ZAIDI ya Sh. Bilioni 1.3 zinahitaji katika awamu ya utafiti
wa kiuchumi na kiteknolojia kwenye mradi wa Kiwanda cha magadi soda, bonde la
Engaruka wilayani Monduli mkoani Arusha.
Tayari utafiti ulishaonyesha uwapo wa magadi soda kwenye
eneo hilo unaofikia mita za ujazo Bilioni 4.7 na kila mwaka ujazo huo
unajiongeza kwa mita za ujazo Milioni 1.9.
Akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Ramson
Mwilangali alisema, wanachosubiriwa sasa ni upatikanaji wa kiasi hicho cha fedha.
Mwilangali aliyeongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama aliyetembelea Kiwanda
cha Kilimanjaro Machine Tools kinachomilikiwa na NDC alisema, kazi ya utafiti huo
inaweza kuchukua takribani Miezi 6 hadi 8.
“Baada ya utafiti wa awali uliobaini ubora na wingi wa
magadi yatakayozalishwa sasa tunaingia kwenye utafiti kuangalia masuala ya kiuchumi
na kiteknolojia katika mradi huu yanaweza kutekelezwa vipi,” alisema Mwilangali
na kuongeza:
“Hapo tutakuwa tumekalisha kiwango kikubwa sehemu ya mradi,
tunachosubiria ni fedha kiasi cha Sh. Bilioni 1.3 tukizipata wakati wowote
tunaweza kuanza awamu hiyo ya utafiti. Lakini pia uzalishaji ifikapo 2020 hadi
2022,”alisema.
Alisema Mita za ujazo Bilioni 4.7 za magadi soda
zilizogundilika katika utafiti wa awali eneo la Engaruka na Selela zinaweza
kutumika kwa miaka 500 ijayo, ukiwa ni mradi mkubwa kutekelezwa nchini.
Alisema baada ya kukamilika utafiti wa kiuchumi na
teknolojia hatua itayofuatia ni utafiti wa athari za mradi katika mazingira na
jamii utakaochukua takribani miezi 4 mpaka 6 au zaidi ikitegemea Baraza la Mazingira
la Taifa (NEMC),litakavyoelekeza.
Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa NDC, alisema kwa sasa Halmashauri
ya wilaya ya Monduli inaendelea na kazi ya kuthamanisha mali zilizopo katika maeneo
mbalimbali ya mradi huo wa magadi soda.
Kugunduliwa kwa kiasi hicho cha magadi soda Engaruka baada
ya Ziwa Natron kuingia kwenye mvutano wa kimazingira na kukwamisha mradi huo
eneo hilo, kunaifanya Tanzania kuwa ya tatu kwa utajiri wa magadi soda, baada
ya Uturuki na Marekani.
Uzalishaji unatajwa utasaidia viwanda vingi nchini kutokana
na malighali hiyo kutumika kutengeneza bidhaa kama vioo, dawa za hospitali,
sabuni, karatasi, nguo na uokaji mikate hatua itakayochochea zaidi ukuaji wa
sekta ya viwanda.
No comments:
Post a Comment