JAMII nchini imetakiwa kuwatunza na kuwalinda ndege waliopo
kutokana na kuwa sehemu ya vivutio vinavyochangia kuimarisha mapato kwenye sekta ya utalii.
Viumbe hao muhimu kwenye Ikolojia wametajwa kuwa na jukumu zito
katika ustawi wa taifa hasa wanapotumika kusambaza mbegu kutoka mti mmoja kwenye
eneo jingine.
Hayo yalisema mjini hapa jana na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini
Asasi isiyo ya Kiserikali ya Asili ya Tanzania (Nature Tanzania),Gloria
Bideberi alipoelezea faida na umuhimu wa ndege kijamii na kisayansi.
Akifafanua kuhusu faida za viumbe ndege Bideberi alisema,
viumbe hao wamekuwa wakifanya kazi ya kufurahisha kwa watu kuangalia na
kufuatilia aina ya maisha yao.
“Maisha ya ndege hufanya watu kusafiri umbali mrefu ili kuona
aina fulani ya ndege. Lakini pia wazee wa zamani wawalitumia kutabiri baadhi ya
mambo kama mvua na ujio wa wageni,” alisema.
“Kisayansi tunamuona ndege kama msambazaji muhimu wa mbegu kwani
ili misitu iendelee kuwapo ni lazima mbegu zisambazwe na kazi hiyo inafanywa
zaidi na ndege pia viumbe wengine.”
“Kuna baadhi ya mbegu huwa haziwezi kuota mpaka zipite
kwenye matumbo ya baadhi ya wanyama na ndege ni mmoja wapo, hivyo utaona
umuhimu wa viumbe hawa,” alisema Bideberi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Bodi ya Wadhamini Asili ya
Tanzania John Saleh, alisema asasi hiyo yenye miaka miwili tangu kuanzishwa
kwake imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na Idara za Serikali, asasi binafsi
na wadau wengine.
Alisema Asili ya Tanzania inajishughulisha na mazingira
yanayotunza ndege ambayo kwa kawaida kabisa mazingira hayo huanzia nyuma ya
nyumba zilizozungukwa miti.
“Tunaangalia mazingira yenye umuhimu wa uhifadhi wa ndege,
maeneo ya hifadhi za Taifa, Ngorongoro, Hifadhi za Wananchi, Maziwa kama
Manyara na Natron.
“Kwa muda mrefu utalii umelenga wanyama wakubwa na Tanzania
bado hatujaweza kupata faida kutokana na rasilimali zetu zote, ndege ndio
anakuja kuongeza thamani ya utalii nchini,” alisema Salehe.
Akifafanua zaidi Salehe alisema, wadau wa utalii kwa sasa
wameanza kutambua uhitaji wa wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanaopenda
kuja,kuona na kuelewa kuhusu ndege wa Tanzania.
Naye Mratibu wa Shirika la Kimataifa la Maisha ya Ndege (Birdlife),
lililopo jijini Nairobi nchini Kenya, Ken Mwathe alisema wanatekeleza miradi
katika nchi 25 barani Afrika.
Akielezea kuhusu mradi uliopo Ziwa Natron Mwathe alisema
mradi huo umelenga utalii endelevu katika eneo hilo ili wananchi waliopo maeneo
hayo waweze kunufaika na rasilimali zilizopo.
“Pale tunatengeneza mpango mkakati wa kuongoza utalii,
sehemu kama ile inahitaji mkakati utakaoelezea watalii wangapi, vivutio vya
aina ngani vinapatikana pale.
“Pia tunaangalia namna
gani wadau wanafanya kazi namna gani ikiwamo mpangilio utakaohusisha wadau wote
watafanya kazi ili kuendeleza utalii Ziwa Natron eneo lenye Flamingo wengi,”
alisema Mwathe.
No comments:
Post a Comment