Na JANETH MUSHI,
-ARUSHA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (Tanapa),limepongezwa kwa
kuitikia wito na kuwasaidia wawekezaji wazawa kuwekeza ndani ya Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti,hatua iliyochangia kuongeza wigo wa kufanya biashara na
kukuza utalii.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Umoja wa
Waongoza Watalii Tanzania (Tato),Wilbard Chambulo,alipokuwa akizungumza katika
maonyesho ya utalii ya 'Karibu Travel Market Fair',yaliyofanyika katika viwanja
vya Magereza,vilivyopo eneo la Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Chambulo alisema kuwa Tanapa imewasaidia kuwekeza na kupanua
wigo kibiashara tofauti na miaka ya nyuma ambapo hadi sasa kuna
kambi za kitalii 138 katika hifadhi hiyo ambazo zote ni za wawekezaji wazawa.
"Serengeti tunafanya nao kazi vizuri kwelikweli ninafikiri
watu wote wanafahamu hapa,Tanapa kwa ujumla nawapongeza kwa kuitikia wito na
kutusaidia sisi hasa watanzania kuwekeza ndani ya hifadhi ya Serengeti,kule
tuna kambi nyingi"alisema na kuongeza
"Unajua sisi waswahili unakuwa na Dola za Marekani 10,000
au 20,000 unanunua vihema vyako,unapiga kule unafanya biashara,hadi sasa
biashara imepanuka leo kule Serengeti tuko 138 tumewekeza,hii ni habari nzuri
tunaishukuru Tanapa na juhudi za serikali kwa ujumla,kwani imetuongezea wigo wa
kufanya biashara,"
Kiongozi huyo aliwataka wadau wa utalii kuhakikisha wanafanya
biashara zao kwa kuzingatia na kufuata kanuni na sheria ikiwa ni pamoja na
kulipa kodi,kukata leseni na kuwa Umoja huo hautakuwa tayari kumtetea
mfanyabiashara anayekiuka sheria au taratibu zilizowekwa.
Awali akizungumzia sekta ya utalii,Waziri wa Maliasili na
Utalii,Prof Jumanne Maghembe,alitaja changamoto nyingine inayoikabili sekta
hiyo ambalo inaendelea kuwa kubwa ni kuingizwa kwa idadi kubwa ya mifugo katika
hifadhi hasa mifugo kutoka nchi jirani.
Alisema katika hifadhinza taifa hapa nchini mifugo mingi
inayochungwa ndani ya hifadhi inatoka nchi za jirani,akitolea mfano upande wa
Magharibi mwa Tanzania asilimia 68 ya ng'ombe waliopo kwenye hifadhi wanatoka
kwenye nchi moja ambayo hakuitaja,huku asilimia 27 nyingine wakitoka kwenye
nchi nyingine.
"Tumezidiwa na tatizo la kuchunga ng'ombe kwenye
hifadhi,hili ni tatizo kubwa,mtalii hawezi kutoka Scotland anakuja kuona
pundamilia badala yake anaona punda au ng'ombe huku kiingilio kwenye hifadhi
kikiwa Dola za Marekani 200 halafu wanachoona ni ng'ombe,unajua siyo vizuri
lazima tushirikiane tumalize tatizo hili,"alisema na kuongeza
"Lazima tujue kitu kimoja,hawa wenye mifugo siyo ya watu
nje ya jamii yetu na lazima na wenyewe tushughulike nao vizuri.Siyo leta kiboko
chapa ondoka,hapana lazima tulimalize kwa kushirikia na ndani ya kipindi cha
mwaka mmoja na nusu ujao liwe limeisha,"
"Hao wafugaji wa nje wanaona hapa kwetu tuna ardhi ni
shamba la bibi,kwa hiyo hii hatuwezi kuvumilia hawa lazima waondoke,hivyo
lazima tufikirie namna ya kushughulika na wa kwetu wanaobaki,maana na wenyewe
iko shida,na kuangalia namna ya kusaidia mahitaji ya watu wenye mifugo lakini
hawana mahali pa kuchunga,"alisema Profesa
Kuhusu ujangili alisema serikali inapambana na tatizo hilo kwa
kiasi kikubwa na kuwa hadi sasa watuhumiwa 966 bado kesi zao
zinaendelea,huku katika kipindi cha mwaka 2016-2017 walihukumiwa zaidi ya watu
276 na vifungo vyao vikiwa kati ya miaka 12 hadi 30 na wengine
kifungo na wakitoka walipe faini ya Dola za Marekani Milioni 54.
Mwisho
No comments:
Post a Comment