Wednesday, March 21, 2018

TANZANIA NA UJERUMANI ZAKUBALIANA KUENDELEZA TAFITI ZA MASALIA YA MIJUSI KATIKA ENEO LA TENDAGURU MKOANI LINDI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin Ujerumani (Berlin Museum of Natural History), Prof. Johannes Vogel kuhusu masalia ya mjusi wa Tanzania yaliyofadhiwa katika makumbusho hiyo.

.....................................................

Ujerumani na Tanzania zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la Tendaguru mkoani Lindi.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin (Berlin Museum of Natural History) nchini Ujerumani yanapohifadhiwa pia masalia ya mijusi waliopatikana eneo la Mlima Tendaguru mkoani Lindi.

Maj. Gen. Milanzi aliongoza msafara wa Tanzania ulioshiriki maonesho ya Kimataifa ya utalii ya ITB Berlin 2018 yaliyohitimishwa jana nchini Ujerumani. Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 7 mwezi huu yalihusisha taasisi 5 za Serikali na Makampuni binafsi 60 kutoka Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho hiyo, Prof. Johannes Vogel alimueleza Maj. Gen. Milanzi kuwa shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti kwa ajili ya maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusu Dunia, viumbe pamoja na mazingira ili maarifa na ufahamu huo usaidie binadamu kutawala maisha yake na mazingira yanayomzunguka.

Akizungumzia fursa zilizopo za kushirikiana kutafiti maeneo yalikopatikana masalia ya mijusi hao na viumbe wengine Prof. Johannes alisema, Makumbusho yake ipo tayari kushirikiana na Wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa kufanya utafiti na kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya maarifa na sayansi ya viumbe na mazingira.

“Ili kuwa na utafiti endelevu, ni vema kwa nchi ikawekeza kwa wataalamu wake ili kuendeleza utafiti na maendeleo ya sayansi.  Hivyo tupo tayari kushirikiana ili kujenga uwezo kwa wasomi wa Tanzania kuweza hatimaye kufanya utafiti na kuleta maendeleo kwa nchi yao” alisema.

Akizungumzia kuhusu masalia ya mijusi waliopatikana Tendaguru na ambayo yanahifadhiwa katika makumbusho hiyo, alisema badala ya kuwarudisha nchini Tanzania, ni vema wakachukuliwa kuwa elimu, utafiti na maendeleo ya sayansi yanayopatikana kutokana na kuwafanyia utafiti ni kwa maendeleo na ustawi wa dunia nzima.

“Ichukuliwe kuwa huu ni urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa urithi huu hauachi ukapotea.  Hivyo, ni vema tukaimarisha utafiti katika eneo walikopatikana ili kupata masalia mengi zaidi na kuitangaza Tanzania katika Nyanja za utafiti.

“Makumbusho yangu ipo tayari kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za Tanzania mapema iwezekanavyo ili utafiti katika eneo la Tendaguru uendelee kwa manufaa ya Tanzania na Dunia nzima”. alisema Prof. Johannes. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Milanzi aliahidi kuwapa ushirikiano ili kuwezesha tafiti hizo kufanyika kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi wa nchi zote mbili.  Alimkaribisha Prof. Johannes na timu yake kuja Tanzania mapema iwezekanavyo ili kujadili na kukamilisha makubaliano ya kuendeleza tafiti hizo.

Awali, Maj. Gen. Milanzi alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdalla Possi. Miongoni mwa mambo waliyozungumza ni pamoja na masalia hayo ya mjusi wa Tanzania anayehifadhiwa katika moja ya makumbusho nchini humo.

Balozi Possi alisema kuwa kwa maoni yake haoni kuwa wazo la kuhamisha masalia hayo kurudishwa Tanzania kuwa litakuwa na tija kwa maendeleo ya utalii na utafiti wa sayansi kwa nchi yetu. 

Alitoa baadhi ya sababu kuwa sio kweli kuwa masalia hayo ndiyo kivutio kikubwa pekee kinachofanya wanasayansi na watalii wengi kutembelea makumbusho hiyo na hivyo kuipa mapato makumbusho hiyo. 

“Makumbusho inapata ruzuku kutoka serikalini na kiingilio ni sehemu ndogo sana ya mapato ya makumbusho hiyo.  Fedha nyingi za kufanyia shughuli za Makumbusho ya Berlin zinatokana na fedha zinazolipwa kwa ajili ya kufanya utafiti na si viingilio katika makumbusho” alisema Dk. Possi.

Alisema makumbusho hiyo ina mikusanyo mingi ya viumbe mbalimbali zaidi ya milioni 30 ikiwemo ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani.  Mkusanyiko huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na watalii kutembelea na kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo. 

Dk. Possi alisema kuendelea kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo kuna manufaa zaidi ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utafiti wa kisayansi kuliko masalia hayo yatakapoondolewa katika makumbusho hiyo na kurejeshwa nchini Tanzania. 

Alisema kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo ni kama Balozi wa utalii na utafiti wa kisayansi anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani. 

Akizungumzia mchakato unaoendelea hivi sasa hapa nchini wa kuandaa Utambulisho mpya wa Tanzania (National Branding), Balozi Possi alishauri kuwa ni vema mabadiliko yatakayopelekea kuondokana na utambulisho unaotumika hivi sasa ukaangaliwa kwa umakini kwa kuwa kuna hatari ya kupoteza msisitizo uliopo katika vivutio maarufu vya utalii nchini na kutoa fursa kwa washindani kutangaza utalii wao kupitia vivutio hivyo.

Alisema endapo hakuna athari kwa kutumia utambulisho wa sasa ambao ni maarufu (Tanzania the Land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar), ni vema zikaangaliwa pia athari zitakazopatikana kwa kuachana na “brand” inayotumika hivi sasa.

Alisema kuwa baadhi ya vitu vinavyotumika kwenye utambulisho wa sasa tayari ni “brand”.  Alitoa mfano kuwa Mlima Kilimanjaro ni Brand maarufu na inayojiuza, hali kadhalika kwa Serengeti na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment