Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), katika kipindi cha miaka
miwili ya fedha limeweza kuchangia kiasi kisichopungua Sh.Bilioni 61 katika
Mfuko Mkuu wa Serikali.
Fedha hizo ni sawa na ongezeko la Sh. Bilioni 7, ambapo Mwaka
2015-2016 zilichangwa kiasi cha Sh. Bilioni 27 huku Mwaka 2016 -2017
zikichangwa Sh. Bilioni 34.
Akihojiwa katika kipindi cha “TUNATEKELEZA” kilichorushwa na
Televisheni ya Taifa (TBC) juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA),
Allan Kijazi alisema mafanikio hayo yalitokana na ongezeko la watalii nchini.
Alisema utalii umeendelea kukua kila mwaka kwa ongezeko la
asilimia 4 mpaka 7 na kusababisha mchango katika hifadhi za taifa zinazosimamiwa
na Shirika lisilotegemea ruzuku kutoka serikalini kuendelea kuongezeka kila
mwaka, huku asilimia 80 ya utalii ukitokana na hifadhi za taifa.
“TANAPA tunajitegemea kwa asilimia 100 bila kutegemea ruzuku
kutoka serikalini, hivyo tunatakiwa kuchangia mapato katika mfuko mkuu wa
Serikali.
“Kwetu sisi mapato yamekuwa yakiongezeka ndio maana mchango wetu
nao unaongezeka, na hasa ikichukuliwa sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2
ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni zikitokana na utalii,”
alisema.
Katika mahojiano hayo Kijazi alizitaja nchi zinaongoza kwa raia
wake kutembelea nchini kuwa ni Marekani, Ujerumani, Uingereza, Italia, Ufaransa
na Hispani.
Alisema watalii kutoka nchini Marekani wamekuwa wakipendelea
kutembelea soko la Tanzania kutokana na nchi kuwa na vivutio vya asili na vya
kipekee ukilinganisha na nchi nyingine duniani.
Kuhusu njia wanazotumia kujitangaza alisema awali walikuwa
wakitembelea wadau katika masoko wanayoyalenga, ambapo kwa sasa wanatumia zaidi
mfumo wa digitali kusambaza taarifa kwa wageni na wadau wanaoonyesha nia ya
kutembelea vivutio vilivyopo.
“Tumekuwa tukipeleka taarifa mbalimbali za vivutio vya utalii
kwenye ofisi za balozi zetu ili kuwashawishi wateja. Kwa ujumla tunahitaji
kuongeza juhudi za kujitangaza zaidi kuliko nyuma katika masoko ya nje ya nchi.
“Teknolojia imetusaidia kujitangaza na kuweka wazi vivutio
tulivyonavyo ikiwamo kuondoa uvumi wa propaganda za ushindani wa kibiashara.
Hivi sasa idadi kubwa ya watalii kutoka nje wanaelewa Mlima Kilimanjaro upo
Tanzania,” alisema Kijazi.
Alisema kwamba kwa sasa wamekamilisha mkakati wa kitaifa
unaotaka kuwe na mfuko wa maendeleo ya utalii utakaowezesha vivutio vyote vya
utalii nchini kutangazwa kwa pamoja badala ya kila mmoja kutangaza kivyake.
Akielezea kuhusu matukio ya ujandiri Kijazi alisema matukio hayo
yamepungua kwa asilimia 80 baada ya mamlaka kushirikiana na Jumuiya za
kimataifa kutokomeza soko la bidhaa zitokanazo na ujangiri.
“Ujangiri tumeudhibiti hasa wa wanyama wakubwa kama Tembo na
Faru. Hata ukiangalia idadi ya wanyama waliokuwa wakiwindwa kwa inazidi
kuongezeka kuzaliana na kuonekana,” alisema Kijazi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment