Na ABRAHAM GWANDU
-ARUSHA.
VIJANA wametakiwa kuongeza thamani na ubunifu wa ziada katika
bidhaa wanazotengeneza ili bidhaa hizo ziingie kwenye ushindani na kutumia
masoko ya kibiashara yaliyopo katika eneo la Afrika ya Mashariki.
Akizungumza jana katika kongamano lililoshirikisha vijana
wapatao elfu moja kutoka wilaya zote za Mkoa wa Arusha ,Mkurugenzi wa taasisi
isiyokuwa ya kiserikali ya Foundation For Civil Society Francis Kiwanga alisema
soko hilo ni fursa adhimu ambayo vijana wa Tanzania wanapaswa kuichangamkia.
Pamoja na mambo mengine kongamamo hilo pia lilikuwa na lengo la
kuwaunganisha vijana hao na wadau mbalimbali kutoka nchi zote sita za EAC ili
waweze kujifunza namna ya kuongeza thamani katika bidhaa zao na kuweza
kutumia fursa zilizopo kujipatia soko la uhakika ndani na nje
ya nchi.
Kiwanga alisema kongamano hilo ni hitimisho la kampeni maalumu
ya kuhamasisha vijana wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki
fursa mbalimbali zilizopo.
Alisema kuwa, taasisi hiyo imefanya kampeni ya siku kumi
iliyolenga kuhamasisha vijana kubadilika kifikra na kuachana na maswala
ya kuajiriwa ili waweze kutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa
zao na hatimaye kupata soko ndani na nje ya nchi.
Kiwanga alisema kuwa, lengo la kuwakutanisha vijana hao ni
kuweza kuzitambua fursa mbalimbali zilizopo katika jumuiya ya Afrika mashariki
kwani kama vijana wana nafasi kubwa ya kushiriki katika soko la jumuiya
na kuweza kuinua uchumi wa nchi zetu.
"Lazima kama vijana tuangalie namna ya kushiriki kikamilifu
katika uchumi wa nchi yetu na kuhakikisha tunatoka na kwenda kwa wenzetu wa
nchi jirani katika kuinua uchumi wetu kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo
"alisema Kiwanga.
Naye Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega
alisema kuwa umefika wakati sasa wa vijana kufikiria tofauti nje ya
boksi na kutumia fursa mbalimbali zilizopo nje ya nchi kwa kuhakikisha wanapata
soko la uhakika litakalowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Aliwataka vijana hao kuhakikisha wanawatumia wataalamu
waliobobea katika maswala ya kiuchumi na biashara ili kuongeza thamani ya
bidhaa zao na hatimaye kuweza kupata soko la uhakika .
Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha,
DK Richard Masika alisema katika kuhakikisha kuwa wanaunga mkono
juhudi za vijana kupata ajira wamekuwa wakiwajengea uwezo vijana wa
kitanzania ili waweze kujiajiri kwa kutoa mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na
muda mfupi ambayo yatawawezesha kupata ajira ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa, kwa sasa hivi wemeanza kuwaandaa vijana ili waweze
kupata ajira katika maswala ya gas ambapo wameanzisha programu ya kuwafanya
wahitimu watambulike kimataifa zaidi.
Mwisho .
No comments:
Post a Comment