JAPHET Legimani (37) Mkazi wa Daraja Mbili jijini Arusha amepandishwa
katika Mahakama ya wilaya ya Arumeru, kwa makosa ya kufanya mapenzi na watoto
wake wawili wa Darasa la Sita na Kidato cha Kwanza.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,Patricia Kisinda,Wakili
wa Serikali,Riziki Maayu,alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo kati
ya mwaka 2016 na 2017 kwa watoto wake wenye umri wa miaka 14 na 12.
Katika kesi ya kwanza,Legimani anadaiwa kufanya mapenzi na ndugu
wa damu,kinyume na kifungu cha 158 (1), cha Sheria ya Kanuni ya adhabu
ambapo katika tarehe tofauti Mwaka 2016 katika maeneo ya Daraja 2,alifanya
mapenzi na mtoto wake (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka
14,anayesoma kidato cha kwanza jijini Arusha.
Riziki alidai mahakamani hapo kuwa katika kesi ya pili, Legimani
anadaiwa kufanya mapenzi na ndugu yake wa damu ambapo anadaiwa katika tarehe
tofauti kati ya mwezi Januari hadi Mei Mwaka huu alifanya mapenzi na mtoto wake
(jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 ambaye anasoma darasa la 6 katika
moja ya shule za msingi jijini hapa.
Mshitakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo na Wakili huyo wa
Serikali aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na
kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kuitaja kesi hizo.
Hakimu Patricia alimweleza mshitakiwa huyo kuwa dhamana iko wazi
ambapo alitakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni waajiriwa wa taasisi
inayotambulika na mahakama na kila mdhamini kusaini dhamana ya Sh Milioni 5 na
kuwa mshitakiwa huyo akikidhi masharti ya dhamana hataruhusiwa kutoka nje ya
Arusha bila ruhusa ya mahakama.
Kesi zote mbili ziliahirishwa hadi Juni 28 Mwaka huu
zitakapotajwa tena na mshitakiwa huyo na amerudishwa mahabusu baada ya kukosa
wadhamini.
No comments:
Post a Comment