Na JANETH MUSHI,
-ARUSHA
BUNGE la Nne la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA),lililopangwa
kuanza Juni 5, Mwaka huu, huenda lifanyike kutokana na uchaguzi wa wabunge
kutoka nchini Kenya kushindwa kufanyika kwa wakati.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Arusha jana na Spika wa Bunge
hilo Daniel Kidega muda mfupi baada ya kulivunja bunge la tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari Spika Kidega alisema mpaka
sasa nchi tano wanachama zimeshakamilisha uchaguzi wa wabunge wa EALA na
kusalia nchi moja ya Kenya.
Alizitaja nchi ambazo tayari zimeshakamilisha uchaguzi huo ni Tanzania,
Uganda,Burundi,Rwanda na Sudani Kusini ambapo kila nchi imekamilisha uchaguzi
wa wabunge tisa.
“Kenya pekee ndiyo hawajafanya uchaguzi mpaka sasa wa wawakilishi
wao,jambo linaloweza kuchangia kukwama kuanza kwa Bunge la Nne, kwani lazima
wawakilishi wa nchi zote wawepo ndipo bunge lianze,” alisema Spika Kidega
aliyemaliza muda wake.
Alisema EALA imepanga kuwasiliana na Serikali ya Kenya ili
kuomba uchaguzi huo ufanyike haraka hatua itakayowezesha vikao vya bunge hilo
kwenda kwa wakati uliopangwa badala ya kuchelewa.
"Tunaomba Kenya iharakishe kufanya uchaguzi wa wawakilishi
wao,hatutaki tatizo kama lililotokea kwenye Bunge la Pili baada ya kuchelewa
kuanza kwa takribani miezi Sita. Kinachoonekana nchini Kenya ni uchaguzi wa
wabunge EALA kuingiliana na uchaguzi Mkuu,"alisema Spika Kidega.
Akihitimisha mazungumzo yake nje ya ukumbi wa Bunge la EALA
mjini hapa Spika Kidega aliwashukuru waandishi wa habari kwa namna walivyojitoa
kuandika habari za bunge hilo vikiwamo vikao mbalimbali.
Aidha katika kikao hicho cha mwisho,Mbunge wa EALA kutoka
Tanzania,Shyrose Bhanji,aliwasilisha hoja binafsi iliyoungwa mkono na
wabunge wengine, kuhusu maazimio ya kuwepo mtaala wa pamoja wa elimu katika
Shule za Msingi na Sekondari za nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Akiwasilisha hoja hiyo Shyrose alisema kuwa kuanzishwa kwa
mtaala huo wa pamoja utaimarisha ushirikiano katika nchi wanachama na kuwa
itaboresha masuala ya biashara,jamii na ustawi wa kiuchumi kwa ujumla.
Alisema kuwa kuoanisha mitaala kutasaidia jamii kuwa na uelewa
kuhusu jumuiya kwani asilimia 65 ya idadi ya vijana waliopo katika nchi
wanachama,wana uelewa kidogo kuhusu faida za ushirikiano na umoja wa Jumuiya
hiyo hivyo kuna haja ya kuweka mkakati wa kina ili kuendelea kutoa elimu
kuhusu jumuiya ili vijana watambue fursa zilizopo.
Akichangia hoja hiyo Mbunge kutoka Rwanda,Martin Ngoga alisema
kuwa hoja hiyo ni ya msingi na kuwa hivi karibuni nchini Rwanda
kumeshapitishwa sheria kwamba lugha ya kiswahili ianze kufundishwa
mashuleni hivyo masomo kuhusu jumuiya yatakapoanza kufundishwa,itarahisisha
kuwaweka wananchi karibu na kusaidia kusonga mbele.
"Hii ni hoja ya msingi kwani katika mkataba wa uanzishwaji
wa jumuiya,mojawapo ya misingi muhimu sana ni kwamba tuwe na jumuiya ambayo
imejengwa kwenye misingi ya kukubalika kwa watu wa jumuiya.Kwa hiyo ili tuwe na
wananchi wanaoikubali jumuiya na ambao wako tayari kuitetea na kuilinda ni
lazima tuanzie na vijana ambao ndiyo wengi,"alisema na kuongeza
"Somo kuhusu Jumuiya lina umuhimu wake na misingi yake na
likifundishwa kwa kiswahili itakuwa vizuri kama ambavyo tulipitisha
azimio kwamba tufanye lugha ya Kiswahili kama lugha mojawapo rasmi ya
Jumuiya,itarahisisha kuwaweka wananchi karibu,"
Mwisho
No comments:
Post a Comment