Na MWANDISHI WETU
-SIMANJIRO
ASKARI Polisi wilayani Mirerani wilayani Simanjiro mkoani
Manyara wanatuhumiwa kuwafyatulia mabomu mawili ya machozi wachimbaji wadogo
waliokuwa chini ya mgodi takribani Mita 240.
Wachimbaji hao Saba walikuwa mgodi namba P.M.L 0000049 Kitalu D
unaomilikiwa na Theresia Wapalila walikumbwa na tukio hilo lisiloruhusiwa
kisheria baada ya kutoboza eneo la Delta Kitalu C linachomilikiwa na Kampuni ya
Tanzanite One.
Kutokana na tukio hilo baadhi ya wachimbaji kwenye mgodi huo
walikamatwa na askari polisi na kufunguliwa taarifa ya kipoli kwa ajili ya
kupatiwa matibabu kutoka Kituo cha Polisi Mirerani.
Wakizungumzia tukio hilo juzi Mirerani wachimbaji hao walidai
kitendo cha kupigwa mabomu chini ya ardhi ikiwamo kuharibu mundombinu ya umeme,
kunyang’anywa vifaa vya kazi kimewaathiri zaidi kisaikolojia pamoja na afya
zao.
Wachimbaji waliokamatwa na kufikishwa kituo cha polisi kisha
kupewa fomu ya matibabu ni Boxer Dennis (35), Phillipo Paul (31), Ramadhani
Hamza, Hamis Hassan (30), Edmund Mosha, Benjamin Shakoti (47) na Emmanuel Afred
(25)
Akizungumza kwa niaba yao Meneja wa Mgodi huo Frank Mushi
alisema vitendo hivyo vya kupiga mabomu na kutembea na silaha za moto chini ya
migodi vimekuwa vikifanywa na askari polisi wanaotumia na mwekezaji wa
Tanzanite One.
Alisema siku ya kutekwa kwa wachimbaji hao askari hao polisi
wakiwa na maofisa wa Tanzanite One walizama chini ya mgodi wakiwa na silaha za
moto na mabomu ya machozi ambapo katika purukushani hiyo vijana wawili
walinusurika na kuja kutoa taarifa.
“Hiki ni kilio kwetu pindi tunapotobozana wamekuwa wakitumia
nguvu kubwa kinyume na sheria kwani wanatumia uporaji wa vifaa vya kazi. Tangu
tumeanza kazi kwenye hii Shafti tulifikisha Mita 240 na tayari tulikuwa
tumeanza kufanya uzalishaji.
“Tukarudishwa nyumba na kubaikiziwa Mita 30 kutoka kwenye sehemu
tunayoiita kiraka ili tubadili muelekeo, tuliwaambia kwanii waturudishe mita
zote hizo wakati inatakiwa kurudi Mita 10 au 15 nyuma,” alisema Mushi.
Akizungumzia tukio hilo Mkurugenzi mwenza wa Tanzanite One
inayochimba kwa ubia na Serikali kupitia Shirika la STAMICO, Faisal Juma
alisema, changamoto kubwa inayojitokeza ni kwa wachimbaji wadogo kushinda
kutambua mipaka na kuheshimu sheria.
“Mgodi ule si wa kwetu pekee pale tunachimba kwa ubia na
Serikali kupitia STAMICO. Hivyo ni lazima vyombo vya Dola viwepo ili kusimamia
maslahi ya umma na kuona yakilindwa.
“Sasa kwa eneo la Delta ambalo hawa wanalalamika kuwa lilikuwa
halichimbwi hiyo si sababu sasa hivi limeanza uzalishaji na linamilikiwa
kisheria na Tanzanite One. Ni kweli wachimbaji wadogo katika harakati zao za
kuchimba wanapitiliza na kuingia eneo hili.
“sisi na serikali kwa pamoja tunayo haki ya msingi ya kusimamia
maeneo hayo yawe salama.Uamuzi unaochukuliwa mara nyingi ni wa kuwarudisha
nyuma ambao umekuwa ukilenga usalama mgodini na kulinda maslahi ya serikali na
mwekezaji,” alisema Juma.
Naye Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Adam Juma
akizungumzia kitendo hicho alisema kwamba licha ya sheria ya madini
kutozungumizia suala mabomu chini ya ardhi bado wao kama Wiara hawaruhusu
kufanyika kwa vitendo hivyo.
“Hatuhitaji kutumia nguvu kubwa ya kuwapiga Watanzania mabomu ya
machozi chini ya ardhi kwasababu tu ya mtobozano wa uchimbaji suala hili
linahitaji mazungumzo zaidi.
“Hata hao Tanzanite One tulishawapa maagizo ya maandishi kwamba
hairhusiwi kutumia risasi za moto chini wala mabomu.Sisi tuna ofisi pale
Mirerani wanatakiwa kwenda kutoa taarifa muda wowote na tumekuwa
tukishawashauri kufanya mazungumzo badala ya kutumia nguvu.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment