Thursday, December 21, 2017

MAPORI YA AKIBA YATAJWA KUWA KIUNGO MUHIMU KWA HIFADHI ZA TAIFA, MAENEO YALIYOHIFADHIWA


Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dk. Manongi

MHIFADHI Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk. Freddy Manongi amesema, Mapori ya Akiba yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), ni kiungo muhimu kinachosaidia kupunguza msukumo wa maisha ya kawaida ya binadamu ikiwamo matumizi ya ardhi maeneo ya hifadhi.


Dk. Manongi alisema Serikali ilianza kwa kuwa na mapori ya Akiba ikiwa na malengo ya shughuli za uwindaji wa kitalii ambapo mapori yaliyoonekana kuwa na umuhimu zaidi yalipandishwa hadhi na kuwa hifadhi za taifa au maeneo ya uhifadhi kama Ngorongoro.

“Serikali iliacha maeneo hayo likiwamo Pori la Akiba la Maswa, Mkungunero, Sakasaka kwa lengo la kupunguza msukumo wa muingiliano wa maisha kati ya binadamu na wanyama,” alisema Dk. Manongi na kuongeza.

“Mengine ni Pori la Akiba Ikorongoro-Grumet yaliyopo ukanda wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori Tengefu la Loliondo, mapori haya na mengineyo yanasaidia kupunguza msukumo wa shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi muhimu,” alisema.

Wakati Dk. Manongi akielezea umuhimu wa mapori hayo, Kaimu Meneja Pori la Akiba Maswa Joel Pallangyo alisema wanaendelea kukabiliana na changamoto za wafugaji kuingiza mifugo hifadhini pamoja na wakulima kulima maeneo yenye zaidi ya Mita 500 kutoka ulipo mpaka.

“Mpaka sasa tumekamata ng’ombe 1,000 ndani ya hifadhi, kati yao 553 wametaifishwa na kuuzwa kwa mnada waliokutwa na mifugo walihukumiwa kifungo. Tulikamata ng’ombe wengine 458 hawa wametaifishwa, taratibu zinaendelea na 119 kati yao kibali cha kuwauza kipo tayari,” alisema Pallangyo.

“Changamoto ya kuingiza mifugo ndani ya mapori ya akiba, wakulima kuendesha kilimo ndani mita 500 bado zinatishia ustawi wa uhifadhi. Pori la Akiba Maswa lenye kilometa za mraba 4,223 limezungukwa na vijiji 26 vya wilaya ya Itirima, Bariadi na Meatu mkoani  Simiyu wakazi wake ni wakulima na wafugaji,” alisema.

Naye Afisa Wanyamapri Mkuu kutoka TAWA Seth Ayo alisema, Pori la Akiba la Maswa lina wanyama zaidi ya 30 wakiwemo Nyumba na Tembo, pamoja na kuendesha shughuli za utalii wa picha na uwindaji.

Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dk. Manongi akizungumza na vyombo vya habari

“Pori la Akiba la Maswa limekuwa msaada mkubwa kwa NCAA kutokana kupakana na hifadhi hiyo kwa kukinga baadhi ya shughuli za kibinaadamu kufanyika moja kwa moja ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Ayo.


Mwisho.  

No comments:

Post a Comment