Na JACKLINE LAIZER
-ARUSHA
TIMU ya Mwangaza Veterani inatarajiwa kushuka dimbani
kesho (Jumapili) kupambana na Kitambi Noma katika mchezo wa kirafiki
utakaochezwa katika uwanja wa Kitek uliopo Suye nje kidogo ya jiji la Arusha.
Akizungumza mjini hapa jana Katibu mkuu wa Timu ya
Mwangaza Veterani Charles Swati alisema maandalizi kuelekea mchezo huo wa
kirafiki na mahasimu wao umekamilika, na wachezaji wake wapo katika mazoezi
mepesi kujiandaa na mtanange huo.
“Katika kuhakikisha tunatekeleza agizo la Makamu wa Rais
mama Samia Suluhu kuwa inatupasa kufanya mazoezi ili kuimalisha miili yetu
tumeamua kuandaa mchezo huu wa kirafiki ukiwa na lengo la kuhamasisha kila mtu
anahitajika kufanya mazoezi kwa faida yake" alisema Swati.
Alisema lengo lingine la kucheza mchezo huo wa kirafiki ni
katika kuhakikisha wanadumisha mahusiano na urafiki mwema kati ya mfanyakazi na
mfanyakazi kwani wakishirikiana kwa pamoja upendo na ufanisi wa kazi utazidi
mara dufu.
Alisema miili inayojiimalisha na mazoezi inakuwa imara
zaidi ya ile ambayo haijihusishi na mazoezi na wanatumia michezo kuendelea
kupiga vita utumiaji wa madawa ya kulevya.
“Tumeamua kuwaalika timu ya Kitambi noma kwa kuwa ni
maveteran wenzetu ambao na pia tumekuwa na upinzani nao mkubwa katika michezo
hivyo mchezo huo utakuwa na hisia ya aina yake”alisema Swati.
Aidha alieleza kuwa mara baada ya mpambano huo timu ya
Mwangaza Veterani inajiandaa kwenda Babati kuchuana vikali na timu ya
Babati Veterani hivi karibuni.
Timu ya Mwangaza Veteran ninaundwa na wachezaji walicheza
soka miaka ya nyuma wakiwa na lengo la kuwajenga na kuwanyanyua vijana
wanaochipukia katika soka na hivi karibuni Mwangaza veteran ilishuka dimbani
kucheza na timu ya AICC veteran mchezo uliomalizika kwa kushinda mabao 4-2.
Mwisho
No comments:
Post a Comment