MAJERUHI watatu wa
ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent waliopo nchini Marekani kwa matibabu
zaidi hatimaye wameanza kujihudumia wenyewe ikiwamo kuoga.
Majeruhi hao walipata ajali Mei 6, Mwaka huu wilayani Karatu
huku wanafunzi wenzao 33, walimu wawili na dereva wakipoteza maisha kwenye
ajali hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook Mbunge Singida Kaskazini (CCM)
na Mwenyekiti mwenza wa Shirika la STEMM Lazaro Nyalandu alisema jana kuwa
madaktari wamejiridhisha kuhusu maendeleo ya kupona kwa mifupa ya watoto hao.
Alisema Sadya Awadh na Wilson Tarimo walipelekwa Kituo cha CNOS-(Center
for Neurosurgery Orthopedics and Spine) Jimbo la Dakota Kusini ambako madaktari
walijiridhisha na maendeleo ya kupona kwa mifupa hivyo wakawatoa bandeji ngumu.
“Sadia na Wilson wameondolewa "Cast" walizokuwa
wamewekewa na sasa wanaweza kujiogesha wenyewe kwa mara ya kwanza tangu
wafikishwe hospitalini,” alisema Nyalandu kupitia ukursa wake wa Facebook.
Kwa upande wake Muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru Symphrosa Silali aliyeongozana na majeruhi akimzungumzia majeruhi Doreen Mshana aliyefanyiwa upasuaji katika uti wa mgongo alisema afya yake inaendelea kuimarika.
“Jumatatu wiki hii alitolewa pini kwenye mkono wa kushoto lakini
pia ameweza kuchezesha mguu wake wa kulia hatua inayo onesha matumaini katika
uponaji wake,” alisema kupitia ukurasa wa facebook wa Nyalandu.
“Watoto wote wanafanya mazoezi mara tatu kwa wiki, wapo
watalaamu pia wanaowafanyia mazoezi ya namna gani wanaweza kukabiliana na vitu
vilivyokuwa mbele yao ili waweze kuvisahau.
“Lakini pia kuna mazoezi ya viungo yanayowezesha viungo vyao
kuendelea kuzoea kutumia mikono, miguu yao. Lakini pia wanafundishwa kufanya
vitu vidogo vidogo wenyewe kama kupiga mswaki, kuoga na kuvaa nguo.
‘Jumatano watoto wote wametolewa mihogo na wanaendelea vizuri
hatau ambayo imewawezesha kutumia viwiko vya mikono vizuri ikliwamo kuendelea
na kufundishwa namna ya kukunja mikono na kuinyoosha,” alisema Silali na
kuongeza:
“Mazoezi haya ni madogo yanaendelea kuwajengea uzoefu wa
kujitegemea Lakini kwa upande wa Doreen yeye bado ni tofauti kidogo na
wenzake kwani mkono wake wa kulia alikuwa akifundishwa kutumia misuli yake ili ukae
vizuri pamoja na mguu wa kushoto.
“Na anaendelea kufundishwa namna ya kukaa kwani bado anahitaji
msaada wa kukaa. Kwa kweli tunashukuru kwa maombi ya Watanzania wanaoendelea
kutuombea tangu tulipofika hapa Marekani,” alisema.
Aidha Muuguzi huyo aliushukuru pia Ubalozi wa Tanzania nchini
Marekani kwa kuwa karibu yao na kuendelea kuwasaidia wakiwamo pia Watanzania
waishio Marekani ambao nao wamekuwa wakiwatembelea na kuwasaidia kwa kila
namna.
No comments:
Post a Comment