Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA
SERIKALI ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya (KFW),
imetoa kiasi cha Euro Milioni 2.9 kwa ajili ya shughuli za upembuzi yakinifu wa
Barabara ya Arusha hadi Mara kupitia mkoani Simiyu.
Barabara hiyo inayotarajia kubadilisha maisha na uchumi wa
wananchi sasa itapita katika maeneo ya wilaya ya Karatu, Mbulu, Singida,
Lalago, Kolandoto mkoani Simiyu kisha kuingia Mara.
Ujenzi wa barabara hiyo uliopangwa awali kupita katikati ya
Hifadhi ya Serengeti, lakini Mashirika na Asasi za kiraia duniani zinashughulika
na mazingira zilipinga mradi huo zikidai utaathiri Ikolojia ya Hifadhi ya
Serengeti.
Akizungumza wakati wa mkutano ulioshiikisha wadau kutoa maoni
yao juu ya kuanza kwa upembuzi yakinifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo aliwataka
wadau kutoa mapendekezo makini yatakayolenga mambo
muhimu ya kusaidia mradi kuwa na tija
kwa wananchi na Taifa.
“Tunaihitaji barabara, pia
uhifadhi ni muhimu na tunauhitaji. Lazima tuhakikishe mambo haya yote
yanawekwa bayana na kujadiliwa kwa kina ili
kuhakikisha mradi unakuwapo lakini pia rasilimali zinakuwa
salama,” alisema Gambo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi ya Barabara kutoka Wakala
wa Barabara nchini (TANROAD), Makao Makuu Crispin Ako alisema, kazi ya upembuzi huo
imeshaanza na inatarajiwa kukamilika ifikapo June
Mwaka, 2018.
Nao baadhi ya wadau waliohudhuria majadiliano hayo akiwamo Mkuu
wa wilaya ya Maswa inakopita barabara hiyo Dk. Seph Shekalage alisema,
ujenzi wa barabara hiyo utainua hali za kiuchumi za wananchi hao.
“Maeneo mengi ambako barabara hii itapita kuna fursa
nyingi za wananchi kuwekeza na hatimaye kukuza kipato
chao, huko kuna wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilima na mazao yao
kushindwa kuyafikisha sokoni kwa wakati,” alisema Dk. Shekalage na kuongeza:
“Tunaamini fursa sasa zinakwenda kufunguka kwa wananchi wa
maeneo hayo ili nao waweze kujiongezea kipato na kupata maendeleo kupitia
barabara,” alisema.
Akiwa pia ni mtaalamu katika eneo la afya Dk. Shekalage alisema
ujio wa barabara hiyo utakuwa pia muhimu na faida kubwa kwa wananchi walioteseka
kwa miaka mingi kwa kushindwa kufika katika hospitali za kisasa kutokana na
miundombinu mibovu.
Naye Mtaalamu wa masuala ya Uhifadhi Gerald Bigurube
alionyesha kufurahishwa na barabara hiyo kupita kwenye mikoa ambayo haihusishi
Hifadhi ya Seerengeti kama yalivyokuwa mapendekezo ya awali.
“Kwa sasa hakuna eneo litakaloharibu
uhifadhi wala kugusa ikolojia ya viumbe
wengine wakiwemo wanyamapori,” alisema Bigurube na kuongeza:
"Kubwa hapa ni maeneo kama ya wilaya ya Mbulu
ambayo kwa miaka mingi licha ya kuwa na
fursa kubwa za kilimo bado maendeleo yaliendelea
kudororo kutokana na kukosa miundombinu bora ikiwamo
ya barabara,” alisema.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment