CHUO cha ufundi
Arusha(ATC), kilichopo mjini Arusha kimeanzisha program maalumu ya kukabili
ukosefu wa wataalamu katika fani za Nishati ya gesi viwandani, majumbani,
mafuta na umeme wa maji nchini.
Program hiyo ya
miaka mitatu inatarajiwa kuendeshwa kwa ushirikiana na Serikali ya Canada,
lengo likiwa ni kuzalishali wataalamu wa kutosha katika maeneo hayo.
Akizungumza mjini
hapa jana, Afisa Uhusiano wa ATC Gasto Loseiyo alisema, program hizo
zinaanzishwa kutokana na mahitaji makubwa yanayolikabili taifa hususani kwa
wataalamu hao.
Alisema kuanzishwa
program hizo kumezingatia sera ya taifa ya uanzishwaji viwanda inayohitaji
wataalamu na mafundi wakutosha kwani kukosekana kwa wataalamu hao kumekuwa
kukiligharimu taifa fedha nyingi.
“Ukosefu huo
umesababisha kutegemea wataalamu kutoka nje ili kuendesha mitambo mbalimbali
iliyopo nchini na kujikuta mzigo ukibebwa na serikali,” alisema Loseiyo na
kuongeza:
“Wanachuo watakaodahiliwa kwa ajili ya kozi hizi zinazotokana na
ugunduzi wa gesi nchini watalipiwa sehemu kubwa ya gharama na Serikali huku wao
wakichangia kiwango kidogo tu,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya mitambo chuoni hapo Nicolaus
Mgusa, alisema kutokana na ukosefu wa wataalamu katika maeneo hayo uliilazimu
Serikali kuleta wataalamu kutoka nchini India kwa ajili ya usafirishaji wa gesi
kutoka Songosongo hadi jijini Dar es Salaam.
Alisema kama wataalamu hao wangekuwa wamezalishwa tayari nchini
ni wazi kuwa wangefanya kazi hiyo na hatimaye kupunguza gharama zilizolipwa.
“Hata pia katika mradi wa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
nao watalamu wake wametoka nchini China, hata wale wanaendelea na ujenzi wa
mtambo wa gesi kutoka Lindi,” alisema Mgusa na kuongeza:
“Kwa sasa kuna mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini
Uganda hadi jijini Tanga, mradi huu unahitaji mafundi na wahandisi ni
wazi kuwa program hizi zitasaidia kumaliza tatizo la ukosefu wa wataalamu
wazawa,” alisema.
Naye Mhadhiri katika Idara ya Uhandisi wa Umeme na Nishati
chuoni hapo, Kefa Mkongwe, alisema lengo la program hizo ni kutoa wataalamu wa
kutosheleza mahitaji ya taifa.
“Program hii itawezesha kabisa kuondoa utegemezi wa wataalamu
kutoka nje ya nchi,” alisema Mkongwe.
Alisema kuanzishwa kwa program hiyo ya kipekee kwa nchi za
Afrika Mashariki na Kusini kutoa mafunzo hayo kwa vitendo kutasaidia
kuzalisha vijana wengi zaidi wenye ujuzi.
“Hapa kwetu kwa bahati nzuri tuna miliki kituo cha kuzalisha
umeme cha Kikuletwa kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambacho hiki
kimekuwa msaada kwa mafunzo ya wanafunzi,” alisema Mkongwe.
No comments:
Post a Comment