Na Dixon Busagaga -Kilimanjaro.
MPANDA milima mashuhuri duniani kwa kutumia Baiskeli ,Juanito
Oiarzabal ameweka rekodi ya kuwa Mhispania wa kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro
huku akitumia saa 31 akiendesha baiskeli kwa siku tano hadi kufika kilele cha
Uhuru.
Juanito na wenzake wawili , Eduardo Pascuaz na Ramon Abecia
waliianza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia Baiskeli ,wakianza
safari yao kupitia lango la Kilema, aina hi ya utalii ikiwa ni bidhaa mpya
katika Milima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Aina hii mpya ya utalii ambayo kwa sasa imeanza kushika kasi
katika Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro,Arusha na Saadani inatokana na Shirika
la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuendelea kupanua wigo wa vivutio vya utalii
katika Hifadhi zake 16.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
Pascal Shelutete anaeleza hatua ya Juanito na wenzake kufika katika kilele cha
Uhuru inaashiria kuanza kufunguka kwa aina hii mpya ya utalii katika Hifadhi za
Taifa .
Shelutete anaeleza namna ambavyo Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa)
limekuwa mstari wa mbele katika kubuni aina mpya ya bidhaa za utalii ili
kushindana na nchi nyingine duniani katika uuzaji wa safari kwa watalii.
Kwa upande wake Juanito Oiarzabal ambaye amepata ulemavu wa
kukatika vidole kutokana na barafu katika milima mbalimbali aliyopanda amesema
changamoto aliyokutana nayo wakati wa kupanda mlima ni kuzoea hali ya hewa ya
mlima ambayo imekuwa ikibadilika kila mara.
Mkurugenzi wa kampuni ya Safari Bike Africa iliyoratibu
changamoto ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia Baiskeli kwa wageni
hao,Mario Martos amesema kampuni yake imekusudia kuleta mabadiliko katika sekta
ya utalii kwa kufanikisha safari za watalii wa kutumia baiskeli.
Shirika la Hifdhi za Taifa (TANAPA) limejipanga kuhakikisha
usalama wa hali ya juu kwa wageni watakaofanya aina hii mpya ya utalii katika
Hifadhi zake kwa kuwa na taahadhari sambamba na waongoza wageni waliobobea
katika kazi ya Utalii.
No comments:
Post a Comment