MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), imefanikisha
zoezi la kuhamisha wanyamapori katika maeneo ya makazi ya viongozi wa kitaifa
ikiwamo Ikulu ya Chamwino Dodoma inayoendelea kukarabatiwa.
Kuhamishwa wanyamapori hao kulianza Mei hadi Agosti mwaka
huu kukihusisha Pimbi zaidi ya 300, Nyoka zaidi ya 50, Kenge na Mijusi ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hayo yalibainishwa na Meneja wa Pori la Akiba la Swaga
Swaga lililopo wilaya ya Chemba na Kondoa, Alex Choya alipokuwa akijibu maswali
ya wanahabari waliotembelea pori hilo ili kujionea vivutio na changamoto.
Meneja Choya
Akijibu maswali Meneja Choya alisema, pori hilo lililoanzishwa
mwaka 1997 lina Kilomita za mraba 871 lina vivutio vingi vya utalii wa upigaji
picha na uwindaji, huku wanyama Simba, Tembo, Tandara wakubwa na wadogo
wakipatikana.
Alisema TAWA inayosimamia wanyamapori nchini hivi karibuni ilipokea
ilipokea agizo la kuhamisha wanyapori katika makazi ya viongozi wa kitaifa
yanayofanyiwa ukarabati ikiwamo Ikulu ya Chamwino na makazi ya Waziri Mkuu
Dodoma.
“Wizara ya Maliasili na Utalii ilipokea agizo la kuhamisha
viumbe hai wakiwamo Nyoka zaidi ya 50, Kenge, pimbi zaidi ya 300 na mijusi
kutoka makazi makuu Ikulu ya Rais Chamwino Dodoma na Waziri Mkuu.
“Zoezi la kuwahamisha na kuwaleta Pori la Akiba la Swaga
Swaga lililopo karibu lilifanyika kwa ufanisi. Na aina mojawapo ya nyoka
waliohamishwa ni Swila na Vifutu,” alisema Choya na kuongeza:
“Wanyamapori hao walikuwa wakiishi kwenye makazi yao ya
asili yenye majabali, miamba na misitu mikavu ambayo nyoka hupendelea na wakati
mwingine hata kwenye makazi ya watu kwasababu nao ni viumbe hai kama sisi,”
alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAWA Dk, James Wakibara
akizungumzia ufanisi wa zoezi hilo alisema, zoezi la kuhamisha wanyamapori la
kawaida kufanyika kulingana na mahitaji ya eneo husika na aina ya wanyamapori
waliopo.
“Tulipoambiwa kuwahamisha wanyamapori kuwatoa Dodoma na
kuwaleta huku Swaga Swaga kilikuwa ni kitu kidogo na cha kawaida,” alisema Dk.
Wakibara na kuongeza:
Dk.Wakibara
“Tunajivunia kutoa huduma hiyo kwa Makao Makuu yetu ya nchi
Dodoma. Lakini pia imezidi kutututambulisha TAWA ni shirika kubwa katika uhifadhi
wanyamapori,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi anayesimamia huduma za usimamizi wa
wanyamapori TAWA David Kanyata zoezi hilo lilifanyika kwa ufanisi mkubwa
kutokana na kazi hiyo kuwa sehemu ya majukumu waliyokabidhiwa.
Kupelekwa kwa wanyamapori hao katika Pori la Akiba la Swaga
Swaga kumekuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhamia kwa viongozi wa kitaifa katika
makao makuu ya nchi Dodoma.
Tayari Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alishamia Dodoma ikiwa
ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli kuhakikisha viongozi wote wa
kitaifa wanahamia makao makuu ya nchi.
Mbali ya Waziri Mkuu tayari Makamu wa Rais Mama Samia
Hassan Suluhu naye amehamia kwenye makazi yake mjini humo hivi karibuni huku
Rais Dk. Magufuli akitarajiwa kuhamia mjini Dodoma mwakani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment