Wednesday, May 31, 2017

GAEY ATAMBA MBIO ZA BOLDER BOULDER

NA JACKLINE LAIZER
-ARUSHA

MWANARIADHA Gabriel Geay wa Tanzania amelamba kitika cha Dola 8000 baada ya kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika mashindano ya mbio za Km 10 za Bolder Boulder zilizofanyika juzi nchini marekani.


Geay alifanikiwa kuchukuwa kitika hicho baada ya kutumia muda wa dakika 29:02:19, huku mshindi wa pili ni Leonard Korir wa nchini Marekani yeye alitumia dakika 29:02:81 na mshindi wa tatu ni Sam Chelanga nae wa nchini Marekani alitumia dakika 29:07:66.

Akizungumza mjini hapa Katibu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Wilhelm Gidabuday alisema wanariadha watatu ndiyo walikwenda kuwakilisha nchi katika mashindano.

Aloiwataja wanariadha wengine kuwa ni Ismail Juma aliyeshika nafasi ya 18 na Josephat Gisemo aliyemaliza katika nafasi ya 20, huku katika matokeo ya jumla Tanzania imeshika nafasi ya nne.

"Nawashukuru wanariadha wote wanaofanya vizuri katika mashindano mbalimbali kwani fursa tunazowatafutia wamekuwa wakuzitumia vizuri kwa kupata  ushindi, ila ninatoa onyo kali kwa mwanariadha yeyote ambae chama kinamtafutia mashindano halafu anakataa kwenda kushiriki kwani huo ni utovu wa nidhamu na hautakubalika" alisema Gidabuday.

Alisema mwanariadha yeyote ajira yake ni mbio  na muda wowote lazima awe tayari katika mashindano yatakayoweza kujitokeza mbele hivyo ni nini sababu ya mwanariadha kukataa kushiriki mashindano ambayo umetafutiwa tena kwa faida yake.

Gidabuday aliongeza bado wataendelea kuwatafutia wanariadha wao mashindano ya kutafuta viwango vya kushiriki mashindano ya Dunia yatakayofanyika Agost mwaka huu nchini Uingereza.

"Mashindano ya mbio zozote za kutafuta viwango ni ya uwanjani isipokuwa viwango vya mbio za marathoni, na haya mashindano ya Bolder Boulder yalikuwa ni ya barabarani hivyo ninawahaidi wachezaji kuwa bado tuna muda wa kuwatafutia mashindano mengine kwa ajili ya viwango" aliongeza Gidabuday.


Mwisho

No comments:

Post a Comment