BAADHI ya wafanyabiashara waliopo Kituo
kidogo cha mabasi mjini Arusha wametakiwa kulipa malimbikizo mbalimbali ya kodi
ya pango wanayodaiwa.
Kwa sasa maduka ya wafanyabiashara hao yamefungwa
kutokana na mgogoro wa muda mrefu kati yao na Halmashauri ya Jiji la Arusha
inayodai kodi hizo bila mafanikio kutoka kwa wafanyabiashara.
Akizungumzia madai hayo jana mjini hapa,
Mkurugenzi wa Jiji hilo Athuman Kihamia alisema kwamba, hakuna mgogoro wowote
kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya wafanyabiashara hao.
“Hakuna mgogoro kama inavyoelezwa,kilichopo
maduka yamefungwa wahusika wanadaiwa malimbikizo mbalimbali ya kodi ya pango niwashauri
wakalipie ili waendelee na biashara zao salama,” alisema Kihamia.
Wakizungumzia sakata hilo, wafanyabiashara
hao walisema maduka hayo yamefungwa kwa miezi miwili na watu wanaojiita
wawekezaji wajenzi waliowaamuru kuondoka.
Akizungumza kwa niaba yao Mwenyekiti wa
wafanyabiashara wapangaji, Josephine Shirima alisema, Mei, Mwaka huu watu
waliojitambulisha kama wamiliki wa maduka hayo walifika usiku na kufunga maduka
bila kuelezea sababu zozote.
Alisema kwamba ndani ya kituo kidogo cha
mabasi jijini hapa kuna jumla ya wafanyabiashara zaidi ya 762 wanaotegemea
kipato kulisha familia zao lakini hadi sasa hawajui pakwenda hivyo walimuomba Rais
Dk. John Magufuli kuingilia kati mgogoro huo.
“Tunamwomba Rais Magufuli aingilie kati
mgogoro huu wa muda mrefu sisi wafanyabiashara tunanyanyasika tumejaribu kwenda
mamlaka mbalimbali lakini tumegonga mwamba,”alisema Shirima.
Kwa upande wake Mwenyekiti Msaidizi, Maclean
David alisema Juni 14, Mwaka huu waliingia makubaliano na wawakilishi
wajenzi wa vibanda vya biashara na wawakilishi wapangaji katika eneo lao ambapo
walikubaliana na kumaliza mgogoro huo.
“Tofauti na makubaliano hayo tunashangaa
imekuwa kinyume na sasa tumeamriwa
kuondoka,” alisema David huku akionyesha Hati ya makubaliano hayo iliyosainiwa
na Mkurugenzi Kihamia.
No comments:
Post a Comment