AGOSTI 8, Mwaka huu raia wa Kenya takribani milioni 19
waliojiandikisha kupiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka
mingine mitano ijayo, huenda wakajitokeza kwa idadi hiyo kutimiza haki yao ya
kikatiba.
Wagombea katika Uchaguzi Mkuu huo wa wanaopewa nafasi ya
kuchaguliwa ni Rais Uhuru Kenyata anayemaliza muda wake kupitia Chama cha
Jubilee, Raila Odinga kupitia muungano wa upinzani (National Super Alliance
–NASA).Wengine ni Cyrus Jirongo (UDP), Dk. Ekuru Aukot kutoka Third way
Alliance, Abduba Dida (ARC) na wagombea huru Joseph Nyagah, Profesa Michael
Wainaina na Dk. Japheti Kaviga.
Kenya moja ya kati ya nchi Sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), inatajwa kuwa imara zaidi katika uchumi ikilinganishwa na nchi
nyingine wanachama zilizopo ukanda huo.
Licha ya uchumi imara, nchi hiyo imetajwa kupiga hatua zaidi
katika masuala ya demokrasia ambapo uchaguzi wa mwaka huu mbali ya kutoa fursa
hiyo kwa raia walio Kenya, imekwenda na kutoa haki ya kupiga kura kwa raia
wanaoishi nje ya nchi.
Lakini kama haki hiyo ya kidemokrasia imepanuka zaidi kwa kwa
kutoa fursa kwa wafungwa nchini humo kutumia haki ya kikatiba kuchagua viongozi
wanaowataka wakiwa ndani ya magereza tofauti na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki.
Kama ilivyokuwa kwa raia waishio nchini Kenya kujitokeza kupiga
kura za kuchagua viongozi wao jana, ndivyo ilivyokuwa pia mkoani Arusha
Kaskazini mwa Tanzania ambapo kulikuwa na kituo cha kupigia kura kwa watu
waishio na kufanya kazi nje ya Kenya.
Saa 12 asubuhi kama zilivyo taratibu za upigaji kura kituo cha
kupigia kura kwa raia wa Kenya waishio mjini Arusha na maeneo jirani
kilifunguliwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Kutokana na madhari ya kituo hicho kuwa ya kiusalama zaidi
wapiga kura wenye sifa ya kupiga kura katika kituo hicho wanaokadiriwa kufikia
370 walikuwa wakijitokeza katika eneo hilo kwa makundi huku wengine wakiwasili
kwa magari yao.
Kwa kadiri muda ulivyokuwa ukisonga ndivyo idadi yao ilikuwa
ikiongezeka na hata kwa wakati mwingine kujikuta wakilazimika kupanga foleni ya
kuanzia watu Tisa hadi 10. Hatua iliyoonyesha ni kwa jinsi gani raia hao
wamehamasika kupiga kura.
Usalama wa eneo hilo ulikuwa umeimarishwa kutokana na kuwapo
askari polisi walioimarisha doria ndani ya ukumbi pamoja na nje huku baadhi yao
wakitoa maelekezo kwa wapiga kura kufuata taratibu za kupanga foleni na
kusimama eneo sahihi kabla ya kwenda kupiga kura.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana Afisa Msimamizi wa
Kituo hicho kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Patrick Nyakira
anasema tangu kufungulia kwa kituo hicho upigaji wa kura ulikuwa katika hali ya
utulivu na usalama.
Nyakira anasema, kituo hicho kilifunguliwa Saa 12 asubuhi na
wanatarajia kukifunga Saa 11 jioni ambapo kwa wapiga kura wote watakaokuwa
kwenye foleni wataendelea kuhudumiwa.
“Wapiga kura wanaendelea kujitokeza kama unavyoona wamepanga
foleni. Na hadi kufikia Saa 5 asubuhi tayari wapiga kura zaidi ya 100 walikuwa
tayari wamepiga kura zao ikiwa ni sawa na asilimia asilimia 33.Tunatarajia
wapiga kura wengi watajitokeza kwa kadri muda unavyokwenda,” anasema Nyakira.
Kwa upande wake mpiga kura raia wa Kenya anayeishi nchini Sista
Jane Waithira kutoka Shirika la Masista wa Mary Emmaculate- Burka Jimbo Kuu la
Arusha yeye ameipongeza Serikali ya Kenya kwa kutoa fursa ya kupiga kura kwa
raia waliopo nje ya nchi.
Sista Waithira anasema, fursa hiyo ya kupiga kura akiwa nje ya
Kenya ameisubiria kwa miaka mingi na hivyo kwa mwaka huu amefurahia kutimiza
ndogo yake ya kuchagua kiongozi akiwa nje ya nchi.
“Nimefarijika sana kupiga kura nikiwa nje ya nyumbani, fursa hii
tuliingojea kwa miaka mingi hatimaye imewadia na imenipa haki ya kuchagua
kiongozi kwani vurugu zilizotokea mwaka 2007 kwa hakika hazikuwa na afya kwa
nchi yetu,”anasema Sista Waithira.
Kituo hicho kilichopo ukumbi wa Jiji la Arusha ni sehemu ya
vituo 40,883 vya kupigia kura vilivyo sajiriwa na Tume ya Uchaguzi ambapo kwa
wapiga waliopo nje ya nchi wao watashiriki kupiga kura ya rais peke yake.
Kwa raia waliopo nchini Kenya wamepiga kura ya kuchagua Magavana
wa Kaunti, Wabunge, Maseneta wawakilishi wa Wanawake na Wawakilishi wa Wadi.
No comments:
Post a Comment