Askofu Dk. Stanley Hotay
Na MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
ASKOFU wa Kanisa la Anglikan
Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Dk. Stanley Hotay ameishauri
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutofanya mabadiliko ya mara kwa mara
katika Sera ya elimu nchini.
Kauli
hiyo aliitoa mjini Moshi wiki iliyopita wakati wa Ibada ya kuweka wakfu jina la
Shule ya Bishop Alpha Memorial High School iliyohudhuriwa na mgeni rasmi Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha.
Ibada
hiyo ilifuatiwa na changizo la kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo la
chakula shuleni hapo ambapo kiasi cha Sh milioni 56.3 zilikusanywa huku Naibu
Waziri Ole Nasha akichangia Sh milioni 8.
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa ibada ambayo mahubiri yake yalitolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, Askofu Dk. Hotay alisema mabadiliko ya mara kwa
mara yamekuwa yakiyumbisha elimu.
“Wizara
ya elimu fikirini kwa upya sera ya elimu mnawezaje kumsaidia mtoto wa Tanzania,
mabadiliko haya ya kila wakati hayamsaidii mwanafunzi,” alisema Askofu Dk.
Hotay.
Kwa
upande wake mgeni rasmi Naibu Waziri Ole Nasha akizungumza kwenye uzinduzi wa
jina jipya la sekondari hiyo alisema, serikali inatambua mchango unaotolewa na
shule binafsi na za Taasisi za dini katika maendeleo ya sekya ya elimu.
“Sera
ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inasema serikali itaweka mazingira bora na
kuhakikisha kuwa sekta ya elimu na mafunzo inatoa rasilimaliwatu ya kutosha na
mahiri ili kukithi mahitaji ya sekta mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.
“Ili
kufikia azma hiyo ushiriki wa wadau wengine kama shule binafsi na taasisi za
dini ni muhimu, hivyo Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa shule hizi ili
ziweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwake,” alisema Naibu Waziri Nasha.
Akifafanua
kuhusu kupanua kwa fursa za elimu nchini, Naibu Waziri Ole Nasha alisema mpango
wa ElimuMsingi bila malipo umewezesha zaidi ya wanafunzi 462,530 kuingia darani
kutoka mwaka 2015 hadi 2017.
“Serikali
inatoa kila mwezi Sh Bilioni 23 kwa ajili ya kutekeleza mpango ElimuMsingi bila
malipo. Na mpango huu umeongeza wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza
kutoka 1,386,592 mwaka 2015 hadi 1,849,122 mwaka 2017,” alisema Naibu Waziri
Nasha.
Alisema
serikali imefanya pia ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na
sekondari kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo (P4R), ikiwa ni pamoja na
ukarabati wa shule zote kongwe 88 nchini.
Kupitia Ibada hiyo Naibu Waziri
Ole Nasha alitolea pia ufafanuzi suala la wazazi na walezi kuchangia katika
maendeleo ya elimu akisema kwamba serikali hajiakataza.
Alisema ni muhimu kuzingatia
maelekezo ya Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2016 katika uchangiaji kwa
kuhakikisha kuwa michango yote inaratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Halmashauri kama ilivyo kwenye michango mingine ya maendeleo.
“Wanafunzi wasifungamanishwe na
mchango wa aina yeyote kwa maana ya kumzuia kuhudhuria masomo au kumnyima cheti
kwa kigeo cha mzazo au mlezi kushindwa kuchangia,” alisema Ole Nasha.
Akisoma
taarifa ya shule hiyo Ofisa uongozi shuleni hapo, Fadhili Chibago aliyataja
malengo ya shule hiyo iliyojulikana awali kama Pasua Sekondari, kuwa ni
kurudisha matumaini mapya kwa wanafunzi waliokosa nafasi za kidato cha kwanza
kwenye shule mbalimbali za serikali.
“Shule
yetu imekuwa ikijitahidi katika ufaulu kitaaluma na ukilinganisha na aina ya
wanafunzi tunawapokea kama shule ya kanisa.
“Mfano
mwaka 2015 kidato cha nne shule ilishika nafasi ya 79 katik ya shule 292 kimkoa
na 906 kati ya shule 3,452 kitaifa. Pia jumla ya wanafunzi 23 walichaguliwa
kwenda kidato cha tano kati ya wanafunzi 70 waliofaulu,” alisema Chibago.
Chibago alisema shule hiyo ni Bweni na kutwa ipo katika Kata ya Pasua mjini Moshi ambapo wazo la kuanzishwa kwake lilitolewa na wananchi wa kata hiyo kwa kushirikiana na Kanisa la Anglikana St. Paul mwaka 1994.
"Maombi hayo yalitumwa wizarani na Kamishna wa elimu alikubali Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro kuanzisha, kumiliki na kuendesha shule hiyo tangu Oktoba 1997," alisema Chibago na kuongeza:
"Shule hii ilisajiliwa rasmi Machi 16, mwaka 1998 na kupewa namba S.927, baada ya hapo ilisajiliwa na Baraza la Mitihani (NECTA) na kupewa namba S. 1067. Lakini pia shule hii ni kituo cha kufanyia mitihani ya QT (Qualifying Test), na PC (Private Candidates) chenye usajili namba P. 1067," alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa Dk. Nchimbi
akihubiri kwenye Ibada hiyo alisema Kanisa la Anglika kumiliki na kuendesha
shule hiyo ni moja ya dhamana kubwa waliyokabidhiwa ya kuandaa taifa lijalo.
“Elimu inayotolewa hapa itawapatia
vijana wetu uelewa mpana wa kuelewa dunia inakwendaje wao kuwa na uhakika wa
kuishi mahali popote,’ alisema Dk. Nchimbi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment