Na Hamza
Temba, Dodoma
SERIKALI imesikia
kilio cha wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii nchini na kuamua kuongeza muda
wa miaka miwili ya umiliki wa leseni za vitalu 95 vya uwindaji wa kitalii
ambazo zilikuwa ziishe muda wake tarehe 31 Desemba mwaka huu (2017).
Uamuzi huo
umefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati wa
kikao cha majumuisho na watendaji wa Wizara hiyo muda mfupi baada ya kumalizika
kwa mkuano wa wadau wa sekta hiyo ulioandaliwa na Wizara hiyo mjini Dodoma
jana.
Akizungumzia
uamuzi huo Dk. Kigwangalla alisema, lengo ni kuwapa muda wawekezaji hao ili
waweze kujiandaa na mabadiliko ya mfumo mpya wa utowaji wa leseni za vitalu vya
uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ikiwemo kurudisha baadhi ya gharama za
uwekezaji walizoweka katika vitalu hivyo.
Awali
akizungumza katika mkutano huo wa wadau Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa
Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini, Michael Mantheakis alimuomba Waziri
Kigwangalla kuwaongezea muda wa umiliki wa leseni zao kuanzia miaka mitano au
mitatu na nusu ili waweze kurudisha gharama za uwekezaji walizowekeza katika
vitalu hivyo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, makambi na vifaa vyake pamoja na
maji.
Hata hivyo,
Waziri Kigwangalla aliweka wazi msimamo wa Serikali wa kutimiza azma yake ya
kuingia kwenye utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa
kitalii kwa njia ya mnada na kusema kuwa kamwe haitorudi nyuma na kwamba
utekelezaji wa zoezi hilo hauwezi kusubiri muda mrefu kiasi hicho.
Akizungumzia
kuhusu hatua ya utekelezaji wa utaratibu huo, Waziri Kigwangalla alisema kwa
sasa taratibu za kuandaa Sheria za usimamizi zinaendelea na zinatarajiwa
kukamilika mwezi Februari 2018 pamoja na kanuni zake zinazotarajiwa kukamilika
mwezi Aprili 2018.
Aidha,
alisema mfumo maalumu wa kielektroniki unaandaliwa ambapo maombi yote ya leseni
za umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada yatafanyika kwa uwazi kwa
njia ya mtandao.
Alisema
baada ya kukamilika kwa taratibu zote na mfumo huo mpya wa utoaji wa leseni za
vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na maombi kuwasilishwa, mnada
wa kwanza utaanza tarehe 1 Julai, 2018 kwa kuanza kunadi vitalu 61 ambavyo kwa
sasa havina wawekezaji.
Mnada wa
pili utafanyika mwaka 2020 baada ya kuisha kwa muda huo wa nyongeza wa miaka
miwili ukihusisha vitalu 95 vilivyoongezewa muda wa umiliki wa leseni pamoja na
vitalu vingine endapo vitabaki katika mnada huo wa kwanza kwa sababu
mbalimbali.
Alisema
sheria na kanuni zinazoandaliwa hivi sasa zitazingatia mambo muhimu ikiwemo
kuwapa nafasi watanzania wenye mitaji midogo kuweza kuingia kwenye biashara
hiyo pamoja na kuweka adhabu kali dhidi ya wafanyabiashara watakaohujumu
biashara hiyo kwa makusudi.
Mkutano huo
wa siku moja ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, wakurugenzi, wakuu wa
vitengo na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na waandhishi wa
habari.
Oktoba 22
mwaka huu (2017) wakati akiongoza kikao cha wadau wa sekta ya Maliasili na
Utalii mjini Dodoma, Waziri Kigwangalla alitangaza kufuta leseni za vitalu
vya uwindaji wa kitalii zilizokuwa zianze mwezi Januari, 2018 ili kupisha
utarartibu mpya wa utoaji wa leseni hizo kwa njia ya mnada ikiwa ni mkakati wa
Serikali wa kuimarisha sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment