Tuesday, March 6, 2018

UTAFITI: WAKULIMA, WAFUGAJI HAWANA UELEWA WA TOZO WANAZOKATWA




ARUSHA

UTAFITI wa Baraza la Kilimo na Mifungo nchini (ACT), umebaini wakulima na wafugaji wilayani Arumeru mkoa wa Arusha hawana uelewa wa fedha zinazotengwa kutoka kwenye tozo wanazokatwa ili ziwasaidie katika shughuli za kilimo.

Matokeo ya utafiti huo yaliwasilishwa mjini hapa jana na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mohamed Samkunde wakati wa majadiliano yaliyoshirikisha wadau wa kilimo na wakuu wa Idara ya Halmashauri ya Meru.


Alisema, ili kupata taarifa sahihi juu ya malalamiko wilayani humo kupitia utafiti huo waliwahusisha wakulima, wafugaji, Taasisi mbalimbali za kijamii, Maafisa kilimo na Maafisa wa serikali.

“Utafiti huu ulianza mwaka jana Novemba ukihusisha wilaya ya Arumeru ulilenga kuangalia ni kwa kiwango gani Serikali kupitia halmashauri inasaidia wakulima na wafugaji kupitia tozo inazowatoza,” alisema Samkunde na kuongeza:

“Tumebaini vitu vingi kimoja ni wakulima kutokujua kabisa kama kuna fedha zinatengwa ili kusaidia shughuli za kilimo baada ya kukusanya mapato kutoka kwa wakulima,” alisema.

Alisema kupitia fedha hizo inatakiwa kuanzia 10 zirudi kwa wakulima na wafugaji ili kuwasaidia kujikwamua matoke yake imekuwa ngumu kurudishwa kutokana na madai ya halmashauri kutokuwa na fedha za kutosha.

“Fedha hizo hutumiwa kuendeshea shughuli nyingine za kiofisi kutokana na maelekezo au matamko ya serikali badala ya kurudi kwa mkulima na wafugaji.Faida inayotokana na tozo wanazolipa haionekani kwani hakuna vyoo, maji safi na masoko hayaendelezwi.”

“Utafiti umebaini pia Halmashauri ya Meru vijana wamekata tamaa ya kilimo wamekimbia vijijini, wanaoshughulika na kilimo ni wazee hiyo ni kutokana na kutokuwapo uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya kilimo,” alisema Samkunde.

Kwa upande wake Khalid Ngassa anayefanya kazi na ACT alisema, wilaya ya Arumeru ni miongoni mwa wilaya 10 zilizopo nchini walizozichagua kwenye majaribio yaliyolenga kuibua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakulima na wafugaji.

Kutokana na changamoto ni nyingi wilayani huo ACT iliona haja ya kuja na mkakati unaoweza kuishauri Serikali Kuu na halmashauri zitenge angalau asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuona zinawezaje kusaidia shughuli za kilimo kwa wakulima hasa wadogo.

“Tulianza mwaka 2015 tukitoka hapa tunakwenda Kanda ya Ziwa kufanya tafiti nyingine. Maeneo tuliyopita tumeona mafanikio mfano Mbozi na Njombe tulifanya utafiti wa pembejeo zisizo na ubora leo tatizo hilo limepungua,” alisema Ngassa.

Naye mshiriki wa majadiliano hayo Afisa Kilimo kutoka Halmashauri Meru Grace Solomoni alisema, utafiti huo umetoa picha halisi ya kinachotokea kwa wakulima na wafugaji.

“Ni kweli, halmashauri zinakusanya mapato kutoka vyanzo vingi  vinavyotokana na kilimo na mifugo. Na kiasi kidogo hurudi kwenye huduma za ugani kupitia ujenzi wa madarasa na huduma za afya,” alisema Solomoni na kuongeza:

“Serikali ilitoa waraka ulioelekeza asilimia 20 ya mapato yatokanayo na vyanzo vya kilimo yarudi kuendeleza shughuli hizo na asilimia 20 ya mapato yatokana na vyanzo vya mifugo na uvuvi yaendeleza huduma za ugani na miradi,” alisema.

Aidha, mkulima wa mbogamboga katika Kijiji cha Lekitatu wilayani humo Alfred Ole Loibaguti  aliomba tafiti za aina hiyo ziendelee kufanywa ili kuwakomboa wakulima wadogo kwani kupitia utafiti matatizo yao yataibuliwa.

No comments:

Post a Comment