Friday, July 14, 2017

RPC ARUSHA AONYA WANANCHI UKAIDI AMRI ZA MAHAKAMA

KUVUNJWA kwa nyumba (maboma) ya baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kilimatinde, kilichopo Kata ya Moita Bwawani wilayani Monduli kumetokana kudaiwa kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha.

Wananchi hao wanadaiwa kuvamia sehemu ya shamba hilo namba 88, L.O 105358 lenye hekari 1832 linalomilikiwa kisheria na mwekezaji Arusha Art Limited, kisha kujenga maboma kwa ajili ya makazi na mifugo yao.


Akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi hao ofisini kwake mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo alisema, kuondolewa kwa nguvu kulitokana na kumalizika kesi ya msingi ya madai.

Alisema madai ya watu hao kuwa waliondolewa kwa uonevu na dalali wa Mahakama kwenye shamba la mwekezaji yapo kisheria hivyo wanapaswa kurejea mahakamani kukata rufaa badala ya kutuhumu jeshi la polisi lililokwenda kusimamia zoezi hilo.

“Kama wanaona wameonewa warudi mahakamani kukata rufaa kuelezea taratibu zilikiukwa. Mahakama ilitoa amri kwa Dalali wa Mahakama kutekeleza amri hiyo ikiwa ni sehemu ya kazi yake kisheria,” alisema RPC Mkumbo na kuongeza:

“Jeshi la Polisi haliwezi kuzuia uamuzi wa Mahakama, tuliamriwa kwenda kusimamia amani eneo walilotolewa wavamizi. Ni lazima tuhakikishe hakuna madhara au sheria itakayokiukwa kutoka eneo kunakotekelezwa amri ya Mahakama.

“Askari wa Monduli ndicho walichofanya kuangalia usalama na kazi ya Dalali wa Mahakama ikitekelezwa kwa mujibu wa sheria. Hao wananchi wameshindwa kesi, sasa hata kushindwa mahakamani ni sehemu ya haki yako kisheria,” alisema.

Kwa upande Mwekezaji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Art Limited Aatish Sachdev alisema, shamba wanalolimiliki tangu mwaka 1988 lilivamiwa na wananchi hao mwaka 1999.  

“Baada ya majadiliano ya ikiwamo kuzungumza na wananchi hao ambao waligoma kuondoka tangu miaka hiuo tuliamua kwenda mahakamani kudai haki,” alisema Mwekezaji Sachdev na kuongeza:

“Kesi ilisikilizwa kwa miaka 21, juzi hukumu imetolewa ikiwataka wavamizi kuondoka. Hata hivyo waliendelea kugoma mpaka Mahakama ilipotoa tena amri nyingine ya kuwaondoa kwa nguvu kupitia Dalali wa Mahakama,” alisema Mwekezaji.

Alisema pamoja na kutoa hekari 350 kwa ajili ya malisho ya mifugo na ujirani mwema kwa wananchi hao bado waliendelea kuvamia shamba hilo ikiwamo kukata miti iliyokuwa imepandwa pamoja na kuvamia maeneo yaliyoandaliwa kwa uwekezaji.

Naye mmoja wa wazee wa boma lililovunjwa kwenye shamba hilo Lepiral Lukas alikiri kupewa shamba hilo na serikali ya Kijiji cha Moita Bwawani miaka ya 1995.

“Shamba hili nilipewa na serikali ya kijiji lakini sikuliendeleza, kwa sasa nimechoka kusumbuliwa hivyo naiomba serikali inisaidie eneo jingine la kuhamia,” alisema Lukas.

Aidha Mtendaji wa Kata ya Moita Bwawani, Emmanuel Naishitie alinukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni akielezea kuhusu mgogoro huo akidai amri ya kuondolewa kwa wananchi hao ilitolewa na Mahakama Kuu.

“Kumekuwapo mgogoro wa muda mrefu eneo hilo, baada ya amri ya Mahakama Serikali ya Kijiji itakaa kuona kama kuna eneo mbadala watakalopewa wananchi hao,” alisema Naishitie.


No comments:

Post a Comment