Thursday, September 21, 2017

RAIS DK. JOHN MAGUFULI ASHUSHA KISHINDO MIGODI YA MADINI YA TANZANITE MIRERANI





Rais Dk. John Magufuli akikata utepe kuzindua barabara ya lami kutoka KIA hadi Mirereni Simanjiro


-SIMANJIRO

RAIS Dk. John Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwaachia wawekezaji ‘wenye umuhimu’ katika migodi ya Tanzanite waliokamatwa kwa ajili ya kusaidia kutoa taarifa nyeti, wakakae na Kamati ya kujadili madini ili kurekebisha mkataba utakaokuwa na faida kwa serikali nasi wa kinyonyaji.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kupitia SUMA JKT kuanza haraka ujenzi wa ukuta katika eneo lote la vitalu A mpaka D lenye eneo la Kilomita za Mraba 81.99 linalotajwa kuwa na Tanzanite nyingi huku nchini nyingine zikiendelea kunufaika na Serikali ikipata asilimia 5 tu inayotokana na madini hayo.

Maagizo hayo aliyatoa wilayani hapa jana akiwa Kata ya Naisinyai alipokuwa akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua Barabara yenye kiwango cha lami kutoka Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mpaka Mji mdogo wa Mirerani yenye urefu wa Kilomita 26.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Rais Dk. Magufuli aliyeonekana kuumizwa na wizi wa madini ya Tanzanite alisema, ameona ni vyema kuanza na hatua hiyo huku akiwa na uhakika mwekezaji wa Tanzanite One na wawekezaji wengine watakaa na Serikali kutengeneza mkataba mwingine.

“Ninafahamu palikuwa na hatua kadhaa zilikuwa zimeanza kuchukuliwa kwa wawekezaji kama njia ya kupata taarifa vizuri. Na vipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, kwa sasa hivi wale waliokuwa wanahusika katika kusaidia kutoa taarifa hizo muwaachie wale ambao ni muhimu wakae na Kamati ya Waziri wa Sheria na Katiba Professa Palamagamba Kabudi.

“Wapitie kwa pamoja mkataba huu waurekebishe wasaini upya ili asilimia kubwa ya fedha zibakie hapa. Fedha hizo zikapopatikana tuanze mpango wa kuweka maji ya uhakika hapa Simanjiro. Nimeona tuanze na hiyo haiwezekani wananchi wakaendelea kulia, kusikitika na wengine wakicheka kwa faida ya wanyonge.

Nimesema hapana, ndani ya mamlaka yangu ni lazima tujipange vizuri. Hili suala naona linafikia mwisho, tumechezewa vya kutosha. Najua kulikuwa na watu wanafaidika, biashara ya Tanzanite haijazuiliwa bali tunaitoa kwenye magendo na kuwa biashara halali.

“Nataka Tanzanite iwe halali na si haramu, wachimbaji wadogo chimbeni ukipata mali yako ukiwa ndani ya uzio kauze unavyotaka. Tunataka soko la Tanzanite liwe Simanjiro si Arusha, wanaotoka Marekani na India waje wanunue hapa, akishuka na ndege hapo KIA aje kwa gari hapa anunue Tanzanite akauze anakojua.

Huku akimsifia Mbunge wa Jimbo hilo James Ole Millya (Chadema) Rais Magufuli alisema mbunge huyo alilelewa na CCM akiwa UVCCM iliyomfanya kupata ubunge alisema,hivyo hapaswi kuonekana kama adui wala vyama vya siasa bali adui mkubwa ni maendeleo.

“Nawashukuru kwa kumchagua Millya, ni mchapa kazi amelelewa na CCM ukimuona sura yake ni kama Chadema lakini moyo wake ni CCM kabisa,” alisema Magufuli huku akisisitiza kwamba ujenzi wa ukuta huo utakuwa na Kamera na vifaa maalum vya kubaini wizi wa Tanzanite.

“Kutakuwa na mlango mmoja wa kuingilia ili kudhibiti utoroshwaji. Hata ukimeza Tanzanite tumboni au kuficha kwenye viatu, itaonekana. Ndugu zangu viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali hizi kama wangezisimamia vizuri leo hii Watanzania wasingekuwa masikini.

“Kubwa linafanyika kwa sisi viongozi tunaopewa mamlaka ya kusimamia tunakuwa sehemu ya mafisadi wa kuwauminza Watanzania maskini, viongozi tunasahau tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.Tanzanite hii haitakaa miaka yote katika uongozi wangu nimeamua kuiongoza hii vita.

“Leo nimekuja kufungua barabara, nitaifungua lakini nataka tuzungumze suala la Tanzaniate tunafanya nini?” Alihoji Rais Magufuli na kuongeza:

“Sina sababu ya kumung’unya maneno madini ya Tanzanite yanaibwa sana ni shamba la bibi la mabibi waliokufa miaka mingi, watu wanachukua kuliko hata shamba la bibi. Mgodini kuna wawekezaji wameingia ubia na Shirika la Madini nchini (STAMICO) kila mtu ana asilimia 50, lakini bado mali inasombwa,” alisisitiza.

Hivi karibuni Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma na Hussein Gonga wanaochimba Tanzanite kwa ubia na STAMICO, walikamatwa kwa mahojiano zaidi ikiwa ni siku chache tangu Kamati ya Bunge itoe taarifa ya uchunguzi wa madini hayo iliyosomwa mbele ya Rais Dk. Magufuli.   

WAWEKEZAJI
Akifafanua kuhusu wawekezaji kuja nchini kuwekeza Rais Dk. Magufuli alisema Serikali inawahitaji wawekezaji wenye nia njema na si wawekezaji wanaopanga kuja kuiibia nchi.

“Kama kutakuwa na mwekezaji anayetaka kuja nchini kutuibia basi huyo asije kabisa atakuwa amekula wa chuya kwani wakati huu hataiba bali atalia. Na hili nalisema kwa wazi tumeamua kupambana kwa vita ya uchumi wa taifa letu.

“Nchi yetu ni tajiri, juzi tumekamata madini ya Almasi yenye thamani ya fedha nyingi, kwenye madini ya dhahabu ndio usiombe ni uozo mtupu, hovyo. Hawa watu wametujengea mazingira eti wao ndio wanacho sisi hatuna kumbe sisi ndio tunacho wao hawana. Wengine wanajifanya wafadhili kumbe hawana lolote,” alisema Rais Dk. Magufuli.

STAMICO
Rais Dk. Magufuli akielezea ushiriki wa Shirika hilo katika kusimamia madini ya Tanzanite aliagiza kuondolewa mara moja kwa baadhi ya watu walioshiriki kufanya mambo ya hovyo.

“Kama kuna watu waliofanya ya hovyo watolewe mara moja, ni lazima tujipange vizuri. Vyombo vya ulinzi, polisi na usalama hakikisheni  Tanzanite haivushwi hovyo hovyo atakaye toka na Tanzanite kwnda nje ya nchi awe halali amelipia kila kitu aende zake salama apewe na vibali.

“Tupo kwenye vita kubwa ya kubadilisha hii nchi tumechezewa mno yale ninayoyaona kule ni maajabu mengi. Nilipoingia madarakani mnafahamu tulifanya nini watumishi, wanafunzi tumekuta hewa.
“Juzi tumegundua kuwapo kwa mbolea hewa yenye thamani ya Sh Bilioni 58 kuna mtu alisema ataleta mbolea kumbe ni hewa. Haya yote yalikuwa yanafanyika katika nchi inayoitwa Tanzania.

“Mlinituma kwenda kufanya kazi, nilipoyakuta haya sikunyamaza na wala sintanyamaza nitalala nao mbele mpaka wakome kwasababu Tanzania haikuumbwa kwa ajili ya mafisadi bali kwa ajili ya wanyonge,” alisema Magufuli.

BOT
Katika mkutano huo aliiagiza kwa mara nyingine Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutengeneza mkakati wa kushiriki katika ununuzi wa madini ya Tanzanite kwani madini hayo si rahisi kudanganya kama inavyoweza kufanywa kwenye dhahabu.

Katika hatua nyingine uwanjani hapo Rais Magufuli alishangwa na kitendo cha Mji huo wa Mirerani kutokuwa na gari la kubebea wagonjwa ilahali kuna madini ya Tanzanite yanayopatokana duniani pekee katika Kata hiyo ya Naisinyai.

“Hivi ni kwanini Mungu atupe Tanzanite sisi peke yetu halafu hata gari la wagonjwa hamna. Hiyo gari nitawaletea mimi, na kuhusu suala la maji hilo pia niachieni nalifanyia kazi,” alisema Magufuli.

Kwa upande wake Mbunge Millya aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo pamoja na wabunge wengine kutoka mikoa ya Manyara na Arusha alimuomba Rais Magufuli kuhakikisha anaacha alama ya uongozi wake katika maisha ya wananchi wa Simanjiro.

“Mheshimiwa Rais Magufuli nakuomba ujio wako ukabadili maisha ya wananchi hawa waliojitokeza kusikiliza, madini ya Tanzanite yameisha, nakuomba uweke mkono wako katika ardhi ya Mirerani na Simanjiro,” alisema Millya.

Naye Waziri wa Ujeni, Uchukuzi na Mawasiliano Professa Makame Mbarawa alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa kiungo muhimu cha kibiashara kwa wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

“Barabara hii imegharimu Sh Bilioni 32 zikiwa ni fedha zilizotolewa na serikali kutoka kwenye kodi za Watanzania,” alisema Prof. Mbarawa.

Mara baada ya kuzindua barabara hiyo iliyopo mkoani Manyara, Rais Magufuli amewasili mkoani Arusha ambapo Septemba 23, mwaka huu anatarajiwa kutoa kamisheni kwa maofisa wa jeshi.
Shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa badala ya viwanja vya Chuo cha Maofisa wa Jeshi (TMA) kilichopo wilayani Monduli.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment