Wednesday, May 31, 2017

KWAHERI PAUL SOZIGWA

* Alichokisema miaka 11 iliyopita

Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA

MWAKA 2006 nilifanya mahojiano ya Dakika 60 na nguli wa siasa nchini, propaganda, mtangazaji na kiongozi aliyejitambulisha kuwa ni mzoefu katika mambo ya fujo.


Miaka 11 tangu nikutane na Mzee Paul Sozigwa (84), nyumbani kwake Kurasini, hatimaye Mei 12, Mwaka huu Mungu amemuita akiwa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam.

Mahojiano hayo ya habari na Makala yaliyochapishwa Gazeti la Rai, ambapo marehemu Sozigwapamoja na mambo mengine alichambua kwa uwazi masuala ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Habari na makala ile baada ya kuchapoishwa kuchapishwa chini ya Mhariri Muhingo Rweyemamu, Mkuu wa wilaya mstaafu, Katibu Mkuu mstaafu Yussuf Makamba “alimuhoji’Sozigwa.

Kuhojiwa huko, kulimsukuma afike Sinza Kijiweni ofisi za Rai akimsaka Mwandishi madai yake yakiwa ni kupotosha mazungumzo. Sasa kumbuka hapo unasakwa na mtu aliyejitambulisha mzoezi katika mambo ya fujo.

Sozigwa baada ya kumkosa mwandishi aliyefanya naye mahojiano alilazimika kupeleka kanusho lake lililochapishwa Gazeti la Uhuru la kesho yake.

Hatua hiyo yena ilimuibua Mhariri Rweyemamu kuamuru mahojiano yake yachaandikwe upya neno kwa nenompaka kicheko ili kusisitiza alichokisema marehemu Sozigwa.

Leo baada ya kifo chake nibahati kukutana na Tape hiyo kwenye maktaba yangu na kujikuta nikusukumwa kurejea mahoajino hayo kwa ufupi akiwa anaelezea yaliyoihusu CCM, Vita ya Uganda, Maasi ya wanajeshi na imani waliyokuwa nayo wakoloni mpaka kumpa kazi Kisarawe.

Marehemu Sozigwa aliyesoma nchini Uganda Chuo Kikuu cha Makerere Mwaka 1953 hadi 1957 baada ya kumaliza masomo yake alipewa ajira ya Afisa wilaya (DO) wilayani Kisarawe alikozaliwa.

Alisema wakoloni waliamini kwamba kama msomi angewasaidia kupambana na TANU eneo alilozaliwa, bila kujua wakati huo kumbe Sozigwa alikuwa mwana TANU.

“Nilikata Kadi ya TANU Mwaka 1956, kwa vile wakati huo ukiwa mwanachama wa TANU hupati ufadhili wamasomo “Scholarship” niliificha kwa mwalimu aliyekuwa akifundisha Shule ya Minaki ambayo nilisoma.

“Nilifanya kazi ya DO Kisarawe vizuri nadhani kwa imani hiyo, Wakoloni walinitaka niondoke nikafanye kazi kubwa zaidi ya Propaganda.

“Kazi zote hizo niliteuliwa na Gavana sikuwahi kuomba. Niliondoka Kisarawe kwenda Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) kuwa mtangazaji,” alisema marehemu Sozigwa enzi za uhai wake.

Akiwa TBC iliyokuwa ikikagharamiwa na Uingereza Sozigwa akiwa kiongozi wa Idhaa ya Kiswahili alifanikiwa kuinua hali ya utangazaji akiwa na wafanyakazi wakimo akina Suleiman Hega.

“Bahati nzuri Wakoloni hawakuwahi kugundua ndani ya roho yangu kuna TANU. Na hakika niliyofanya Redioni kwa faida ya Chama changu ni makubwa huwezi kuyasilimulia,” alisema.

Akitolea mfano wa mambo magumu aliyofanya akiwa redio alisema moja ni siku Ian Smith alipotoa maelekezo ya kutangazwa kwa tukio la Rhodesia (Zimbabwe) kupata uhuru kwani alizima Redio kwa sababu alizojua yeye.

Baada yakuendelea na kazi alisema walimuamini hivyo walimpeleka masomo kusomea Shahada ya Mawasiliano mwaka mzima nchini Uingereza.

Alisema baada ya kurejea kutoka masomo aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC na kufanya kazi mpaka siku ya Uhuru akiwa ndiye mtangazaji wa sherehe hizo.

“Baada ya Uhuru nilionekana nafaa kusimamia nchi kwenye mambo ya Propaganda.Mwalimu Julius Nyerere aliniteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Utangazaji.

“Nilifanya kazi hiyo kwa miaka minne na kuifanya redio isikilizwe maeneo ya Afrika Mashariki, nakumbuka wakati ndipo tulipambana na Wakenya nikawaita Manyang’au, hawakunisamehe mpaka leo,” alisema.

Katika muendelezo huo Mwalimu Nyerere aliamua kumchukua kuwa Katibu wake wa Rais, akiwa na jukumu kubwa la kuuelezea ujamaa.

“Nilikuwa natoa dozi ndogo ndogo kila siku redioni kwa dakika tano kuhusu ujamaa mpaka wananchi wakaukubali haikuwa kazi rahisi.

“Kila siku nilitoa hadithi ubunifu huo ulihitaji ujanja wa elimu ya mawasiliano, niliweka hadithi za makabila nikaunganisha na ujamaa, mpaka waliukubali huku wengine wakiwa hawauelewei lakini waliukubali.”

Alisema katika kipindi hicho ndipo aligombea Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya MNEC, kisha kufanikiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu.

Akiwa Ikulu Sozigwa alisema kulikuwa na utaratibu wa kufundishwa mazoezi ya mgambo kupitia maofisa wa Jeshi na baadaye ndipo vita ya Iddi Amini ilipoanza Kagera.

VITA YA UGANDA.

Alisema akiwa kwenye nafasi ya Katibu wa Rais, kuliibuka mjadala wa nani atakayetumiwa kwenye eneo la propaganda ya vita ambapo Mwalimu Nyerere alilazimika kumpeleka tena eneo hilo kutokana na uzoefu.

Alisema kupewa kazi hiyo kulimfanya asikilize Redio Uganda kila siku na kukusanya taarifa ambapo kila asiku jioni alikuwa akizijibu kupitia redioni.

“Wakati wao wakisema moja mimi nilikuwa nasema Saba. Lakini pia nilikwenda mstari wa mbelewa vita kila wiki ili kupata hali halisi ya vita ili nikirejea niwaambie nini wananchi

“Nilikwenda mstari wa mbele wa vita mara 12, nikizungumza na askari kuwauliza wanayoyaona na yanayowakera,” alisema Sozigwa bingwa wa Propaganda.

Sozigwa aliyesisitiza katika eneo hilo la vita kuwa bado ni mwanajeshi mwenye namba na sare za kijeshi baada ya mafunzo ya mgambo alikuwa tayari kurejea vitani wakati wowote ili kuipigania nchi yake.

“Siwezi kurudisha hizi sare mimi ni mwanajeshi, adui akitokea nipo tayari kurudi vitani mazoezi ya siku mbili tu hapa,”

ALICHOFANYA KWA UJUZI

Alisema siku waliyoteka Jiji la Kampala alifika eneo la Mitiana akiongozana na askari sita waliomlinda.

Alisema akiwa hapo kamanda alimpa handaki hata hivyo hakuweza kulala siku hiyo kwani Saa 11 asubuhi milio ya risasi ilianza kusikika.

“Tukiwa pale yaliletwa magari ya Mawaziri waliotekwa na maelekezo yalitolewa wasiuawe, hivyo walinyang’anywa magari. Wenzangu walitaka kunipa gari moja nikawaambia sitaki ntatumia Landrover.

“Saa 1 asubuhi tayari Kampala ilishakamatwa na maelekezo kutoka Ikulu yalikuwa ni kushika Redio. Nilipofika Redio Uganda nilikuta askari wetu tayari wameshaua askari wa Uganda waliokuwa wanalinda Redio.

“Kati ya wale askari walikuwa wamebakia watatu, niliwauliza askari wetu nyine mmekamata redio hawa mbona mmewaua wakati ndio mngewalazimisha watangaze na wangeaminika zaidi na wananchi wao.

“Hawa mngewabana sehemu za siri wakatangaza vita imeisha. Tulijaribu kuwasha mitambo wale askari wa Uganda wakasema hakuna umeme tukavujwa kituo cha mafuta jirani.

“Tuliweka mafuta kwenye Genereta kisha mitambo ya Redio ikaanza kutangaza na tulipotangaza tu shangwe kutoka milimani wananchi walifurahia na kusema Kampala imechukuliwa na Watanzania,” alisema Sozigwa.

MAASI YA ASKARI

Alisema Mwaka 1964, ilikuwa hali ya hatari kwani askari wetu wakati huo walikuwa wanataka “Africanization” utawala wa kiafrika mpaka majeshini wakati Serikali ilikuwa bado haijajiandaa.

Alisema asakri hao walikuwa na hoja kwani walitaka kuona askari wazawa wakiwa na vyeo jeshini badala ya kuwaachia wazungu, walituhoji kwanini wasipatikane watu kama akina Nyirenda.

Kutokana na mafunzo aliyopata yaliweza kumsaidia kuokoa jahazi hilo la maasi ya askari wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Wizara.

Alisema siku hiyo askari hao walikuwa wamefanya fujo Redioni kisha kutuma baadhi yao kwenda nyumbani wake kukutana naye wakitaka akawashe redio ili watangaze kero zao.

“Walipofika kwangu wakauliza hii ndio nyumba ya Sozigwa, nikawaambia ndio mnasemaje wakasema wanataka nikafungue Redio.Niliwauliza kwani kuna nini wakashangaa, kwani wewe hujui?”

“Niliwauliza kuna nini, wakaniambia wanamalalamiko yao kama skari basi tukaondoka mpaka Redio Tanzania pale nikakuta askari wamezingira jengo lengo lao mmoja wao aseme dunia isikie.

“Ukweli walikuwa na hoja na wangefanikiwa sisi tungepeta taabu, basi mimi na fundi wangu mitambo tukaingia studio na askari watatu waliopangwa kuzungumza.

“Tukiwa mle nikamwambia fundi mitambo wangu Richard Max afungue mitambo kisha apige wimbo wa taifa atakaposkia nimeanza kupiga wimbo wa canal bog basi azime mitambo.

“Kulikuwa na Meja mmoja nikawaita, nikawaambia mtaka kusema maneno gani haya semini hapa kwenye Tape Recorder walisema maneno mabaya matusi makubwa nikayarekodi dakika tatu.

“Baada ya hapo nikawauliza mmemaliza? Wakasema ndio, nikaweka kwenye mashine kisha nikaanza kupiga ile “canal bog” ilipoisha tu nikafungua Tape hapo askari wakaskia kumbe kule kwenye Transmitter fundi alishazima.

“Askari waliokuwa ndani studio wakawaanza kuwaambia wenzao mmesikia tumezungumza basi ndio ikawa mwisho wa mchezo, wakasambaa kurejea makwao, wakijua mambo yametangazwa kumbe hakuna,” alisema Sozigwa.

Alisema wakati huo mwalimu Nyerere alikuwa mafichoni, hivyo baada ya kumaliza mchezo huo alirejea alikutana na Sozigwa aliyemwelezea tukio zima.

“Nilimwambia Mwalimu Nyerere, mimi kwenye jambo lenye maslahi kwa nchi na Chama changu siangalii maisha yangu. Nikamwambia lazima na yeye aseme jambo. Hivyo Saa 1 jioni baada ya habari akasema maneno akiwa Ikulu.

“Na kuanzia pale ndipo Mwalimu akapandisha wadhifa Generali Sarakikya kuwa Mkuu waMajeshi hiyo ndio faida ambayo niliipata kutoka kwa wakoloni wakidhani wameniweka pale niwasaidie kumbe naisaidia nchi yangu.”

AZIMIO LA ARUSHA

Akielezea kuhusu Ujamaa Sozigwa alisema Ujamaa ni imani, kwani si wengi wanaupenda ujamaa sasa hivi. 

Kwasababu ujamaa maana yake ya msingi ni wewe uliyenacho kupunguza kidogo uwape wasionacho, ukubali mlingane katika hali ya maisha.

Alisema katika vikao vya Kamati Kuu wakati ule walikubaliana kuwa binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima.

“Ninavyoona mimi dira hiyo ni kama imepungua kidogo, tamaa sasa ya mali ya kumzidi mwingine ni kubwa sana kila mahali, hata ndani ya CCM.

“Maana kwa nafasi yangu ndani ya CCM nimegundua kuna wanachama wa CCM si wachache ambao wamepata nafasi zao kutokana na fedha walizotumia, sio wachache, sijasema wengi.

“Hili tatizo naliona kweli kweli, mimi mwenyewe mniligombea Nafasi ya NEC kwa mara tatu nikashindwa kwasababu sikuhonga na mimi nikasema sintahonga.

“Nikasema chukueni cheo chenu sitaki kuhonga, siwezi kuhonga kwa ajili ya kutafuta cheo au nafasi ya madaraka ili uonekane una cheo. Nami nilijua kabisa ninatashindwa na watu waliohonga.

Alisema masuala hayo ya kuhonga ili kupayta vyeo yalikuwa yakimkera sana lakini kwa vile hakuwa kwenye vikao vya maamuzi hakuwa na namna ya kufanya.

“Mimi ni Mwenyekiti wa Shina namba Tatu la Minazini, Mjumbe wa Kamati ya siasa ya Tawi langu hapo nina kauli, hapa kwenye tawi langu mtu hapenyi kwa rushwa nitasema,” alisemaSozigwa.

VYAMA VYA UPINZANI

Nimesoma Katiba chache za vyama vya upinzani ni nzuri sana nimesoma ya Chadema ni nzuri sana, ya CUF ninayo mezani.

Alisema kwa malengo Katiba hizo zinaonekana ni nzuri, lakini utekelezaji wa malengi bado si mzuri.

Sisi tulifungua milango ya vyama vingi ili kukwepa kugandisha mawazo ya wana CCM kwa kukosa mtu wa kuchokonoa na kufikiri pale ambapo mawazo hayakufikiria.

“Nilishiriki katika uamuzi huo nikiwa Jumbe wa Kamati Kuu ya CCM, sasa vilivyo leo sivyo badala yake vimekuwa na mawazo ya kiuhasama. Badala ya kuwa na upinzani makini unaopingana kwa sera na si kuchukiana.

Akimzungumzia Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema alisema angalau kiongozi huyo amekuwa na siasa zenye mlengo mzuri, hata alipokuwa Mwenyekiti Edwin Mtei ambaye walisoma Tabora kisha Chuo Kikuu cha Makerere.

BAADA YA UTUMISHI

Alisma matarajio yake makubwa kabisa ni katika sekta ya kilimo kwani anapenda kulima.

“Nitatafuta fedha za kutosha ili nilime ninalo shamba hekari 20 Msongola wilayani Ilala, kwani huko hugombani na mtu zaidi ya Nguruwe.”  

Hata alipoulizwa kuhusu kushindwa kifanikiwa kwa kilimo cha jembe la mkono, Sozigwa alipinga na kusisitiza kilimo hicho kinafanikiwa isipokuwa tu kama huna mtaji.

“Kilimo cha mkono ni kizuri kuliko hata kutumia trekta kwasababu trekta linaharibu ardhi na kuifanya ife haraka wakati jembe la mkono halifiki mbali.

“Lakini pia gharama lita moja ya mafuta ni sawa na kibarua mmoja, unajua watu wengi wapo kijijini sasa kutumia treka unawanyima wengi kukulimia kwa mikono ili wajifunze.

“Lakini ukilima kwa trekta wale wataendelea kuwa vibarua wako miaka yote, wakati wakilima kwa mikono wataiga ili nao waende kulima,” alisema Sozigwa.

UKARIBU NA NYERERE

Akizungumzia ukaribu wake na Mwalimu Nyerere, Sozigwa alisema moja ya mambo ambayo yaliwaumiza lakini hawakuwa na namna zaidi ya kufanya ilikuwa ni kutaifisha mali za watu na kuzifanya kuwa za Serikali.

“Mambo yake yalikuwa magumu nikiwa na Mwalimu aliweza kutaifisha mali za mabepari, bepari ni bepari tu hana rangi. Lakini mabepari wengine walikuwa ni wana TANU kabisa na wana Kadi lakini ni mabepari.”

“Kwa hiyo wakati anataifisha ilikuwa ni jambo gumu kulifanya kwani kulikuwa na marafiki zetu wengine wa kiasia kama akina Sir Chande, wale walinyonya kwa ruhusa ya Serikali.

“Lakini kwasababu ya sera mpya za ujamaa ilikuwa ni lazima kutaifisha mali zao na wakati mwingine kuna wengine walikuwa msaada mkubwa kwa TANU.” alisema Sozigwa enzi za uhaki wake katika mahojiano nami

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment