Tuesday, September 19, 2017

WADAU WATAKIWA KUTEKELEZA MALENGO ENDELEVU YA ELIMU

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jaffo.


Nteghenjwa Hosseah, Tamisemi – Dodoma.


WADAU wa Elimu nchini wametakiwa kujielekeza katika kutekeleza malengo endelevu ya Elimu ili kutoa Elimu bora na jumuishi kwa watoto wote na waweze kunufaika na mpango huu pasipo kujali tofauti za kimazingira na kibiologia.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dr. Leornard D. Akwilapo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa pamoja wa wadau wa Elimu kwa lengo la kujadili  mapitio ya Sekta ya Elimu kwa mwaka uliopita kinachofanyika Mjini Dodoma.

Amesema umefikia wakati sasa wadau wote waliopo katika Sekta ya Elimu kujielekeza katika vipaumbele vilivyoainishwa katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014 sambamba na Mpango wa Elimu uliopitishwa mwaka 2017.

“Tunafahamu fika kuwa wadau wote kwa ujumla mmejitahidi kukabiliana na changamoto za Elimu zilizokuwa zinaikabili jamii nzima katika kupata Elimu bora na mmekuwa mkiunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha Sekta nzima ya Elimu; Hakika mnastahili pongezi lakini zaidi ya hapo inabidi tujielekeze zaidi kwenye maeneo ya kipaumbele”.

Aliongeza kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa Elimu mashuleni, uboreshaji wa miundombinu ya kusomea na kuhakikisha walimu wenye taaluma stahiki wanakuwepo wa kutosha kuwafundisha watoto wa Jamii ya Kitanzania; Tunahitaji ushirikiano sana toka kwqa wadau ili tuweze kuboresha na kutokomeza changamoto ambazo bado zinatukwaza katika Sekta hii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huu na kuwasilisha salamu za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda amesema kimsingi Wizara hii ndiyo inayotekeleza Sera iliyowekwa na Wizara ya Elimu hivyo tunaratibu utoaji wa Elimu ya awali, Msingi na Sekondari na kusimamia Elimu katika mfumo rasmi na usio rasmi.

 “Sisi kama watekelezaji wa Sera, Viwango na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu tunatumia jukwaa hili kuwasiliana na wadau kuhusu namna bora ya kuondoa vikwazo vinavyoweza kupunguza kasi ya kuwawezesha watoto kupata Elimu bora”.

Aliongeza kuwa kwa pamoja tutaweka mipango ya kuhakikisha tunajenga miundombinu ya shule, tunaboresha mazingira ya kufundishia, kuimarisha taaluma ya Elimu bora ili kuweza kutoa Elimu bora kwa watoto wote na kutomuacha mtoto yeyote nje ya Mfumo.

Katika kuboresha mazingira ya Elimu Kwa sasa tunaendelea na kampeni ya kujenga majengo ya shule yasiyokuwa na ngazi ili kuwawezesha watoto wote kuyatumia kwa urahihsi wakati wa kupata masomo yao katika mazingira rafiki na salama.

“Tumeshuhudia hapo awali miundombinu ya shule haikuwa rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu na walikua wanapata shida sana kufika darasani ilikua mpaka wabebwe na wenzao ila kwa majengo mapya yanayojengwa hivi sasa hayatakuwa na Ngazi hivyo itakua na nafuu kwa wote kufika darasani” alisema Nzunda.

Akiwasilisha taarifa ya Utangulizi Mkurugenzi wa Bajeti na Miradi ambaye pia ndiye mratibu wa Mkutano huu Gerald Mweli alisema mkutano huu umewakutanisha wadau wa Elimu wa ndani na nje ya Nchi   kwa lengo la kufanya mapitio ya sekta ya elimu ili kujadili  mafanikio, changamoto  na kutafuta njia za pamoja za kutatua changamoto hizo kwa maslahi mapana ya  kuboresha Sekta ya elimu nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mweli  amesema mkutano huo unalengo la kujadili utekelezaji wa mipango ya elimu ya mwaka uliopita, kutathmini na kuweka mipango ya pamoja ili kutekeleza malengo yaliyowekwa katika sekta ya elimu.

Mkutano huu wa siku nne unatarajiwa kuhitimishwa Alhamisi Septemba 21, 2017  

No comments:

Post a Comment