Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Professa Jumanne Maghembe amesema
Bodi mpya ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeteuliwa kuendesha
shirika la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si ubia kati ya
wananchi wenyeji na Serikali.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana mara baada ya kuzungumza na
wajumbe wapya wa bodi hiyo ambayo imekuwa tofauti na bodi zilizopita zilizokuwa
zikijumuisha pia wajumbe kutoka Baraza la Wafugaji kutoka Tarafa ya Ngorongoro.
Alisema uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo uliangalia maslahi mapana
ya Serikali ikiwamo utekelezaji wa kazi zilizopo katika eneo hilo linaloiingia
Taifa fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote.
“Katika kuangalia wajumbe hakuna mahali pamesema wajumbe kutoka
kwa Wasukuma au Wangoni, imeangalia maslahi mapana ya nchi. Uteuzi huu
umefanywa kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu,” alisema Waziri Maghembe na
kuongeza:
“Bodi hii si ya ubia kati ya Serikali na wananchi wanaoishi
ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro imeteuliwa kuendesha shirika.Bodi haiwezi
kutengenezwa kwa mazoezi kwamba lazima iwe na wajumbe kutoka Baraza la wafugaji
hapana,” alisema.
Waziri Maghembe awataka wajumbe wa bodi hiyo kutambua majukumu
yao kuwa ni kutekeleza mlengo ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambayo ni
kuhifadhi kuhamasisha utalii wa nje na ndani na kuangalia huduma kwa wananchi
wanaoishi ndani ya eneo hilo kisheria.
“Hayo ndio mambo muhimu nimewasisitizia wahakikishe
yanatekelezwa, zipo changamoto kama ongezeko la watu na mifugo ndani ya
Mamlaka, ambazo kwa sasa hatua kubwa za makusudi zinaendelea kuchukuliwa
kukabiliana nazo.
“Nimeagiza wahakikishe hatua za makusudi za kuzuia uhamiaji wa
watu wengine ndani ya eneo la hifadhi pamoja na ongezeko la mifugo ambapo
kwasasa tunaendelea na sensa ya watu na mifugo kuweka alama ili kujua ni mifugo
ya nani ina kaa wapilengo ni kusaidia kuendeleza uhifadhi na kujua idadi kamili
ya mifugo,” alisema.
Akizungumzia kuhusu baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo
ya hifadhi Prof. Maghembe alisema, hatua zinazochukuliwa kwa sasa ni kuondoka
wenyewe kwa hiari kwenye maeneo hayo pamoja na mifugo yao.
“Naagiza watu hao waondoke mara moja kitakachofuata ni
kuondolewa kwa maboma yao na mifugo pamoja na kuwapeleka mahakamani. Kwani hivi
sasa kuna watu wanaingia na kutoka wakijifinya na wao ni wenyeweji tunataka
kufahamu wenyeji na kuijua mifugo yao.
Alisema awali ndani ya eneo hilo la Mamlaka ya Hifadhai ya
Ngorongoro kulikuwa na wenyeji wasioupungua 9,000 lakini kwasasa idadi hiyo
imeongeza na kufikia takribani watu 100,000 wanaoishi na mifugo yao ndani ya
Mamlaka.
Akifafanua kuhusu kuwapo kwa taarifa za kulipuka kwa Mlima
Oldonyolengai uliopo ndani ya eneo hilo Waziri Maghembe aliwataka wananchi
kutokuwa na wasiwasi wowote kwa sasa kwani Serikali ipo na itaendelea kutoa
taarifa kwa kila hatua.
“Tunaomba Mungu kulipuka kwake isiwe mbaya sana tunaendelea
kufuatilia kwa karibu bado hatujajua mlipuko wake utakuwa mkubwa kiasi gani.
Tukishafahamu tutawashauri wananchi wajiandae kuondoka eneo hilo.
“Kwasasa wasiwe na wasiwasi, kwani mlipuko wake bado hatujajua
utakuwa mkubwa kiasia gani baada ya vipimo vya Jiolojia vinavyoendelea
kufanyiwa uchunguzi tutawaambia wananchi.
“Kazi ya Jiolojia inafanyika muda wote, ndio maana tulisema
utalipuka ila kiasi gani itatoka, aina gani kwa maana ya moto, vumbi au ujiuji
bado hatutajua. Lakini wananchi waendelee na shughuli zao,” alisema Waziri
Maghembe.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Mudhihiri
Mudhihiri alisema, wamejipanga kutekeleza yale yote waliyokabidhiwa na
kuaminiwa na Serikali.
“Tumejipanga kuongeza nguvu mpya mimi na wajumbe wangu mahiri
tuliochaguliwa mchanganyiko wa watu hawa umenitia matumaini kuwa tutafanya kazi
vizuri,” alisema Mudhihiri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment