MGOGORO wa muda mrefu
kati ya wachimbaji wadogo wa Tanzanite na kampuni ya Tanzanite One umezuka tena
na kusababisha hali usalama migodini hapo kuwa tete.
Habari za jana zilisema
mchimbaji mdogo Nembles Mbatia, alifariki dunia jana baada ya kukosa hewa kwa
kile kilichodaiwa kuwa kilitokana na kukosa hewa akiwa mgodini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Manyara, (RPC), Francis Massawe, alithibitisha kifo hicho na kusema
polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
“Taarifa zinaonyesha
alikosa hewa akiwa mgodini, lakini tunachunguza. Uchunguzi wa awali
haujaonyesha kama marehemu alikuwa na majereha,” alisema.
Katika tukio lililotokea
Ijumaa iliyopita, wachimbaji wawili wadogo walijeruhiwa macho na kulazwa
Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi na mwingine Kituo cha Afya cha
Mirerani, wakipata matibabu.
Akizungumzia tukio hilo,
Meneja Mkuu wa mgodi wa Gem & Rock Venture, Joel Saitoti Mollel, alisema
tukio hilo lilitokea majira ya saa 10 alasiri na saa 4 usiku ya Ijumaa
iliyopita.
“Jana (Ijumaa) saa 4
usiku baadhi ya walinzi wa Tanzanite One walipita katika mitoboano na kuingia
katika mgodi wangu na kupiga mabomu ya machozi.
“Katika tukio hilo vijana
10 waliumia, hata sasa wamepiga tena na mmoja ameumia.
Hali hii inatokea kila
wakati tunapokaribia kupata vito, (maarufu kama mawe) hawa wenzetu wakiona
hivyo hufanya ‘mitobozano’ na kuingia upande wetu na kupiga mabomu ya machozi
wakidai ni eneo lao,” alisema.
Kufuatia hali hiyo,
wachimbaji hao wamemuomba Rais John Magufuli, ambaye anawajali wanyonge
kuingilia kati na kuwanusuru dhidi ya unyanyasaji wanaofanyiwa.
Aidha walimuomba Rais
Magufuli kutembelea Mirerani na kusikia mwenyewe kero wanazopata.
Vurugu hizo, zilimuibua
RPC wa Mkoa wa Manyara, Massawe, kutoka Babati hadi Mirerani kukutana na
wawakilishi wa pande mbili hizo katika mkutano uliofanyika Kituo cha Polisi
Mirerani juzi.
Akizungumza na waandishi
wa habari baada ya kikao hicho, Kamanda Massawe, alisema ametoa amri kusitisha
uchimbaji wa vito katika eneo wanalogombea hadi muafaka utakapofikiwa kati yao
na Wizara ya Nishati na Madini.
“Mgogoro huu ni wa muda
mrefu, usipochukuliwa hatua za haraka unaweza kuleta madhara makubwa,” alisema
na kuongeza, “huu ni mgogoro wa mipaka na unatakiwa kushughulikiwa na wizara
husika na sisi tumechukua hatua hii ya haraka.”
Alisema Wizara ya Nishati
na Madini iliunda tume maalum kuchunguza na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo
lakini taarifa bado haijatoka na kufanyika kazi.
Alisema ugomvi uliotokea
wiki iliyopita ulianza baada ya walinzi wa kampuni ya Tanzanite One kurusha
mabomu ndani ya njia ya mgodi ambako wachimbaji wadogo walikuwa wakifanya kazi.
Aidha Kamanda Massawe,
alithibitisha kuwepo kwa majeruhi wawili wa vurugu hizo na kwamba wamelazwa
hospitalini kwa matibabui ya macho.
Kamanda aliweza kuonana
na mmoja wa majeruhi aliyekifikishwa kituo hapo akiwa haoni kabla ya kupelekwa
Kituo cha Afya cha Mirerani.
“Suala la uchimbaji
madini Mirerani ni nyeti kwa sababu eneo hili limechukua idadi kubwa ya watu
kutoka maeneo mbalimbali, hivyo tumeamua kutoa amri kusitisha uchimbaji katika
eneo husika kama hatua ya haraka,” alisema.
Hata hivyo, alisema eneo
hilo linalindwa na kikosi maalum cha polisi kinachofanya kazi ya doria usiku na
mchana.
Mmoja wa shuhuda wa tukio
hilo, Charles Mnyalu, ambaye ni mfanyakazi kiongozi wa wachimbaji wadogo,
alisema wakiwa chini waliona watu wanawafuata kupitia eneo la tobo na baadaye
wakapigwa mabomu kiasi cha wengine kuumizwa.
“Tunayo maganda saba ya
risasi za mabomu ya machozi na maganda matatu ya risasi za mabomu ya kishindo,”
alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha
Wachimbaji wadogo Tawi la Mirerani, Jaffar Bakari Faraji, alisema walikuwa na
rasimu waliyoiandaa ambayo ilikuwa ikielekeza kwamba mmoja anayefanya mtobozano
kwa eneo la mwingine anatakiwa arudishwe nyuma hatua 15.
Alisema rasimu hiyo
iliandaliwa na Kamati ya Usuluhishi wa migogoro inapotokea na akataka hatua
hizo zizingatiwe.
Alisema kwa kuwa
uchimbaji wa Tanzanite unafuata mshazari tofauti na uchimbaji kama wa kisima
cha maji, rasimu hiyo ikizingatiwa inaweza kuleta muafaka.
Kwa upande wake, Mary
Richard, akizungumza katika eneo la mgodi huo alidai wamekuwa wakinyanyaswa
katika shughuli zao za uchimbaji wa vito na hata ununuzi wa magonga (madini
machafu) ambayo wanayauza na kujipatia riziki.
MWISHO
No comments:
Post a Comment