Friday, July 14, 2017

KESI: AFISA ARDHI AMKAANGA DC WA ZAMANI MAKANGA

SHAHIDI wa kumi katika kesi ya kughushi mukhtasari wa serikali ya mtaa wa Levolosi iliyofunguliwa na mkuu wa wilaya mstaafu ,Dahn Makanga ameiambia Mahakama kuwa hakumbuki iwapo ofisi yake iliwahi kumpatia mlalamikaji huyo nakala ya muhtasari unaobishaniwa mahakamni hapo.


Akitoa ushahidi wake jana mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Arusha Gwanta Mwankuga, shahidi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Diclay Nyato akiwa na cheo cha afisa ardhi Jiji la Arusha aliiambia mahakama kuwa ni Jeshi la Polisi pekee ndio wanaweza kupewa nakala ya nyaraka hizo katika mazingira ya lazima kwa mujibu wa sheria.

Makanga ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Bariadi Mashariki na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma alifungua kesi namba 430 ya mwaka 2016 akimtuhumu mfanyabiashara maarufu Jijini hapa Mathew Mollel kuwa alighushi muhutasari huo ili kujipatia kiwanja ambacho awali kilikuwa mali yake .

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili Mary Lucas uliwasilisha mahakamani nakala hiyo kama uthibitisho kuwa mfanyabiashara huyo alighushi nyaraka ili kujipatia hati miliki ya kiwanja ambacho sio mali yake .

Katika malalamiko yake Makanga alidai mahakamni hapo kuwa ,Mollel ambaye anauhusiano naye kindugu alighushi mukhtasari wa serikali ya mtaa wa Levolosi jijini Arusha na kujipatia hatimiliki ya kiwanja namba 231 kitalu DD kilichopo eneo la  Mianzini jijini hapa.

Akihojiwa na wakili wa upande wa utetezi Ephrahim Koisenge ,Nyato aliendelea kuiambia mahakama hiyo kuwa yeye kama afisa ardhi ambaye ana jukumu la kusimamia masuala yote ya ardhi katika Jijini la alisema ikiwa chombo chochote cha dola au taasisi nyingine ya serikali inahitaji nyaraka inalazimika kutumia utaratibu wa kawaida wa kuandika barua kama mfumo rasmi wa mawasiliano serikalini na sio vinginevyo.

Alipotakiwa kuthibitisha iwapo nakala iliyowasilishwa mahakamani hapo ndio halisi , shahidi huyo alikataa kwa madai kuwa ofisi yake huwa inapokea nakala nyingi  za nyaraka mbalimbali hivyo sio jukumu lake kuthibitisha hilo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 27 mwaka huu ambapo upande wa utetezi unatarajiwa kuwaleta mashahidi watatu wakiongozwa na wakili wao Koisenge ambapo watawasilisha utetezi wao mahakamani hapo.

 Mwisho.




No comments:

Post a Comment