvua kwa
kipindi kirefu cha mwaka.
Kilimo cha Parachichi mkoani Njombe kwa sasa kinatajwa kuwa ndio
fursa mpya pekee inayoweza kumtengenezea faida kubwa mkulima endapo tu atakuwa
amefuata kanini na maelekezo ya kupanda miche kisasa shambani mwake.
Wananchi mkoani humo kwa mingi wamejishughuli na ulimaji mazao
mbalimbali na kupandaji miti kwa ajili mbao. Lakini ujio wa kilimo hicho cha
Parachichi ambacho si maarufu sana sasa utafungua ukurasa mpya kwa wananchi
kujiletea maendeleo zaidi.
Kikiwa ni kilimo ambacho bado hakijapata umaarufu sana mkoani
humo kwa sasa, sasa ni takribani miaka miwili tu imepita tayari wakulima
wachache wameanza kuonyesha kupata mafanikio ya kulima parachichi.
Hamasa miongoni mwa wananchi imeshamiri miyoni mwao na
kuwasukuma kulima parachichi ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau
wakipigana kuongeza juhudi za kusaidia utekelezaji wa kilimo hicho ambacho soko
lake linahitaji tani zaidi ya milioni 4.5 kila mwaka.
Ili kukamilisha fursa hiyo kwa wana Njombe, ni wazi kwamba Idara
ya kilimo mkoani humo kwa kushirikiana na Asasi Kilele inayoendeleza kilimo cha
bustani za mbogamboga, matunda na maua (TAHA), wameendelea kuwasaidia wakulima
wa zao hilo kuhakikisha wanafikia mafanikio.
Katika jukumu hilo wamekuwa wakitoa huduma za kitaalamu kwa
vikundi vya wakulima namna ya kulima kilimo cha kisasa cha parachichi
kitakachowezesha wazalishe zaidi na kukidhi haja ya soko, kwani wakulima hao
wanazalisha tani 600 hadi 800 pekee, wakati soko likihitaji tani milioni 4.5.
Afisa Kilimo kitengo cha mazao wa halmashauri ya Njombe Nolasco
Kilumile anasema, mbali ya kushauri wananchi walime mazao mengine, bado
wameendelea kuwashauri kama watalaamu kulima zaidi parachichi kwani linawapatia
fedha kwenye msimu ambao kunakuwa hakuna tunda hilo maeneo mengine.
“Tunawashauri wachague mnyororo wa dhamani unaofanya vizuri,
lakini sisi tunamewaambia parachichi linafanya vizuri zaidi, tungependa
wakulima wengi waingie kwenye kilimo hiki
Kwa upande wake Bwana shamba wa TAHA Damas Kisalala yeye
anasema, mahitaji kwa wakulima yameanza kuwa makubwa hivyo wamelazimika
kuanzisha bustani kwa ajili ya kutoa miche bora kupitia aina ya mbegu bora ya
hasi.
“Tunazalisha mbegu hii ya hasi kwasababu ina fursa nzuri ya
kibiashara sokoni ambayo mahitaji yake ni makubwa na kwa Njombe peke yake zipo
kampuni kubwa zinazohitaji zaidi ya Tani Milioni 1 kwa mwaka,” anasema
Kisalala.
Tofauti ya muda wa uvunaji ni moja ya faida inayotoa uhakika wa
soko la Parachichi kutoka mkoani Njombe ambapo Kisalala anasema, nchi kama
Mexico na Peru mavuno yao ya Parachichi yamekuwa yakiingia sokoni kuanzia
Februari, Machi hadi Aprili.
“Kwa hiyo kuanzia Mei, Juni, Julai hadi Agosti kila mwaka Njombe
pekee ndio huwa inalisha matunda ya Parachichi katika soko la dunia kwani
kwingine kote uzalishaji wake huwa wa chini wakati huku ukiwa juu.”
“Hata tukizalisha tani milioni 1 tuna uhakika kabisa wa kuuza
matunda yetu sokoni,” anasema Kisalala.
Naye Mkulima wa Parachichi kutoka Kijiji cha Itulike mkoani
Njombe Erasto Ngole anazitaja faida alizozipata kutokana na kilimo hicho cha
parachichi katika maisha yake.
Anasema, mwaka wa 2017 amekuwa akiendelea kuzingatia maelekezo
kuanzia katika kilimo hicho kwani mpaka sasa tayari amefanikiwa kuvuna kiasi
cha tani 13 za Parachichi kutoka shambani kwake.
Katika mavuno ya kwanza Ngole anasema alipata Sh. Milioni 16.8
zilizomuwezesha kujenga nyumba ya kisasa kununua gari pamoja na kuendelea
kuboresha shamba lake.
No comments:
Post a Comment