Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Naibu Waziri wake, Mhandisi Stella Manyanya kulia, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kushoto, Mkuu wa wilaya ya Arusha Fabian Daqarro na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Simon Msanjila wakati wa uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa majengo ya Maabara Njiro mjini Arusha.
-ARUSHA
KUKAMILIKA kwa ujenzi wa Mradi
wa Maabara ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), kutaifanya
Tanzania kuwa Kituo mahiri cha Kanda katika masuala ya uhamasishaji na udhibiti
wa matumizi salama ya nguvu za atomiki.
Majengo ya Maabara hiyo ya
kisasa yatarajiwa kukamilika Februari Mwaka 2018, huku ujenzi huo ukigharimu
Sh. Bilioni 2.3, kisha kufungwa vifaa vyenye thamani ya Sh. Bilioni 11 ambapo
baadhi ya vifaa vya Sh. Bilioni 2.6 vimekwishawasili nchini.
Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe
la msingi uliofanywa jana mjini hapa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia
Professa Joyce Ndalichako,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki
(TAEC),Brigedia Jenerali Fulgence Msafiri, alisema mradi huo unaihusisha
Serikali na Umoja wa Ulaya (EU).
Brigedia Jenerali Msafiri
alisema, Maabara hiyo itaiwezesha Tanzania kujenga uwezo katika kusimamia
uchimbaji, uchakataji na usafirishaji wa madini ya Urani kwa kuzingatia usalama
na viwango vya kimataifa, tija na faida, ikiwamo kujengea uwezo maabara za Tume
hiyo.
“Manufaa yatakayotokana na
Maabara ya Teknolojia ya Nyuklia ya TAEC ni
kuongeza ufanisi wa tafiti mbalimbali katika fani ya Nyuklia hususani
kutoa msaada wa utafiti kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika ngazi za Shahada ya
Uzamili na Uzamivu,” alisema Brigedia Jenerali Msafiri na kuongeza:
“Kushiriki kiutafiti na Wizara
ya Afya katika tiba, Wizara ya Kilimo katika kuboresha uzalishaji wa mazao na
hifadhi yake na Wizara ya Nishati na Madini
katika kupatikanaji wa umeme ikiwamo kuongeza ufanisi wa kazi ya
kuhamasisha na kudhibiti matumizi salama ya nguvu za atomiki nchini,” alisema.
Alizitaja Taasisi zinazohusika
na mradi huo nchini kuwa ni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambayo
itahusika kuimarisha uwezo wa kudhibiti mionzi kupitia TAEC, kwa upatikanaji wa
vifaa na mafunzoili kuweza kudhibiti shughuli za matumizi vya vyanzo vya mionzi
ikiwamo uchimbaji urani.
Alisema kwa upande wa Wizara ya
Nishati na Madini itakuwa ni kujenga uwezo wa matumizi ya nguvu za nyuklia,
hususani uzalishaji wa umeme endapo serikali itaweka na kusimamia utekelezaji
wa sera ya matumizi ya nguvu hizo. Kwani Kilogramu moja ya Urani asili
husalisha joto sawa na linalopatikana kutokana na tani 20 za makaa yam awe.
“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano itakuwa na jukumu la usafirishaji wa urani na pia kubainisha uwezo
wa bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo ya daraja la Saba ikiwamo madini
ya urani ikiwamo Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha mradi
husika unakuwa rafiki kwa watu na mazingira.
“Kwa upande wa EU mradi
unahusisha Kampuni ya LOKMIS kutoka Lithunia inayohusika na uboreshaji wa
Maabara za Tume kwa usafirishaji na usimikaji wa vifaa na kampuni ya ENCO: STK
ya Finland na SCK.CEN kutoka Belgium inayohusika na mafunzo,” alisema Brigedia
Jenerali Msafiri.
Kwa upande wake Waziri Prof.
Ndalichako akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi alisema ujenzi wa Maabara
hiyo unafanywa kwa fedha za serikali ambapo awamu ya kwanza tayari Sh. Bilioni
1 zimekwisha kutolewa huku Sh. Bilioni 1.3 zikitarajiwa kutolewa katika awamu
ya pili.
Katika hafla hiyo, Prof.
Ndalichako aliitaka TAEC kuhakikisha Maabara hiyo pindi itakapoanza utekelezaji
wake ianze kuchangia Mfuko wa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi
kutokana na kuanza kuingiza fedha.
“Nitoe wito Maabara hii ni ya Watanzania
wote itumike vizuri kuliingia taifa faida kwani ukamilikaji wake utakuwa wa manufaa
kwa nchi. Na katika bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga Sh. Bilioni 2 kwa
ajili ya kusomesha wataalamu wakiwamo watakaofanya kazi hapa,” alisema Prof.
Ndalichako.
Maabara hiyo itakuwa na vyumba
maalumu vya uhakiki wa vifaa vya kupimia mionzi, chumba cha mionzi ya kupimia
vyuma kwa njia ya kupiga picha kwa kutumia mionzi na chumba cha kutumia mionzi
kwa ajili ya shughuli nyingine ambapo kitrasimikwa kifaa cha kupima viasili vya
mionzi vilivyo mwilini mwa binadamu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment