UZINDUZI TOVUTI MPYA YA MISA TANZANIA
MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo
na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, amesema utafiti uliofanywa na Taasisi
ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika(MISA) Tawi la Tanzania
kwao ni sawa na chakula.
Akizungumza na baadhi ya wanahabari, wanasheria
na wadau wengine wa habari mjini hapa wakati mjadala kuhusu mrejesho wa Utafiti
wa Haki ya kupata taarifa katika ofisi za umma uliofanywa MISA Tanzania
kwa kushirikiana na Shirika la CIPESA kutoka Uganda. .
Dk. Abbas katika mjadala huo
aliipongeza MISA Tanzania kwa kufanya utafiti huo akisema utakuwa kioo kwa
maofisa Mawasiliano serikalini pamoja na watendaji wa idara mbalimbali za
serikali.
“Tafiti kama hizi zinapofanyika huwa ni
chakula kwetu, niwapongeze nimesoma kurasa zote neno kwa neno,” alisema Dk.
Abbas na kuongeza.
“Hii inatuonyesha hata watendaji wa
serikalini wanapaswa kujitahimini katika kutoa habari kwa maofisa mawasiliano kwenye
ofisi zao, tumeona kwenye utafiti baadhi waliotakiwa kutoa taaifa walivyokuwa
wakijibu,” alisema.
Dk. Abbas alisema ili kuimarisha utoaji
taarifa serikalini tayari hatua madhubuti zimechukuliwa ili kuwafanya maafisa
habari na watendaji wao kutoa habari kwa mujibu wa Sheria ya haki ya kupata
taarifa ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo kanuni
zipo tayari, utoaji wa taarifa unatakiwa kufanyika ndani ya siku 21 na iwapo
mhusika atashindwa kutoa kutekeleza atatakiwa kutoa maelezo kimaandishi
akielezea sababu zilizomfanya ashindwe kutoa taarifa hizo.
“Hata kama sheria inataka taarifa
zitolewe ndani ya siku 21. Lakini haimaanishi kwamba ni lazima zifike siku
hizo, zinaweza kutolewa hata siku mbili baada ya kuwasilishwa kwa ombi la
kupata taarifa,” alisema Dk. Abbas.
Katika uchangia huo Dk. Abbas alizindua
pia tovuti mpya ya Taasisi hiyo, (Tanzania.misa.org) huku akisisitiza tatizo la
utoaji taarifa halipo kwa maafisa mawasiliano pekee bali kwa wataalam
(watendaji) ambao huwa hawawasaidii maafisa hao kutoa habari za uhakika.
“Sasa katika hili tumeanza kuwajengea uwezo
maafisa habari kuwa kweli maafisa habari wa maeneo yao husika,” alisema Dk.
Abbas na kuongeza:
“Nataka kila afisa habari awe anajua
habari zote za kwake mkononi, nataka tufike huko ingawa suala kubwa kwetu kwa
sasa ni utendaji kazi unaonekana,” alisema na kuongeza,” alisema.
Awali akiwasilisha utafiti huo Wakili wa
Mahakama Kuu James Marenga na Mhariri wa habari wa zamani, alisema utafiti huo
ulihusisha mikoa Saba kati ya 28 iliyopo nchini.
Aidha alisema siku 21 ziliwekwa
kisheria ili kupata taarifa kikitumiwa kama kilivyo, hakitakuwa na msaada sana
kwa waandishi wa habari kwa sababu baadhi ya taarifa wanazozitafuta kwa ajili
ya habari zinaweza kupitwa na wakati hivyo kutokuwa na thamani tena ya habari.
“Utafiti huu ulifanyika kwenye mikoa 7
kati ya 28 nchini, tulihakikisha tuna upanga katika makundi mawili kundi la
maandishi na kundi la kuhoji kwa mdomo, kupiga simu, email.
“Makundi hayo tuliyapangia alama
kulingana na namna jibu litakavyokuwa likitolewa kwenye kundi husika, nia yetu
ilikuwa ni kuhakikisha hakuna uwazi wa kisingizio cha kutoa taarifa,” alisema
Wakili Marenga.
Kwa upande wake Afisa kutoka CIPESA
Ashnah Kalemera yeye alielezea kuhusu utafiti uliofanyika Ukanda wa Afrika
Mashariki (EAC).
“Nchi ya Sweeden ndio ilikuwaya kwanza
kuwa na sheria ya haki ya kupata taarifa tangu mwaka 1766. Kwa Nchi za Afrika
Mashariki Uganda ilianza mwaka 2005, Rwanda 2013, Sudani Kusini 2013, Kenya na
Tanzania 2016 na Burundi hawana,” alisema Kalemera kutoka CIPESA.
Akifunga mjadala huo, Mwenyekiti wa
Bodi ya Misa Tanzania, Solome Kitomari, aliishukuru Serikali kwa kushirikiana
na taasisi hiyo akisema haki ya kupata taarifa ni muhimu kwa kila Mtanzania.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment