JUHUDI, ujasiri na uimara wa kusimamia rasilimali za Taifa
zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, zitawawezesha Watanzania kuanza kula
‘Siagi’ kama ilivyo kwa wananchi wa nchi zilizoendelea.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Askofu Mkuu wa Kanisa la
International Evangelism Dk. Eliud Issangya alipozungumzia hatua madhubuti za
kusimamia rasilimali za nchi zinazoendelea kufanywa.
Rais Magufuli hivi karibuni alipiga marufuku kusafirishwa kwa
mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi na kuunda Tume mbili zilizoichunguza
kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Accacia.
Taarifa za Tume hizo mbili zimekuwa na matokeo yaliyowaacha hoi
wananchi kutokana na kuonyesha namna taifa linavyoendelea kuibiwa kupitia sekta
hiyo ya madini tangu Mwaka 1998.
Akizungumzia matokeo hayo, Askofu Dk. Issangya alisema Kanisa la
International Evangelism limempongeza kwa dhati na kuendelea kumuunga mkono
Rais Dk. Magufuli.
“Tunatangaza kusimama naye kwa dhati na kumuunga mkono Rais
katika jitihada na uthubutu wake wa kutetea haki za wanyonge,” alisema Askofu
Dk. Issangya na kuongeza:
“Kwa juhudi hizi Tanzania itaingia katika kundi la nchi tajiri
duniani na itawezesha wananchi wake kuanza kula ‘Siagi’ kama ilivyo kwa raia wa
nchi zilizoendelea,” alisema.
Alisema kitendo cha kuhakikisha anasimama kidete kuzuia na
kulinda rasilimali za taifa zilizokuwa zinaendelea kuporwa na kuhamishiwa nje
ya nchi kutaanza kulinufaisha taifa na wananchi wote.
“Namuhakikishia rais kwamba tunamuombea na tunaomba wale wote
waliochukua mali zetu sas waanze kurudisha, kwani hata sisi tunahitaji fedha,
hakuna mtu asiyehitaji fedha kwa maendeleo ya wananchi wake.
“Mali ya nchi yetu ilikuwa imetoroshwa, tunazungumza tukiwa na
hisia za rasilimali zetu tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu, waliochukua mali zetu
warudishe,tukazijengee hospitali,barabara na huduma nyingine za kijamii”
alisema Askofu Dk. Issangya.
Askofu Dk. Issangya aliendelea kusisitiza na kumuomba rais
kuhamishia juhudi hizo katika sekta ya wanyama pori na maliasili kwani limekuwa
moja ya eneo linalotuhumiwa kuhujumu rasilimali za wananchi.
Aidha mbali na maeneo hayo Askofu huyo alimuomba pia kuliangalia
eneo la wanchimbaji wadogo nchini ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisukumwa na
kuondolewa kwenye maeneo yao ili kuwapisha wawekezaji wasio na uchungu kwa
taifa.
“Wachimbaji hawa wadogo ndio wanaobakiza fedha yao nyumbani
tunamuomba waangalie kwa kuwapatia maeneo rasmi ya kuendelea kuendesha shughuli
zao za kutafuta riziki,” alisema Askofu Issangya.
“Nitoe wito kwa Watanzania wote tuendelee kumuunga mkono rais
katika mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma,”
alisema.
No comments:
Post a Comment