Msemaji Mkuu wa Mhadhara Prof. Brian Van Arkadie
AKIWASILISHA mada yake Prof. Arkadie amewataka wataalamu kubadilika katika namna ya kusaidia kuongeza tija katika kilimo na kuachana na dhana za zamani kwamba wakulima wameshindwa kubadilika na kukwamisha maendeleo.
Amesema katika mjadala huo wa hadhara kuhusu maendeleo ya kilimo
kutoka wakati wa uhuru hadi sasa katika jengo la mikutano la ESRF mjini hapa
alisema kwamba tafiti nyingi zimekuwa zikishutumu wakulima kwa kuwa na muono
mdogo na kubisha mabadiliko yanayohitaji kuongeza uzalishaji.
Aidha amesema kumekuwapo na tafiti zinazoonesha kilimo kimekwama katika uasili wake na kuhitajika tafiti za kuona namna bora ya
kukikwamua. Hata hivyo alisema Profesa huyo, kumekuwapo na mabadiliko ya maana
katika uchumi wa vijijini, hasa kwa kuangalia uhalisia wa uchumi kwa kuzingatia
fursa za kiuchumi na masoko katika maisha ya wanakijiji.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo ni dhahiri kusema kwamba
wakulima hawabadiliki ni kushindwa kwa wataalamu ambao ndio walibuni na kupanga
mipango ambayo haikuweza kuwanufaisha wakulima.
Prof. Brian Van Arkadie ambaye pia alishawahi kuwa Mhadhiri Chuo
Kikuu cha Dar es salaam na miongoni mwa watafiti ESRF anasema kuna hatua
mbalimbali zilizofikiwa na wakulima wa Tanzania tangu uhuru na kwamba kuna
uhusiano kati ya kilimo na maendeleo yaliyopo sasa.
Amesema mkutano huo wa hadhara umelenga kuchambua masuala
muhimu yanayojitokeza katika kilimo cha Tanzania na kuona namna bora ya
kukabiliana na changamoto hizo kwa maendeleo ya taifa, kuwa kuanzia miaka ya
1970 mazao kwa ajili ya masoko ya nje yaliporomoka sana na kusababisha taifa
kutafuta njia nyingine ya kurekebisha hali hiyo ikiwamo kuanzishwa kwa mradi wa
kubadili kilimo wa SAGCOT.
Ingawa mazao hayo ya kilimo yameonakana kuporomoka kutoka miaka
hiyo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la pengo la kipato kati ya watu wa mijini na
vijijini huku ukuaji wa vijijini ukikumbwa na udumavu. Pamoja na ukweli huo
amesema profesa huyo, kuna mabadiliko ya kutosha katika maeneo ya vijijini na
katika kilimo kwamba kusema hakuna maendeleo si kitu sahihi.
Alisema zipo sababu za kupungua kwa uzalishaji wa mazao makuu
kama kahawa, tumbaku, mkonge na hilo linatokana na serikali kuingilia kati
mfumo wa masoko ambao haukuwa unaswihi. Profesa huyo alisema hata hivyo, kwa
miaka 50 kilimo cha Tanzania kimefanikiwa kulisha taifa kwa kuwezesha watu wa
mijini na vijijini kupata vyakula hasa vile vya msingi ingawa wakati mwingine
ukame ulileta usumbufu.
Huku Tanzania ikiwa na ongezeko la watu kutoka milioni 12.3 kwa
mwaka 1967 hadi milioni 44.9 kwa mwaka 2012 ni dhahiri ukuaji wa kilimo
umesaidia kuiweka nchi katika hali bora zaidi ya upatikanaji wa chakula ingawa
ifikapo mwaka 2030 watu wa mijini watakuwa wameongezeka kwa asilimia 37 na
kuweka shinikizo ambalo kwa namna nyingine linaweza kuwa na maana kwa kuwa
mazao ya chakula yatakuwa ndiyo ya biashara na hivyo kuacha kutegemea yale ya
asili kama kahawa na tumbaku.
Katika utafiti mwaka 2007, imeonekana kwamba nusu ya mapato ya
watu wa Dar es salaam yamekuwa yakitumika kwa ajili ya kununua chakula na
kufanya kiasi kikubwa cha kazi za kilimo katika mazao ya chakula kuwa biashara
nzuri kwa wakulima.Katika mada yake profesa huyo alisititiza kwamba hakuna
shaka maendeleo nchini katika kilimo yapo lakini tafiti nyingi zimeshindwa
kuelekeza kisahihi maendeleo hayo na ukweli wa kutoneemeka kwa wakulima.
Akijadili mada hiyo ya Prof. Brian Van Arkadie, Mtafiti mshiriki
mwandamizi wa ESRF Prof Samuel Wangwe ameshauri serikali kutonakili mikakati na
sera za nchi zilizoendelea wakati wa utekelezaji wa mikakati ya kugeuza nchi
kuwa taifa la uchumi wa kati linalotegemea viwanda.
Alisema hayo katika mhadhara kuhusu kilimo nchini kwamba si sawa
kunakili sera na mikakati ya nchi zilizoendelea kama Uingereza, Asia ama
Marekani katika kutekeleza sera ya viwanda bali ibuni yenyewe kwa kuzingatia
hali iliyopo.
Akizungumza wakati akijadili mada iliyowasilishwa na Prof Brian
Van Arkadie kutoka Uingereza kuhusu mazao ya chakula kama ndio mazao ya
biashara katika mikakati ya muda mrefu ya kubadili kilimo cha Tanzania na
athari za kisera, Prof Samuel Wangwe alisema kila nchi ina njia yake ya kufikia
ustawi na neema ya viwanda na hivyo Tanzania lazima ifuate njia yake na sio
kunakili.
“Hatuwezi kupita njia ambayo nchi kama Uingereza, Japan, au nchi
za Ulaya zimepita wakati wakikua kiviwanda, lakini tuwe na njia yetu katika
kuelekea uchumi wa viwanda . Kama hatutakuwa makini hatutafanikiwa,” amesema.
Prof Wangwe pia amesema kwamba mapinduzi ya Kilimo lazima yapewe
kipaumbele kama taifa linataka kuwa na uchumi wa viwanda. Akikaribisha wadau
kushiriki katika mhadhara huo Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida
alisema kwamba mhadhara huo ulikuwa ni njia muafaka ya kubadilisha maarifa ili
kuboresha kilimo cha Tanzania kwa kukipatia kilimo hicho mkakati wa muda mrefu
wa kubadilika.
Professa Samweli Wangwe
Amesema katika kuimarisha kilimo hicho ni vyema masuala yanayogusa
mazao ya chakula na yale ya kupeleka nje na sera kuangaliwa kwani masuala hayo
yana athari za muda mrefu katika ukuaji wa kilimo.
Katika hadhira hiyo aliwataka washiriki kuangalia kwa makini
historia ya kilimo nchini, sera na kuona athari za muda mrefu na fupi za sera
zilizopo na kama kweli wataalamu wametekeleza wajibu wao katika kutafuta suluhu
ya wakulima au kuendelea kudai kwamba wakulima hawako tayari kubadilika.
Dk. Kida amesema kwa kuangalia historia ya kilimo Tanzania
wataalamu hao watakuwa na nafasi kubwa ya kuchangia katika kuendeleza kilimo
ambacho ni msingi mkubwa wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kwani wapo asilimia
80 wakitegemea kilimo na taifa ambalo linataka kwenda katika uchumi wa viwanda
ambavyo mali ghafi zinategemewa kutoka katika sekta ya kilimo.
Dk. Kida
Aidha alimshukuru Prof. Brain Van Arkadie ambaye ndiye alikuwa
msemaji mkuu kwa utafiti alioufanya ambao aliuwasilisha mbele ya mkutano wa
wasomi mbalimbali.
Prof. Van Arkadie ambaye ni veteran ameshawahi kushiriki
katika mpango wa miaka mitano wa kwanza wa maendeleo Mwaka 1963. Na kufanyakazi
katika maeneo mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki na Chuo Kikuu cha Dar
es salaam.
No comments:
Post a Comment