Thursday, August 24, 2017

TANAPA, CHEM CHEM FOUNDATION, BURUNGE WMA KUSAKA MAJANGLI KWA PAMOJA

-ARUSHA

VITA dhidi ya ujangili katika eneo la ikolojia ya Tarangire na Manyara, imeongezwa nguvu baada ya Askari wa Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA), kuanza kushirikiana na Taasisi ya Chemchem foundation na askari wa Jumuiya ya Wanyamapori (WMA) ya Burunge kuendesha doria za mara kwa mara kupambana na majangili.


Wakizungumza wakati wa zoezi hilo jana, Askari kikosi maalum cha kupambana na ujangili katika taasisi hizo,walisema mpango huo, utawezesha kuimarishwa ulinzi katika maeneo ya nje ya hifadhi baada  ya maeneo ya ndani ya hifadhi ulinzi kuwa imara.

Katika maeneo ya nje ya hifadhi tayari vitendo vya ujangili vilianza hasa kwa kuuwa wanyama kwa ajili ya vitoweo, ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na uvuvi haramu

Meneja rasilimali watu wa hoteli za Chemchem, Luteni Kanali mstaafu, Leonard Werema alisema wameamua kushirikiana ili kuhakikisha eneo lote la ikolojia ya Tarangire- Manyara linabaki salama.
"Hivi sasa kuna wanyama wengi  wapo nje ya maeneo ya hifadhi hasa katika eneo la Burunge WMA sasa tumeona ni vyema kushirikiana kuhakikisha wanyama hawa wanakuwa salama ndani ya hifadhi na nje ya hifadhi"alisema
Alisema kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi nje ya hifadhi, hivi sasa wanyama kama Simba wameanza kuonekana katika eneo la Burunge WMA na wanyama wengine hatua ambayo inatokana na kuimarishwa uhifadhi na ulinzi.
Meneja uhusiano wa TANAPA, Pascal Shelutete akizungumza mikakati ya kupambana na ujangili, alisema jukumu la kulinda wanyamapori na rasilimali za taifa ni la watanzania wote na akatoa wito wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kusaidia vita dhidi ya ujangili.
"tunawaomba wananchi kutupa taarifa za watu wanaojihusisha na ujangili watowe taarifa katika vyombo vya serikali bila ya hofu na serikali itachukuwa hatua"alisema

Mwenyekiti wa Burunge WMA, Ramadhani Ismail inayoundwa na vijiji 10 wilayani Babati mkoa wa Manyara,alisema  wamejipanga kuhakikisha majangili wanadhibitiwa katika eneo la Ikolojia ya Tarangire na Manyara.

Katika eneo la WMA vijiji vinanufaika sana na fedha kutoka kwa wawekezaji ambao ni Un Lodge en Afrika wanaomiliki hoteli za Chem chem,EBN Hunting Safaris,Maromboi Campsite, Burunge Camp site hivyo lazima tunashiriki ulinzi kuhakikisha eneo hili tunalilinda"alisema.
MWISHO.


No comments:

Post a Comment