CHAMA Cha Wanasheria Wanawake
Tanzania,(Tawla) kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Meru,wameanzisha
jukwaa la wanawake katika halmashauri hiyo,kwa lengo la kuwaandaa na kuwajengea
wanawake uwezo wa kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo juzi,Mratibu
wa dawati la uwezeshaji wananchi kiuchumi katika halmashauri hiyo Saumu
Kweka,alisema kuwa jukwaa hilo litawawezesha wanawake kupata sehemu ambayo
wataweza kukutana kwa pamoja na kujadiliana masuala yanayowahusu ikiwemo
upatikanaji wa haki.
Alisema kuwa jukwaa hilo litawawezesha wanawake kuangalia
fursa zilizopo katika maeneo yao ikiwemo fursa za kiuchumi ili waweze kuzitumia
kujiongezea kipato.
"Jukwaa hili litawakutanisha wanawake ambapo wataweza
kujadiliana masuala mbalimbali yanayowahusu,kuangalia fursa za kiuchumi na
tutajitahidi kuwakutanisha wanawake wengi zaidi ili waweze kuchangia katika
shughuli za maendeleo,"alisema Saumu.
Aidha Mratibu huyo alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake
kujiunga kwenye vikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo mikopo
kutoka kwenye taasisi za fedha pamoja na taasisi nyingine ambazo hutoa mafunzo
ya ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake.
Awali Mratibj wa Tawla tawi la Arusha,Cecilia
Ngaiza,alisema jukwaa hilo litasaidia kupunguza changamoto mbalimbali
zinazowakabili wanawake hasa waishio maeneo ya vijijini ikiwemo ukiukwaji wa
haki unaochangiwa na mila na desturi potofu.
"Huu ni mradi wa kukuza upatikanaji wa haki ikiwemo
ardhi kwa wanawake na unalenga kuanzia ngazi za vijiji,kata,wilaya hadi mkoa
lengo likiwa ni kuwasaidia wanawake ili wapate haki zao ambazo wamekuwa
wakizikosa kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mila na desturi
potofu,"alisema.
No comments:
Post a Comment