Saturday, July 1, 2017

MIRERANI-ACHOMWA MWILINI KWA MIFUKO YA PLASTIKI

MAJERUHI wa kuchomwa moto mwilini kwa kutumia mifuko ya plastiki  Joel Efatha (34) amefichua siri ya ukatili huo aliofanyiwa katika mgodi wa madini ya Tanzanite, Simanjiro mkoani Manyara.


Kwa sasa majeruhi huyo aliyechomwa mgongoni na miguuni wiki iliyopita anaendelea na matibabu Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Akizungumza na MTANZANIA hospitalini hapo jana, Efatha alifichua vitendo vya ukatili alivyofanyiwa na mtoto wa mmiliki wa mgodi unaomilikiwa na mchimbaji mdogo aliyejulikana kwa jina la Mama Kikuyu.

Akizungumza kitandani hapo alisema, akiwa kazini Saa 1:30 jioni akiendelea na majukumu ya kazi kuliibuka ugomvi wa kawaida uliotokana na madai ya kutolipuka kwa baruti iliyokuwa imewekwa shimoni.

Alidai ugomvi huo ulitokana na wafanyakazi kumtuhumu kuhusika kuchimbia baruti ambayo haikulipuka hivyo walianza kumgombeza wakishikirikiana na mtoto wa mmiliki wa mgodi aliyetajwa kwa jina moja la Nick.

“Baada ya kuhitilafiana kwenye mambo ya baruti ambazo hazikupilipuka chini ya ardhi, tulianza kugombana kuanzia chini ya ardhi kisha wakaanza kunichoma na vitu vyenye ncha kali,”alidai Efatha na kuongeza:

“Ajabu hata wafanyakazi wenzangu chini ya mgodi walishiriki kunichomachoma na vitu vyenye nja kali kisha kuanza kuniunguza na mifuko ya plastiki mwilini ambayo walikuwa wakiiweka jikoni kisha
kunidondoshea ute wake mwilini,” alidai.

Majeruhi huyo aliyeunguzwa miguu miwili,mgongo,kifua na sikio aliomba Serikali kumsaidia kuwashinikiza watuhumiwa hao wamlipe fidia kutokana na maumivu na ulemavu aliosababishwa.

“Kwa sasa napitia wakati mgumu kwani sintaweza tena kufanya kazi hii, ndio maana naomba msaada kwa serikali nisaidiwe kulipwa fidia kwani mpaka sasa sijui tena nitaishije,”alidai majeruhi huyo ambaye aliyeanza kazi mgodini tangu Mwaka 2000.

Kwa upande wake ndugu anayemuunguza majeruhi huyo, Essau Maturo alisema walilazimika kwenda Mererani na kumhamisha kutoka hospitali aliyolazwa awali kutokana na hali kuwa mbaya.

“Pale Mirerani tulikuta matibabu si ya kuridhisha tuliamua kumhamishia hapa. Na kwa vile wao ndio waliomsababishia majeraha haya watalazimika kumtibu mpaka apone kazi yangu ni kumkagua,”alidai.

Aidha aliiomba serikali kuhakikisha inasimamia migodi hiyo ikiwamo haki za wafanyakazi pamoja na kukemea vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa na wamiliki wa migodi.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara,Fransic Massawe,alisema kuwa jana mtuhumiwa aliondolewa katika kituo cha Polisi Mererani juzi kupelekwa kituo cha Polisi Orkesmet kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

“Mtuhumiwa ameondolewa kituo cha Polisi Mererani na amepelekwa kituo cha Orkesmet makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kufikishwa mahakamani,”alisema Kamanda Massawe.



No comments:

Post a Comment